• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 5:04 PM
Fahamu chimbuko la hekaya za ‘paka jini’ wa Pwani

Fahamu chimbuko la hekaya za ‘paka jini’ wa Pwani

NA JURGEN NAMBEKA

HABARI nyingi zimeenezwa tangu jadi kuwahusisha paka wanaopatikana maeneo ya Pwani na ushirikina, almaarufu paka jini.

Sifa hizi zimechangia paka wanaofugwa katika kaunti za Pwani, kukosa haki kwa kudhaniwa kuwa na uwezo wa kujigeuza kuwa viumbe wengine ikiwemo kina ‘Fatuma’ na ‘Zaituni’.

Milio inayosemekana si ya paka wa kawaida inayosikika usiku, jinsi wanavyokodolea watu macho hata wanapofukuzwa, wanavyokaa milangoni pa maduka kama walinzi, na uwezo wao kuingia chumbani kupitia vishimo vidogovidogo, ni miongoni mwa mambo ambayo hufanya waogopwe mno.

Wageni wanaotoka bara huogopa paka wanapofika Pwani na vilevile, baadhi ya wenyeji hufanya kila wawezalo ili kuhakikisha hakuna paka anayewakaribia makwao.

“Nimeshuhudia watu wengi ambao wakizuru eneo la Pwani, wanawaogopa paka na kuwadhania kuwa ni binadamu waliojigeuza paka. Mzaha huo huvuka mpaka na wanyama hawa wazuri huhangaishwa, kunyanyaswa na kuuawa,” asema Bi Nusrat Mohamed, mmoja wa wakazi wachache waliojitolea kuwaokoa paka wanaonyanyaswa mitaani.

 

Mmiliki wa kituo cha kuokoa paka wanaokabiliwa na matatizo cha PAW jijini Mombasa, Bi Nuzrat Mohamed. Huwatibu na kuwawezesha paka kuendelea na maisha yao. PICHA | JURGEN NAMBEKA

Bi Mohamed, ambaye ni mmiliki wa kituo cha PAW kinachositiri paka karibu 40 waliokosa makao Mombasa, anasema kuna imani potovu zinazoenezwa kwamba wanyama hao pia huwa na nguvu za kishirikina.

Kulingana naye, baadhi za imani hizo zilianza tu kama utani ila zikaenea hadi bara na kukita mizizi katika jamii.

“Katika sehemu za Likoni, tumewahi kuona paka wanaoishi bila sehemu za mwili kwa sababu ya mambo ya uchawi. Nimesikia wakisema, kwa mfano kuwa, jicho la paka hutumika kuona maisha ya usoni ya mtu,” anasema Bi Mohamed.

Alieleza kuwa, baadhi ya mambo ambayo watu huchukulia kuwa ya ajabu wanapoyashuhudia kumhusu paka huwa ni maumbile ya kawaida ya mnyama huyo wa kipekee.

Alitoa mfano wa milio ya paka ambayo hushtua baadhi ya watu usiku, akisema huwa ni wakati wa paka kujamiana. Milio hiyo inayofanana na ya watoto wachanga hufanya watu kudhani kuna majini ndani ya paka.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Mshirikishi wa Baraza kuu la Kiislamu (SUPKEM) eneo la Pwani, Bw Hamis Akhbar Mwaguzo.

“Watu huogopa milio bila kufahamu jinsi ambavyo paka hushiriki tendo la ndoa. Ukisikia milio, jua tu ni wakati wa madume kuonyesha ubabe,” akasema.

Hata hivyo, Bw Mwaguzo hakupuuza uwezo wa washirikina kutumia mnyama huyo kuendeleza mambo yao ya imani za giza.

Kulingana naye, sawa na jinsi wanyama wengine wanavyotumiwa vibaya, paka pia wanaweza kutumiwa kwa mambo kama vile utoaji kafara na tiba za kiasili.

“Watu wengi humtumia paka vibaya ndio maana wale wanaotoka maeneo mengine ya Kenya wakizuru eneo letu huwaogopa,” akasema.

Hata hivyo, alisema ni kawaida watu wanaoishi Pwani kupenda kufuga paka na hilo halifai kuchukuliwa kumaanisha kuwa wanafuga majini.

Alisema kuwa katika dini ya Kiislamu, paka ametajwa sana kwenye vitabu vitakatifu na sawa na wanyama wengine, hafai kunyanyaswa.

“Kuna watu wanaofuga hata simba, kwa njia iyo hiyo. Tunapaswa kumtunza paka kwa kumfundisha na si kwa kumdhania kuwa mnyama mbaya. Mtume wetu anatueleza kuwa paka ni mnyama wa kuzunguka zunguka nyumbani. Mtume anaeleza kuwa wanyama hawa tunapaswa kuishi nao kwa wema,” akasema Bw Mwaguzo.

Baina ya wakazi, hisia tofauti hutolewa kuhusu ‘paka jini’.

“Kulingana na mimi, hakuna majini katika paka, isipokuwa tu wale watu wanaotumia nguvu za kiganga,” akasema Bw Victor Owino, mkazi wa Mombasa.

Mkazi mwingine, Bw Simon Mwabonje, adai, “Kule kwetu Kilifi, babangu ashawahi kumpiga paka gongo. Siku iliyofuata, akaja mtu kulalama eti baba kampiga. Paka majini wapo ila tu kutambua yupi ni yupi ni vigumu.”

  • Tags

You can share this post!

Hospitali, daktari kumlipa mwanamke fidia ya Sh1.1 milioni...

AFC Leopards kupiga kambi Kakamega kujinoa kwa msimu mpya

T L