• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Bunge lahalalisha Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo

Bunge lahalalisha Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo

NA CHARLES WASONGA

BUNGE limeidhinisha rasmi hoja ya kuhalalisha kuundwa kwa Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (NDC) kusaka suluhu kwa changamoto za kitaifa zilizochochea uhasama kati ya mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja-One Kenya.

Mazungumzo hayo kati ya wawakilishi wa mirengo hiyo miwili yatashughulikia masuala yaliyochangia mvutano kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2022 na mengine ambayo yameorodheshwa na mirengo hiyo miwili.

Hoja hiyo ambayo ilidhaminiwa na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah na mwenzake wa upande wa wachache Opiyo Wandayi, iliungwa mkono kwa kauli moja na wabunge wa Kenya Kwanza na wenzao wa Azimo.

Kamati hiyo ya Kitaifa ya Mazungumzo ina wanachama 10, watano kutoka kila mrengo, na inaongozwa na wenyeviti wenza Kimani Ichung’wah (mwakilishi wa Kenya Kwanza) na Kalonzo Musyoka (Azimio).

Kando na Ichung’wah, wanachama wengine wa upande wa Kenya Kwanza ni; kiongozi wa wengi katika seneti Aaron Cheruiyot, Gavana wa Embu Cecily Mbarire, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Omar Hassan na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Bungoma Catherine Wambilyanga.

Katika upande wa Azimio Bw Musyoka anawaongoza wafuatao: Kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa, Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi, Seneta Okong’o Omogeni na Mbunge wa Malindi Amina Mnyazi.

Aidha, wabunge waliidhinisha kuundwa kwa Kamati maalum za kiufundi, za wanachama wanne kutoka kila mrengo, zitakazotoa ushauri kwa wanachama wa kamati ya NDC kutoka kila upande.

Wanachama wa kamati ya kiufundi ya upande wa Kenya Kwanza ni; Muthoni Thiankolu, Linda Musumba, Nick Biketi, na Duncan Ojwang.

Nao wale wa mrengo wa Azimio ni pamoja na; Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni, Adams Oloo, Zein Abubakar na Isabel Githinji.

Akitetea hoja hiyo Bw Ichung’wah alibanisha kuwa ajenda ya ugavi wa mamlaka haitashughulikiwa katika mazungumzo bali yale masuala yanayoendeleza masilahi ya Wakenya moja kwa moja.

“Raila ameweka wazi kuwa hataki handisheki au ugavi wa mamlaka. Kwa hivyo, ningependa kuwahakikisha wabunge na Wakenya kwa ujumla kwamba suala hilo haliko katika ajenda ya mazungumzo hayo,” akasema Mbunge huyo wa Kikuyu.

Akaongeza: “Mazungumzo haya yanalenga kukita moyo wa uzingatiaji wa utawala wa kikatiba katika nchi yetu ili baada ya kila uchaguzi mkuu atakayeshinda anaruhusiwa kuongoza.”

Bw Ichung’wah alisema kuwa mazungumzo hayo pia yatawezesha upande wa walio wachache kutekeleza ipasavyo wajibu wao wa kufuatilia utendakazi wa serikali.

Kwa upande wake, Bw Wandayi alisema ni kwa manufaa ya kila mwananchi ikiwa amani itarejea nchini kufuatia kupatikana kwa mwafaka wa kisiasa na kuleta mazingira faafu ya kuvutia wawekezaji.

Bw Wandayi alisema mvutano kutokana na uchaguzi mkuu wa 2022 sharti ushughulikiwe ili Kenya iweze kusonga mbele kimaendeleo katika nyanja zote.

“Hakuna mwekezaji ana hiari kuwekeza pesa zake katika mazingira ya fujo na misukosuko. Kama viongozi wa mirengo ya serikali na upinzani sharti tuungane kubuni mazingira yatakayowezesha wawekezaji kuja humu nchini kutoa nafasi za ajira kwa watu wetu,” akasema mbunge huyo wa Ugunja.

Bw Wandayi alielezea matumaini kuwa mazungumzo hayo yatatoa mapendekezo bora kuhusu mageuzi katika mfumo wa uchaguzi kuwekwa kwa mfumo mzuri wa uteuzi wa Makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

“Tunataka uchaguzi huru na wa haki. Hii ndio maana tunataka kuwe na mfumo mzuri na kubalifu wa uteuzi wa makamishna wa IEBC. Kama Azimio tutashiriki katika mazungumzo hayo nia ya kuendeleza ajenda za Wakenya sio mambo ya nusu mkate mkate au robo mkate,” akasema Bw Wandayi.

  • Tags

You can share this post!

Urithi: Mjane atabasamu serikali ikimsaidia kunasua...

Mjakazi anayedaiwa kumuua afisa wa kaunti kuzuiliwa siku 14...

T L