• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:21 PM
Chirchir, Siror waagizwa kufika mbele ya Kamati ya Kawi kuelezea kiini cha stima kupotea

Chirchir, Siror waagizwa kufika mbele ya Kamati ya Kawi kuelezea kiini cha stima kupotea

NA CHARLES WASONGA

KAMATI ya Bunge la Kitaifa kuhusu Kawi imeita Waziri wa Kawi Davis Chirchir na Mkurugenzi Mkuu wa Kenya Power Joseph Siror kufika mbele ya wabunge kuelezea kiini cha kupotea kwa stima kote nchini mnamo Ijumaa na Jumamosi.

Waziri Chirchir na Mhandisi Siror wanatarajiwa kufika mbele ya wabunge kuelezea kiini cha kupotea kwa stima kote nchini baada ya Kamati ya Kawi kusema itawahoji wawili hao kuhusu tukio hilo ambalo pia liliathiri Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi ambao ni kitovu wa uchukuzi wa angani katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Mwenyekiti ameagiza kwamba tuite Waziri wa Kawi na Afisa Mkuu Mtendaji wa Kenya Power kufika mbele ya wanachama ili wawili hao waelezee kilichosababisha kupotea kwa umeme sehemu nyingi nchini, ikiwemo katika uwanja wa JKIA, na kutatiza wasafiri katika uwanja wenye shughuli nyingi,” ikasema taarifa iliyotolewa na Sekritariati ya Kamati hiyo Jumamosi asubuhi.

Kamati hiyo inaongozwa na Mbunge wa Mwala Vincent Musyoka, almaarufu, Kawaya.

Stima ilipotea katika sehemu Pwani, Nairobi, Nyanza, Mlima Kenya na maeneo ya Mashariki kuanzia Ijumaa jioni na kufikia Jumamosi.

Kwenye taarifa, Kenya Power ilisema kuwa hali hiyo ilisababishwa na hitilafu katika mitambo yake ya kusambaza stima sehemu mbalimbali nchini.

“Tunafanya kila tuwezalo kwa ushirikiano na wahusika wote ili kurejesha stima katika maeneo yote yaliyoathirika na hali hiyo ya kusikitisha na isiyokusudiwa,” Kenya Power ikasema.

Kufikia mwendo wa saa sita adhuhuri Jumamosi, stima ilikuwa imerejea katika maeneo kadhaa ya jiji la Nairobi isipokuwa maeneo machache. Baadhi ya wafanyabiashara katikati mwa jiji waliamua kutumia majenereta ya kuzalisha kawi mbadala.

  • Tags

You can share this post!

Vita baridi Mlimani kati ya Rigathi na Ndindi Nyoro

‘Blackout’ mara mbili kwa wamiliki wa baa...

T L