• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Matamshi ya Gavana Kahiga kuhusu nguvu za umeme huenda yakamtia motoni?

Matamshi ya Gavana Kahiga kuhusu nguvu za umeme huenda yakamtia motoni?

NA SAMMY WAWERU

GAVANA wa Nyeri, Mwalimu Mutahi Kahiga anaonekana kujipata kwenye kikaangio moto kufuatia pendekezo lake kwa Rais William Ruto kumfuta kazi Waziri wa Kawi, Bw Davis Chirchir.

Akihutubu Jumanne, Desemba 12 katika Kaunti ya Nyeri wakati wa maadhimisho ya Jamhuri Dei 2023, Gavana Kahiga alielezea kutoridhishwa kwake na jinsi taifa limekuwa likishuhudia tatizo la nguvu za umeme kupotea kila wakati.

Matamshi yake yalichochewa na kisa cha Jumapili, Desemba 10 ambapo maeneo mengi nchini hayakuwa na stima.

Kwenye kauli ambayo huenda hakufahamu fika kuwa ingemtia matatani, Mwalimu Kahiga alimhimiza Rais Ruto kuwatimua ofisini wote wanaojaribu kuvuruga juhudi zake, hasa akimnyooshea kidole cha lawama Waziri wa Kawi Davis Chirchir.

“Kwanza tunaona kuna mawaziri wake wanarandaranda ovyoovyo, hawafanyi kazi. Juzi nimetoka ng’ambo, stima zilikuwa zimepotea (akimaanisha Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta – JKIA). Waziri kama huyo anayehusishwa afutwe kazi asubuhi, na waziri mwingine tutafutiwe,” Bw Kahiga akasema.

Gavana huyo alihoji, Nyeri pekee ina watu wachapakazi ambao wakipewa majukumu hayo watayatekeleza.

“Hapa Nyeri tuna wafanyakazi wazuri tuwapatie kazi…Lakini haiwezi kuwa watu wanazembea kazini…Rais anajitolea, anafanya kazi usiku na mchana. Rais wetu, saa kumi na mbili ameamka. Saa sita za usiku hajalala aking’ang’ana kutengeneza taifa hili.

“Lakini watu wengine wameonelea ni kana kwamba kuna mchezo pale, wanazembea stima zinapotea hapa, genereta tunaambiwa hiki, kesho ni hivi. Mimi nataka niseme hapa ikieleweka mchana peupe, kama wamezembea kazi, Kenya hii yetu ina wananchi milioni 50, Nyeri pekee tuna mawaziri wa kutosha. Tunataka tumwombe Rais, mtu asijaribu kuhujumu utendakazi wako kama mtu hafanyi kazi, nje,” akafafanua.

Mwalimu Kahiga sasa anaonekana kama kiongozi aliyekabwa koo na anahoji matamshi yake yalichukuliwa nje ya muktadha.

Jumatano, Desemba 13, alikanusha kauli zake mwenyewe kwamba alipendekeza kutimuliwa ofisini kwa Waziri Chirchir.

Aliashiria kujutia matamshi yake.

“Kwenye matamshi yangu ya Jamhuri Dei, ningependa kuweka wazi kwamba sikushinikiza Waziri Davis Chichir afutwe kazi kufuatia hitilafu ya nguvu za umeme iliyoshuhudiwa. Nilichosema ni kuwa, nilikuwa na Waziri JKIA stima zilipopotea. Nilisema alipiga simu kadhaa umeme urejeshwe. Nilichosema kitasalia; Suala la stima kupotea JKIA ni aibu ya kitaifa,” Gavana Kahiga akafafanua.

Kwenye taarifa yake, mwanasiasa huyo wa UDA anasema alimshauri kiongozi wa nchi kutimua Waziri anayehusishwa na masuala ya viwanja vya ndege.

“Isitoshe, nilisema Mawaziri wote wanaomuangusha Rais waonyeshwe mlango,” alielezea, akisifia jinsi ambavyo Rais William Ruto huamka alfajiri na mapema na kulala kama amechelewa.

Jumapili, Desemba 10 ambapo umeme ulipotea baadhi ya maeneo nchini, JKIA pia iliathirika jenereta zikikosa kusaidia, jambo ambalo liliibua maswali kuhusu utendakazi wa Wizara ya Uchukuzi, inayoongozwa na Kipchumba Murkomen.

Waziri Murkomen, hata hivyo, alizuru uwanja huo mkuu nchini.

Aidha, Waziri alihimiza Idara ya Polisi Nchini (NPS) kuanzisha uchunguzi, akidai kuna njama inayolenga kulemaza huduma za ndege Kenya.

Kisa cha Jumapili, umeme kupotea hakikuwa cha kwanza, ikizingatiwa awali na chini ya miezi mitatu stima zilikuwa zimepotea mara mbili zaidi.

Katika visa hivyo, JKIA iliathirika Bw Murkomen akitimua baadhi ya viongozi kutokana na aibu ya jenereta kutofanya kazi.

Hali kadhalika, alibuni kamati ya muda kubaini changamoto zinazokumba JKIA.

Na kufuatia tatizo la Jumapili, Waziri wa Kawi, Davis Chirchir aliambia taifa kwamba hitilafu iliyoshuhudiwa ilitokana na nguvu chache za umeme katika baadhi ya maeneo nchini, ikilinganishwa na kiwango cha uzalishaji.

  • Tags

You can share this post!

Wanasiasa Kisii wanaopepeta moto wa fujo kuona cha mtema...

Davis Chirchir aorodheshwa kama Waziri mwenye utendakazi...

T L