• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Barasa adai, Malala ni fuko wa ODM ndani ya Kenya Kwanza, ataka NEC ya UDA impige kalamu

Barasa adai, Malala ni fuko wa ODM ndani ya Kenya Kwanza, ataka NEC ya UDA impige kalamu

NA CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Kimilili Didmus Barasa ameitaka Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) kumsimamisha kazi Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho Cleophas Malala kwa madai ya kutumiwa na ODM kuvuruga muungano wa Kenya Kwanza.

Bw Barasa Jumatatu, Oktoba 9, 2023, alidai kuwa Bw Malala anatumiwa na chama hicho kinachoongozwa na Raila Odinga kuwachafulia jina Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi.

Mbunge huyo wa UDA aliendelea kudai kwamba Bw Malala amekuwa akichochea wananchi katika eneo la Magharibi mwa Kenya dhidi ya wawili hao akidai wamekosa kuwatetea kuajiriwa serikalini kwa watu kutoka eneo hilo.

“Niko na habari kwamba Malala anatumiwa na ODM kuwahujumu viongozi wetu wakuu kutoka Magharibi mwa Kenya; Wetang’ula na Mudavadi ili kutoa nafasi kwa ODM kunawiri 2027,” Bw Barasa akasema kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi.

Kulingana na Barasa, hatua ya Bw Malala kutaka wawili hao, na wabunge wengine wa Kenya Kwanza kutoka magharibi kutoa idadi ya watu ambao wameajiri na idadi ya miradi ya maendeleo walioleta ni sawa na kuharibia sifa serikali ya Rais William Ruto.

“Huyu ni mtu ambaye ametumwa na ODM kuvuruga muungano wa Kenya Kwanza katika eneo letu la magharibi mwa Kenya,” Bw Barasa akasema.

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa akihutubia wanahabari Jumatatu Oktoba 9, 2023 katika majengo ya Bunge, Nairobi ambapo ameitaka NEC ya UDA kumfuta kazi kwa madai ya kuwa kibaraka wa ODM. PICHA|CHARLES WASONGA

 

“Ikiwa NEC ya UDA haitamtoa tutaandamana hadi makao makuu ya chama chetu Hustler Centre na kufanya kile ambacho ODM kilimfanyia Magerer Lang’at,” Mbunge huyo akaongeza.

Bw Barasa alikuwa akirejelea tukio la Oktoba 30, 2014 ambapo wafuasi wa ODM walifurusha kwa nguvu aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa chama hicho Magerer Lang’at kutoka mkutano wa kundi la wabunge (PG) kwa tuhuma za kuwa fuko wa uliokuwa muungano wa Jubilee.

“Tutaandamana hadi katika jumba la Hustler Centre; Tutaelekea huko kwa wingi na kumfurusha kwa nguvu,” Bw Barasa akasema.

Wanahabari walipomtaka kutoa ithibati kuhusu madai dhidi ya Bw Malala, Mbunge huyo alidinda kufanya hivyo, akisema: “Kama Mbunge na kiongozi niko na njia nyingi za kupata habari za kuhusu mambo kama haya”.

Hadi wakati wa kuchapisha taarifa hii, juhudi za Taifa Leo Dijitali kumfikia Bw Malala kusaka kauli yake kuhusu suala hilo hazikuzaa matunda.

Katibu huyo Mkuu wa UDA hakujibu simu za mwandishi huyu wala jumbe fupi kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii wa WhatsApp.

 

  • Tags

You can share this post!

Mudavadi akemea viongozi wa Nyanza kwa ‘kukalia...

Ruto amsifu Uhuru kwa mara ya kwanza tangu aingie...

T L