• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 5:04 PM
Azimio wamteua Kioni kuongoza timu ya ushauri wa kisheria

Azimio wamteua Kioni kuongoza timu ya ushauri wa kisheria

NA CHARLES WASONGA

MUUNGANO wa Azimio la Umoja-One Kenya umemteua Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni kuwa Mkuu wa kikosi cha kisheria na kiufundi katika mazungumzo ya maridhiano kati yake na mrengo wa Kenya Kwanza.

Hatua hiyo imeonekana kama inayolenga kuwaridhisha viongozi wa Azimio kutoka eneo la Mlima Kenya ambao duru zinasema walilalamika, chini kwa chini, kwa kutowakilishwa katika kamati ya mazungumzo.

Kwenye taarifa, kiongozi wa muungano huo Raila Odinga alitangaza kuwa sasa Bw Kioni na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka wataongoza mazungumzo hayo kwa niaba ya upinzani.

“Kalonzo ataongoza kikosi cha kuendesha mazungumzo ilhali mwenzetu Kioni kikosi cha kisheria na kiufundi,” Bw Odinga akasema.

“Tumewashauri wawakilishi wetu na kikosi chetu cha kiufundi wataenda katika mazungumzo hayo kwa moyo wa uwazi na bila masharti magumu,” Bw Odinga akaongeza.

Kiongozi huyo wa Azimio pia alisema kuwa masuala yao ambayo wangetaka yajadiliwe bado ni yale yale na hayajabadilika.

Miongoni mwa maswala hayo ni; gharama ya juu ya maisha, uteuzi wa makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi  na Mipaka (IEBC), kusitishwa kwa mwenendo wa Kenya Kwanza kuingilia vyama tanzu vya Azimio na kuadhibiwa kwa polisi waliowaua waandamanaji.

Bw Odinga pia alikubaliana na pendekezo la Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah kwamba mazungumzo hayo, ambayo yatasimamiwa na Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, yafanywe katika ukumbi wa Bomas of Kenya.

Aidha, kinara huyo wa Azimio alitoa hakikisho kwamba hawataisha maandamano wakati ambapo mazungumzo yatakuwa yakiendelea.

Bw Odinga alitoa wito kwa mrengo wa Kenya Kwanza kujibu wema huo kwa “kukoma kutoa matamshi ya kuchochea chuki za kisiasa katika mikutano yenu ya kisiasa.”

  • Tags

You can share this post!

Bei ya lishe ya mifugo kushuka

Ushoga: World Bank yauma miradi ya umma Uganda

T L