• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Biashara yanoga Maasai Mara uhamaji wa nyumbu ukibisha

Biashara yanoga Maasai Mara uhamaji wa nyumbu ukibisha

NA ROBERT KIPLAGAT

HOTELI, vyumba vya malazi na mahema ya malazi katika mbuga maarufu ya wanyama ya Maasai Mara yamelipiwa yote, watu wengi wanapongoja shughuli ya kipekee ya kuhama kwa nyumbu itakayofanyika baadaye mwezi huu wa Julai.

Wasimamizi wakuu katika maeneo hayo wanasema kuwa wamejitayarisha vilivyo kwa msimu huo wa aina yake, wakiongeza kuwa huenda wakalazimika kutafuta maeneo zaidi ya malazi kutokana na idadi kubwa ya wageni wanaotarajiwa.

Uhamaji wa nyumbu kutoka Mbuga ya Serengeti nchini Tanzania hadi katika Mbuga ya Maasai Mara nchini Kenya ni mojawapo ya matukio ya kipekee sana duniani.

Uhamaji huo ndio huwa mkubwa duniani, kwani huwa unahusisha zaidi ya wanyama milioni mbili. Nyumbu hao huwa wanavuka na kuingia Kenya kutoka Tanzania ili kutafuta malisho. Tukio hili huwa linaanza Julai na kuisha Oktoba.

Wamiliki wa hoteli na wadau wengine katika sekta ya utalii wanasema kuwa vyumba na nafasi zote za malazi zilizopo zishalipiwa. Mamia ya magari ya watalii yamekuwa yakiingia katika mbuga hiyo yakiwa yamewabeba watalii kutoka sehemu tofauti duniani kushuhudia tukio hilo.

Wamiliki hao wanapata faida nyingi, kwani watalii hupitia katika mikahawa hiyo.

Bw Nick Murero, ambaye ni meneja katika Kampuni ya Mahema ya Lilita, alisema kuwa asilimia 70 ya nafasi za malazi katika mahema hayo zimelipiwa tayari. Alisema kuwa kiwango hicho ni cha juu ikilinganishwa na miaka ya hapo nyuma.

“Biashara ni nzuri. Watu walianza kulipia nafasi za malazi miezi miwili iliyopita. Tuna watalii kutoka Ulaya, Asia na wa hapa nchini,” akasema Bw Murero.

Mfanyabiashara huyo pia amewarai Wakenya kutenga muda wao kutembelea vivutio vya watalii hapa nchini.

Wanawake wanajifaidi kwa kuuza shanga, wanazosema zinanunuliwa kwa wingi sana.

Kundi la wanawake wanaouza bidhaa za shanga na nyingine za urembeshaji katika Lango la Sekenani pia wanajipatia mapato mengi.

Bi Loomaretu Sironik na Bi Noltetian Kiu walisema kuwa biashara yao ilianza kuimarika mwezi mmoja uliopita. “Nilikuwa nikiuza bidhaa za Sh1,000 kwa siku. Kwa sasa, ninauza bidhaa za hadi Sh3,000 kwa siku. Biashara si mbaya,” akasema Bi Sironok.

Hata hivyo, wanaitaka serikali ya Kaunti ya Narok kuwaruhusu kuuza bidhaa zao katika hoteli zilizo ndani ya mbuga hiyo ili kuongeza mapato yao.

“Tunaitaka serikali ya kaunti hii angaa kutupa nafasi katika mikahawa ya malazi ili kujipa faida kutoka kwa watalii,” akasema Bi Sironik.

Kauli yake iliungwa mkono na Bi Kiu, aliyesisitiza kuwa baadhi ya mikahawa inafaa kuzuiwa kuendesha biashara ya kuuza shanga na vifaa vingine vya kitalii, na badala yake kuwaachia wanawake.

Shughuli za mwaka huu 2023 zitafanyika chini ya masharti mapya kulingana na Mpango wa Usimamizi wa Mbuga ya Maasai Mara, uliopitishwa miezi miwili iliyopita.

Serikali ya Kaunti ya Narok imeanzisha sheria mpya, baadhi zikiwa utoaji wa tiketi za saa 12 pekee, kinyume na mpango wa hapo awali ambapo tiketi hizo ziliruhusu mtalii kuvinjari kwa saa 24 baada ya mtu kuingia kwenye mbuga.

Kwenye barua kwa wadau wa utalii, Waziri wa Fedha wa Narok, Bw David Munget, alisema kuwa tiketi zitakuwa zikitolewa kutoka saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni.

Kulingana na barua hiyo iliyoandikwa mnamo Juni 26, 2023, wageni wote wanaoishi kwenye hoteli na mahema wanahitajika kulipa ada ya kuingia inayolingana na siku watakazokaa kwenye mbuga.

Wakati huo huo, wale watakaokaa nje ya mbuga watahitajika kulipa ada ya kila siku, kila wakati watakapoingia kwenye mbuga ili kupelekwa kuwatazama wanyama.

Kulingana na kanuni hizo, wale wanaoondoka mbugani wafanye hivyo kufikia saa nne asubuhi, huku wale wanaotumia ndege wawe kwenye kituo cha ndege kufikia wakati huo.

Afisa huyo wa Kaunti pia aliwaagiza wale wanaoendesha puto kusajili safari zote katika Idara ya Kukusanya Mapato ya Kaunti.

Maafisa hao walitoa hakikisho kwamba hakutakuwa na foleni ndefu kwani kampuni za kukusanyia mapato zitakuwa katika viingilio vyote.

  • Tags

You can share this post!

AMINI USIAMINI: Pacu ni samaki mwenye meno kama ya binadamu

Raila abadili mbinu za kukabili ‘udhalimu’ wa serikali

T L