• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:19 PM
Urithi: Mjane atabasamu serikali ikimsaidia kunasua ‘minofu’

Urithi: Mjane atabasamu serikali ikimsaidia kunasua ‘minofu’

NA SAMMY KIMATU

[email protected]

FAMILIA moja ambayo imekuwa ikiishi kwa uchochole bila kujua kuna mali iliyoachwa na mzee baada ya kuaga dunia, imepata afueni baada ya serikali kuingilia kati.

Aidha, familia hiyo imeruhusiwa kumiliki tena mali hiyo kutoka kwa jamaa ambaye amekuwa akikusanya malipo ya nyumba kwa njia ya ulaghai.

Mnamo Jumanne, serikali iliingilia kati kurejesha nyumba 19 zilizojengwa na marehemu, Bw Peter Mutangili aliyekuwa na umri wa miaka 73 katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kenya Wine katika Kaunti Ndogo ya Starehe.

Kamishna msaidizi wa South B, Bw Solomon Muranguri aliambia Taifa Leo kuwa Bi Catherine Mueni Peter na watoto wake watatu walitegemea misaada kutoka kwa wasamaria wema katika nyumba yao eneo la mashambani Wote, Kaunti ya Makueni ingawa mumewe alikuwa na mali Nairobi.

“Mjane huyo alitiwa unyongeni na mpwa wake aliyechukua mali ya mumewe kwa nguvu baada ya mume wake huyo kuaga dunia Aprili 4, 2020, baada ya hali ya kiafya kuzorota wakati wa janga la Covid-19,” msimamizi huyo alisema.

Mpwa huyo, kulingana na mwenyekiti wa Kenya Wine, Bw Boniface Mugeni Nyataru, Stephen Musyoki amekuwa akikusanya kodi kutoka kwa wapangaji wanaomiliki nyumba 19 za marehemu.

“Babake Bw Musyoki alifariki kisha mjombake ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa mtaa wa mabanda wa Kenya Wine, marehemu Mutangili alimwambia mpwa wake aje Nairobi na kuishi naye. Hivyo ndivyo alivyohusika katika sakata hii,” Bw Mugeni akasema.

Kulingana na rekodi kutoka kwa afisi ya Bw Muranguri, Bw Musyoki alikusanya kodi kutoka kwa nyumba 19 huku kila mpangaji akilipa Sh3,000 kila mwezi.

Kijipande cha gazeti chenye habari ya kijana kumjeruhi mke wa ami yake. PICHA | SAMMY KIMATU

Kwa muhtasari, Bw Musyoki alilaghai zaidi ya Sh3.8 milioni.

Kabla ya kuenda mitamboni, Bw Muranguri aliamuru Bw Musyoki aondoke hapo ndani ya siku tatu na kusema ni tishio kwa usalama.

Pia alitoa maagizo kwa Bi Catherine Mueni kuwa msimamizi pekee aliyeidhinishwa kisheria kama mrithi halali kusimamia mali ya marehemu mumewe.

“Kifungu cha 45 cha Sheria ya Urithi, kuingilia mali ya mtu ni makosa kisheria,” Bw Muranguri alisoma.

  • Tags

You can share this post!

Chania High yapokea Sh10 milioni kutoka kwa Rais

Bunge lahalalisha Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo

T L