• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Mudavadi akemea viongozi wa Nyanza kwa ‘kukalia fence’ kuhusu kumuunga Rais Ruto

Mudavadi akemea viongozi wa Nyanza kwa ‘kukalia fence’ kuhusu kumuunga Rais Ruto

Na SHABAN MAKOKHA

MKUU wa Mawaziri Musalia Mudavadi amewaambia viongozi wa Upinzani kutoka Luo Nyanza kukomesha tabia aliyoitaja kama undumakuwili.

Bw Mudavadi, aliyewahi kuwa makamu wa rais, amewataka viongozi hao watangaze msimamo wao kuhusu utayarifu wao wa kufanya kazi na Rais William Ruto.

Alitoa kauli hiyo baada ya magavana kutoka eneo hilo kumkaribisha Rais Ruto aliyefanya ziara ya siku nne eneo hilo kuzindua miradi ya maendeleo.

Awali, viongozi wa ODM, wakiwemo baadhi ya magavana, kutoka eneo hilo waliwakaripia baadhi ya wabunge wa ODM waliomtembelea Rais katika Ikulu ya Nairobi na kutangaza kuwa watashirikiana na serikali yake.

Rais alikita kambi eneo la Luo Nyanza, ambalo ni ngome ya kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga kuanzia Oktoba 6.

Bw Mudavadi pia aliwakosoa viongozi wa Nyanza kwa kuonyesha mapendeleo baada ya magavana wote kumkaribisha Rais kwa moyo mkunjufu. Alidai awali viongozi wa Upinzani kutoka eneo hilo waliwachochea viongozi wa ODM kutoka Magharibi mwa Kenya dhidi ya kumkaribisha Rais na kususia shughuli zake katika eneo hilo.

Bw Mudavadi alisema viongozi wa Nyanza wanaongozwa na nia mbaya ya kutaka Magharibi isifaidike kutokana na ustawi unaotekelezwa na serikali ya kitaifa.

“Rais amekuwa Nyanza ambako alipeleka mambo mazuri na akapokelewa vizuri na magavana wote kutoka eneo hilo. Wakati umetimu kwa wao kukoma kudhani kwamba ni wao pekee yao wanafaa kufaidi kwa serikali kuu,” akasema.

Rais Ruto alipozuru Kaunti ya Siaya alipokelewa na Gavana James Orengo. Alitoa Sh100 milioni kufadhili ujenzi wa Hospitali ya Ugenya Level 4. Mradi huo utatekelezwa na serikali kuu kwa ushirikiano na serikali ya Siaya ambayo itatoa Sh50 milioni.

Rais pia alisema kuwa serikali yake itashirikiana na serikali ya Siaya kuweka vifaa katika hospitali hiyo ujenzi wake utakapokamilika baada ya miezi minne.

Aidha, Dkt Ruto alitoa Sh5 milioni kwa Chuo cha Mafunzo ya Matibabu cha Ugenya na kiasi sawa na hicho cha fedha kwa Shule ya Msingi ya Inungo. Pia alitoa Sh3 milioni kwa Shule ya Msingi ya Urenga na Sh30 milioni kwa ujenzi wa kiwanda cha kutayarisha mchele, Kaunti ya Siaya.

  • Tags

You can share this post!

Ajabu ya hedhi za wanawake kuwa na njama ya kuchocheana

Barasa adai, Malala ni fuko wa ODM ndani ya Kenya Kwanza,...

T L