• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
DCI kutoka makao makuu wafika Mombasa kuchunguza kifo cha mfanyakazi wa benki

DCI kutoka makao makuu wafika Mombasa kuchunguza kifo cha mfanyakazi wa benki

NA FARHIYA HUSSEIN

MAAFISA wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kutoka makao makuu Nairobi wamefika jijini Mombasa ili kuanzisha uchunguzi wa kilichosababisha kifo cha kutatanisha cha Bw Oscar Owino, ambaye alikuwa mfanyakazi wa benki.

Mwili wa Owino ulipatikana katika ghorofa moja eneo la Nyali mwezi mmoja uliopita.

Hatua hiyo inajiri siku chache baada ya familia hiyo kumwandikia barua mkuu wa DCI Bw Mohamed Amin ikielezea kutoridhishwa kwao na jinsi maafisa wa polisi wa Nyali walivyoshughulikia kesi hiyo, wakati familia iliibua wasiwasi kuhusu kifo cha Owino.

Maafisa wa upelelezi waliofika Mombasa asubuhi ya Jumatano wanatarajiwa kuzuru maeneo mbalimbali ambapo Owino anashukiwa kufika dakika zake za mwisho kabla ya kuaga dunia.

Maeneo hayo ni pamoja na hoteli yenye shughuli nyingi na maarufu ya Maasai Beach ambayo inasemekana marehemu alitembelea usiku wa Agosti 14, 2023, pamoja na wenzake kwa vinywaji na sherehe ya siku ya kuzaliwa.

Maafisa hao pia wanatarajiwa kufika katika Jumba la Royal Apartments eneo la Nyali ambapo mwili wa marehemu ulipatikana.

Ni katika ghorofa hiyo ambapo familia katika barua yao kwa DCI ilibainisha wanashuku kifo tatanishi baada ya mashahidi kusema walimwona Owino akiwa na mwanamke mwingine aliyetambulika kama Bi Pheny Kisasati.

Bi Kisasati katika taarifa zake za awali kwa polisi alibainisha kuwa alimwacha marehemu akifurahia vinywaji kwenye roshani ya nyumba yake iliyoko orofa ya tano na akaenda kulala.

“Alitoa taarifa kwa polisi kwamba kwa pamoja walikuwa wamehudhuria sherehe katika hoteli ya Maasai Beach ambapo walikunywa vinywaji hadi usiku kabla ya kurudi nyumbani ambapo yeye alienda kulala, akimuacha Owino kwenye roshani akiburudika kwa vinywaji,” sehemu ya ripoti ya polisi inasema.

Katika taarifa yake kwa maafisa wa DCI, Bi Kisasati alisema kuwa Owino alichukua muda mrefu na alipoenda kufuatilia kilichokuwa kikiendelea hakumpata kwenye roshani.

Baadaye alishuka chini ya ghorofa na kumkuta mpenzi wake huyo akiwa tayari ameaga dunia na ndipo alipiga kelele kuamsha majirani.

Afisa wa uchunguzi ambaye jina lake limebanwa kwa sababu haruhusiwi kuzungumza na wanahabari, alisema ya kuwa taarifa wanazokusanya zitawasaidia kubaini kilichojiri.

Afisa huyo alieleza kuwa watahoji wale walionekana na marehemu ili kusaidia katika uchunguzi.

Faili ya uchunguzi wa mwanzo tayari imetumwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), Mombasa mnamo Septemba 12, 2023, ili hatua zichukuliwe.

Miongoni mwa masuala yaliyoangaziwa na familia ni pamoja na kunyimwa fursa ya kushuhudia matukio kwenye kamera ya CCTV na maelezo jinsi mwili wa marehemu, ikiwa kweli alianguka, haukuonyesha athari yoyote na hakuwa na mifupa iliyovunjika.

Ripoti ya uchunguzi wa maiti ambayo iko mikononi mwetu inasema kuwa Owino alifariki kutokana na mshtuko wa moyo na majeraha kwenye kifua yaliyosababisha kutoboka kwa mapafu.

Tume Huru ya Kuangalia Utendakazi wa Polisi (IPOA) pia imeandikia familia ya Owino na kuahidi kwamba ikiwa hitaji litatokea na umakini wao unahitajika, wataingilia kati suala hilo.

“Tuna imani kuwa barua yako ilitumwa kwa afisi inayofaa, DCI na watahakikisha hatua zinazofaa zinachukuliwa kama ilivyoombwa. Tafadhali tufahamishe ikiwa usaidizi wetu utahitajika,” barua ya IPOA iliyotiwa saini na Mkurugenzi Mtendaji Bw Hussein Aden ilisoma.

  • Tags

You can share this post!

Chiloba asema tuhuma dhidi yake ni ‘madai tu’

Kikosi spesheli kutumwa Tana River na Lamu

T L