• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 6:37 PM
AFC Leopards kupiga kambi Kakamega kujinoa kwa msimu mpya

AFC Leopards kupiga kambi Kakamega kujinoa kwa msimu mpya

NA JOHN ASHIHUNDU

AFC Leopards wanatarajiwa kuondoka Nairobi mnamo Jumapili kuelekea mjimi Mumias, Kaunti ya Kakamega kwa kambi ya mazoezi ya wiki moja kujinoa kwa ajili ya msimu mpya wa 2023/2024 utakaoanza Agosti 26.

Akitangaza habari kuhusu safari hiyo, mwenyekiti wa klabu hiyo Dan Shikanda kadhalika alisema timu hiyo itachezea mechi zake katika uwanja wa Bukhungu, Kakamega hadi uwanja wa kitaifa wa Nyayo utakapokuwa tayari.

Kikosi hicho cha kocha Tom Juma kinaondoka baada ya kushiriki katika mechi kadhaa za kujipima nguvu jijini Nairobi.

Miongoni mwa wachezaji wapya walio kwenye kikosi cha Leopards kinachosafiri ni kiungo mshambuliaji Cliffton Miheso aliyewahi kuwachezea miaka saba iliyopita.

Mchezaji huyo wa kimataifa amejiunga na Ingwe wakati kuna madai kwamba huenda ikazuiliwa kusajili wachezaji wapya kufuatia kesi iliyowasilishwa mbele ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na aliyekuwa kocha wao, Patrick Aussems.

Miheso amekuwa akijianda na klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Kenya (FKF-PL) kwa wiki mbili mfululizo, huku Shikanda akisisitiza kwamba ni miongoni mwa watakaosajiliwa.

Baada ya kuchezea Ingwe hapo awali, Miheso alijiunga na Gor Mahia kwa muda mfupi kabla ya kunyakuliwa na Kenya Police msimu uliopita na kuwafungia mabaoa matano, lakini anatarajiwa kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji wa Ingwe iliyomaliza katika nafasi ya saba, msimu uliopita.

Baada ya kuagana na Leopards mnamo 2016 na kujiunga na Kā€™Ogalo na kuichezea kwa miaka miwili, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 aliyoyomea Afrika Kusini kuchezea Golden Arrows kabla ya kuondoka na kujiunga na Builcon FC ya Zambia na pia Clube Olimpico do Montijo ya Ureno.

Miheso aliwahi kutwaa tuzo ya Mfungaji Bora nchini msimu wa 2021/2022 baada ya kufunga mabao 15, moja mbele ya Derick Otanga wa KCB.

Wachezaji wengine wapya wanaojiandaa na Leopards wakisubiri kusajiliwa ni kipa Humphrey Katasi, Vincent Mahiga, Randy Bakari, Boniface Munyendo, Hassan Beja na Yassin Beja wote kutoka Nzoia FC.

Wengine ni Kevin Kimani zamani wa Mathare United na Brian Yakhama aliyesakatia FC Talanta msimu ulopita.

Leopards imepangiwa kuanza msimu mpya dhidi ya Talanta katika uwanja wa Bukhungu, Kakamega kwenye mechi inayotarajiwa kuvutia mashabiki wengi.

  • Tags

You can share this post!

Fahamu chimbuko la hekaya za ‘paka jini’ wa...

Shabana yasajili sita, wengine wakitarajiwa kuwasili

T L