• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Cherargei aisuta Mahakama kwa kuzima uteuzi wa CASs 50 na kusema watakata rufaa

Cherargei aisuta Mahakama kwa kuzima uteuzi wa CASs 50 na kusema watakata rufaa

NA CHARLES WASONGA

SENETA wa Nandi Samson Cheragei ameisuta Idara ya Mahakama kwa ‘utundu’ kufuatia hatua ya majaji wa Mahakama Kuu kuzima uteuzi wa Manaibu wa Mawaziri (CASs) 50.

Kulingana na majaji hao, Kanyi Kimondo, Hedwig Ongudi na Alnashir Visram, uteuzi wa CASs hao uliofanywa na Rais Wiliam Ruto mwezi wa Machi ulikiuka katiba na kwamba Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) haikuendesha shughuli za kushirikisha umma inavyopasa.

Lakini kupitia taarifa aliyotoa muda mfupi baada ya majaji hao kutoa uamuzi wao, Bw Cherargei aliapa kuwa serikali ya Kenya Kwanza itakata rufaa akisema “mahakama haikuzingatia uzito wa kesi hiyo.”

“Idara ya Mahakama imegeuka mtundu kwa kuamua kwamba hatua ya kubuniwa kwa nyadhifa za Mawaziri Wasaidizi ni kinyume cha Katiba. Lakini inasikitisha kuwa majaji wametoa uamuzi huo pasina kuzingatia umuhimu wa kesi hiyo. Katika mwaka huu wa kifedha wa 2023/2024 Idara ya Mahakama ilipokea Sh4 bilioni zaidi juu ya mgao wake wa kawaida. Lakini inaudhi kwamba bado kuna mrundiko wa kesi mahakamani, ufisadi na utepetevu katika mfumo wa utoaji haki katika Idara ya Mahakama,” Cherargei akasema.

“Tutakata rufaa dhidi ya uamuzi huu unaoenda kinyume na masilahi ya umma na misingi ya haki,” Seneta huyo ambaye ni wakili, akaeleza.

Majaji hao watatu walioketi katika mahakama ya Milimani, Nairobi, Julai 3, 2023, walisema kuwa serikali pia haikufuata kanuni zilizowekwa za kubuni afisi hizo.

  • Tags

You can share this post!

Waliohamia kambini kutoroka Al-Shabaab wamzomea kamishna

CASs wapokonywa minofu mdomoni

T L