• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Davis Chirchir aorodheshwa kama Waziri mwenye utendakazi mbaya zaidi

Davis Chirchir aorodheshwa kama Waziri mwenye utendakazi mbaya zaidi

NA CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Kawi Davis Chirchir ameorodheshwa kama waziri mwenye utendakazi duni zaidi miongoni mwa Mawaziri wote 22 katika serikali ya Rais William Ruto.

Hii ni kulingana na matokeo ya utafiti ulioendeshwa na kampuni ya Trends and Insights for Africa (TIFA) yaliyotolewa rasmi Jumatano, Desemba 13, 2024.

Bw Chirchir ambaye amekuwa akielekezewa lawama na umma kutokana na kupandishwa kwa bei ya mafuta na visa vya kupotea ghafla kwa stima, aliandikisha utendakazi wa asimilia 19.

Katika safu hiyo ya chini kiutendakazi, pia waliorodheshwa Waziri wa Jinsia Aisha Jumwa (aliyewakilisha kiwango cha utendakazi cha asilimia 23) na Waziri wa Fedha Profesa Njoroge Ndung’u akiwa wa tatu kwa utendakaz wa chini kwa kupata asilimia 24.

Waziri wa Maji, Zacharia Njeru na mwenzake wa Ardhi Alice Wahome pia waliandikisha kiwango sawa cha asilimia 24.

Waziri wengine walioko kwenye orodha ya mawaziri 10 wenye utendakazi duni ni pamoja na; Florence Bore wa Leba  (asilimia 25 ), Rebecca Miano wa Biashara (asimilia 27), Moses Kuria wa Utumishi wa Umma (asilimia 27), Peninah Malonza wa Jumuiya ya Afrika Mashariki- EAC (asilimia 27), na  Simon Chelugui wa Ustawi wa Vyama vya Ushirika (asimilia 31).

Jumatatu, Desemba 11, Bw Chirchir alikabiliwa na wakati mgumu alipotakiwa kuelezea sababu ya kutokea kwa kisa cha tatu cha kupotea kwa kawi kote nchini siku iliyotangulia (Jumapili) mwendo wa saa mbili za usiku.

Tatizo hilo lililodumu kwa zaidi ya saa sita, piailiathiri Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).

Hii ni baada ya jenereta ya kuzalisha kawi ya stima ya ziada nyakati za dharura kufeli kufanyakazi.

Hicho kilikuwa ni kisa cha pili cha kupotea kwa stima kote nchini tangu Rais William Ruto alipoingia mamlakani Septemba 13, 2022.

Kando nayo, Wakenya wamekuwa wakilalamikia kupanda kwa bei ya mafuta ambayo sasa inauzwa Sh217.36 (petroli), Sh203.47 (dizeli) na Sh203.06 (mafuta taa).

Aidha, Waziri Chirchir amelaumiwa kuhusiana na mvutano kuhusu umiliki wa shehena ya dizeli ya thamani ya Sh17 bilioni iliyonaswa katika Bahari Hindi ikiletwa nchini.

Mfanyabiashara kwa jina Anne Njeri Njoroge alidai kuwa shehena hiyo ilikuwa mali yake.

Mvutano huo bado unachunguzwa na asasi husika za serikali pamoja na Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Kawi inayoongozwa na Mbunge wa Mwala, Vincent Musyoka, maarufu kama Kawaya.

Wakati huo huo, Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki bado amesalia kidedea kama Waziri mchapakazi zaidi katika serikali ya Rais Ruto.

Alisifiwa na asilimia 65 ya jumla ya watu 3,009 waliohojiwa katika utafiti huo uliofanywa kati ya Novemba 25, 2023 na Desemba 7, 2023.

Mahojiano yalifanywa kwa njia ya simu na kwa kutumia lugha za Kiswahili na Kiingereza.

Profesa Kindiki anafuatwa na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi (asilimia 62), Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu (asilimia 58), Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen na mwenzake wa Afya Susan Nakhumicha wamepata asilimia 57.

 

  • Tags

You can share this post!

Matamshi ya Gavana Kahiga kuhusu nguvu za umeme huenda...

MAONI: Wachuuzi katikati mwa jiji bado ni kero kwa wapita...

T L