• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 1:20 PM
Uhuru ni kikwazo kwa maridhiano, adai Mudavadi

Uhuru ni kikwazo kwa maridhiano, adai Mudavadi

NA PIUS MAUNDU

KINARA wa Mawaziri, Musalia Mudavadi, sasa anamtaka Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta aunge mkono Ripoti ya Jopo la Kitaifa la Maridhiano (NADCO) huku utata ukiendelea kati ya Serikali na Upinzani kuhusu utekelezaji wa yaliyomo kwenye ripoti hiyo.

Bw Mudavadi alimshutumu Bw Kenyatta kwa kuwa kikwazo kwenye utekelezaji wa ripoti hiyo kupitia chama chake cha Jubilee.

Kumekuwa na madai kuwa Bw Kenyatta amekuwa akiwashawishi vinara wa upinzani wapinge ripoti ya Nadco.

 

Rais mstaafu Uhuru Kenyatta. PICHA | MAKTABA

Waziri wa zamani wa Ugatuzi, Eugene Wamalwa, na Kinara wa Narc Kenya, Martha Karua, tayari wamejitokeza na kupinga ripoti hiyo ya Nadco wakisema haigusii suala tata kuhusu jinsi ya kushushwa kwa gharama ya maisha miongoni mwa Wakenya.

Nadco inapendekeza kubuniwa kwa Afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani pamoja na kuweka rasmi wadhifa wa Kinara wa Mawaziri kwenye Katiba.

“Kwa nini sasa Uhuru Kenyatta na wenzake hawataki kuheshimu na kuunga yaliyoafikiwa na jopo la Nadco? Mchezo hapa ni gani?” akauliza Bw Mudavadi.

Bw Mudavadi mwenyewe aliunga mkono ripoti hiyo na kupigia debe utekelezaji wake akisema utachangia amani na maendeleo nchini.

Alikashifu upinzani kutokana na undumakuwili kuhusu matokeo ya mazungumzo hayo ilhali wao ndio walikuwa wakiyataka ili kusuluhisha masuala waliyoyaibua baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

“Waliitisha mazungumzo ya kuzima maandamano na kumekuwa na ripoti kuhusu masuala waliyoyaibua. Kwa nini sasa wanatoroka badala ya kuunga mkono nia ya kuwaleta watu pamoja,” akasema Bw Mudavadi.

Alikuwa akizungumza katika Shule ya Msingi ya Mukuyuni, Kaunti ya Makueni wakati wa sherehe ya kumkaribisha nyumbani Katibu katika Wizara ya Ugatuzi, Teresia Mbaika.

“Nawaomba Wakenya wote wakiwemo viongozi wa Ukambani kuheshimu yaliyoafikiwa kwenye ripoti ya mazungumzo,” akaongeza kinara huyo wa mawaziri.

Alikuwa ameandamana na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Felix Koskei, na mawaziri Moses Kuria (Utumishi wa Umma), Penninah Malonza (Jumuiya ya Afrika Mashariki) na viongozi wengine ambao waliitaka jamii ya Wakamba iunge mkono utawala wa Rais William Ruto.

“Uteuzi wa Bi Mbaika unaonyesha kuwa Rais anawaheshimu wanawake,” akasema Bw Mudavadi wakati wa sherehe hiyo iliyohudhuriwa pia na magavana Hillary Barchok (Bomet), Gideon Mung’aro (Kilifi) na Spika wa Bunge la Kaunti ya Kitui, Kinengo Katisya.

Sherehe hiyo iliongozwa na Askofu Paul Kariuki, ambaye ni Mkuu wa Dayosisi ya Kanisa Katoliki Makueni. Bi Mbaika alisema mchango ambao ulitolewa wakati wa hafla hiyo utatumiwa kujenga sehemu ya Kanisa Katoliki la Makuyuni.

Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse wa Maendeleo Chapchap alimshukuru Rais kwa uteuzi wa Bi Mbaika akisema kuwa ni fahari kwa kaunti licha ya eneo hilo kuunga mkono upinzani katika uchaguzi mkuu uliopita.

“Japo hatukumpa Rais kura za maana kutoka eneo hili, amewapa wake na waume wetu kazi za hadhi katika serikali yake,” akasema Bw Mutuse.

  • Tags

You can share this post!

Gachagua ataka Wakenya wampe Rais Ruto muda wa kuimarisha...

Anapapasa gizani?

T L