• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Anapapasa gizani?

Anapapasa gizani?

NA MWANDISHI WETU

RAIS William Ruto anaonekana kutapatapa kutafuta jibu la matatizo ya Wakenya huku shinikizo zikizidi kwamba atimize ahadi alizotoa kwa wapigakura wakati wa kampeni.

Japo anasisitiza kuwa ana mpango wa kutatua matatizo yanayokumba Wakenya, sera za serikali ya Kenya Kwanza zimekuwa zikiwaongezea raia mzigo wa gharama ya maisha, suala ambalo katika manifesto ya muungano wake wa Kenya Kwanza aliahidi kushughulikia kwa muda wa siku 100 baada ya kuingia mamlakani.

Badala ya kutangaza mipango thabiti ya kuimarisha uchumi, Rais Ruto amekuwa akilaumu serikali ya mtangulizi wake Uhuru Kenyatta mwaka mmoja tangu aingie mamlakani.

“Tuna mipango ya kurekebisha na kubadilisha uchumi kuanzia mashinani. Tumefanya uamuzi unaofaa. Wakati mwingine tumefanya maamuzi magumu mno na yenye uchungu ili kuepusha Kenya kutumbukia katika shimo la madeni na kuipa nchi yetu mwelekeo mpya,” Rais Ruto alisema kwenye hotuba yake katika maadhimisho ya Jamhuri Dei mnamo Desemba 12, 2023.

Gharama ya maisha imeendelea kupanda huku akianzisha aina mpya za ushuru na ada zinazopunguza mapato ya raia na kupuuza ushauri unaoweza kusaidia kuwaletea raia afueni.

Akiwa katika Kaunti ya Kisii mnamo Jumamosi, kiongozi wa nchi alisema hahitaji ushauri wowote wa kupunguza gharama ya maisha akisisitiza kwamba ana mpango wa kushughulikia matatizo yanayokumba raia.

“Hawa wangwana (viongozi) wamenipa mawaidha mengi. Lakini nataka kuwaambia kwamba nilipotafuta hii kazi (urais) nilikuwa na mpango,” alisema.

Ingawa Wakenya wanalia kulemewa na gharama ya maisha, rais alisema “hawana (raia) shida” na badala yake aliwanyooshea wanasiasa kidole cha lawama akidai kwamba ndio wanaochochea raia kukosa utulivu na kulalamika,

“Hawa raia hawana shida, ni sisi viongozi tunaozozana na kuzua vurugu,” alisema.

Rais Ruto alisema hana uwezo wa kupunguza bei ya mafuta ambayo imelaumiwa kwa kuongeza gharama ya maisha akilaumu kampuni za mafuta kimataifa kwa ongezeko la bei za bidhaa hiyo ulimwenguni.

“Kuna kazi ambayo rais anaweza kufanya na hayo mafuta sina njia ya kupunguza bei yake,” alisema.

Wadadisi wanasema kwamba matamshi ya Rais Ruto ya kuelezea kwa nini hajatimiza ahadi zake yamekosa kuridhisha Wakenya licha ya kuyarudia kila wakati.

“Ni kinaya kwa rais kusema kwamba hana uwezo wa kupunguza matatizo ilhali anatazamwa na raia kama kiongozi wao na ambaye serikali yake iliondoa ruzuku na kuongeza ushuru wa thamani (VAT). Kwa ufupi, anaepuka ahadi aliyowapa wapigakura ili asilaumiwe moja kwa moja,” asema mtaalamu wa masuala ya utawala na uchumi James Waki.

Aidha, japo aliahidi kuwa serikali yake ingeheshimu utawala wa sheria na kuhakikisha uhuru wa Mahakama, Rais Ruto amekuwa akitoa matamshi yanayochukuliwa kuwa tishio kwa uhuru huo.

Akiwa Baringo kuhudhuria mnada wa mbuzi wa Kimalel, Rais Ruto aliwalaumu Wakenya wanaowasilisha kesi kupinga ajenda yake ya afya kwa wote akisema wanafadhiliwa na wanaofaidika na ufisadi katika sekta hiyo.

Hii ilikuwa siku chache baada ya kuapa kuwa hakuna anayeweza kusitisha ushuru nyumba alioanzisha licha ya baadhi ya Wakenya kuupinga kortini na kupata agizo usitishwe kwa msingi kuwa unakiuka Katiba.

“Kuna hisia kwamba Rais anakiuka Katiba huku akidai anaheshimu sheria na badala yake kutumia vitisho kushinikiza ajenda zake,” asema Bw Waki.

Anataja Sheria ya Fedha ya 2023 ambapo kabla ya kupitishwa alionya wabunge ambao wangeipinga na baadaye baadhi ya vipengele vyake kikiwepo kile cha ushuru wa nyumba kuharamishwa na Mahakama na kisha akasisitiza haiendi popote.

“Kwa rais aliyeahidi utawala wa sheria, ingekuwa bora iwapo angeacha kuzungumzia masuala yaliyo mbele ya korti na kuacha mkondo wa sheria ufuatwe kikamilifu,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt David Gichuki.

  • Tags

You can share this post!

Uhuru ni kikwazo kwa maridhiano, adai Mudavadi

Pasta mwalikwa kwenye krusedi afurushwa kwa kuvalia suti...

T L