• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Gachagua ataka Mama Ngina arudishie MauMau mashamba, akisema pia yeye ajumuishwe

Gachagua ataka Mama Ngina arudishie MauMau mashamba, akisema pia yeye ajumuishwe

Na SAMMY WAWERU

NAIBU wa Rais Rigathi Gachagwa ameitaka familia ya Rais mstaafu Hayati Mzee Jomo Kenyatta kurejeshea waliopigania uhuru wa Kenya, ndio MauMau, mashamba yao.

Kupitia video inayosambaa mitandaoni, Bw Gachagua akiskika kana kwamba anamjibu mke wa rais huyo wa kwanza, Mama Ngina Kenyatta, amesema familia hiyo haijachelewa kufanya haki kwa mashujaa wa ukombozi wa nchi.

Alhamisi, Mama Ngina ambaye ni mama wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, alitembelewa na Bi Muthoni Kirima mmoja wa kina mama walioshiriki vita vya MauMau ambapo nyanya huyo alimshukuru mke wa Mzee Jomo Kenyatta kwa kumlipia mkopo wa benki wa Sh4.7 milioni na pia kumnunulia nyumba.

“Nimefurahi sana kuona watu jana wakisema wanafikiria vile watasaidia watu wa MauMau. Hata kama hawajawasaidia kutoka 1963, hawajachelewa kwa sababu MauMau na watoto wao wako na shida,” Gachagua akasema mnamo Ijumaa.

Kulingana na naibu rais, hata ingawa hakufichua anaohoji wanakubaliana na kauli yake, wanachoomba ni walioshiriki vita vya MauMau na watoto wao wasaidiwe kwa njia inayofaa.

Alisema, mashamba yaliyonyakuliwa na Mzee Jomo baadhi yarejeshewe mashujaa wa ukombozi wa Kenya.

Mama Ngina Kenyatta. Picha /HISANI

Gachagua amekuwa akidai yeye ni mmoja wa watoto wa wapiganiaji uhuru wa taifa hili, na hata yeye angefurahia kushirikishwa kwenye mgao wa mashamba hayo.

“Yale mashamba yote walichukua ya MauMau waangalie hata kama ni nusu wapee watu wa MauMau na watoto wa MauMau nikiwemo. Ni hayo tu tunauliza. Hakuna shida. Hawajachelewa,” alisema.

Gachagua alielezea kushangazwa kwake na familia ya Kenyatta, kuanzia 1963 Kenya ilipopata uhuru wa kujitawala kutoka kwa Mbeberu haijawahi wazia kusaidia MauMau.

“Kwa sababu wenyewe ndio walichukua mashamba yote ya MauMau, swara ndio wanakula huko na kutembea  huko hakuna kazi inaendelea kwa hayo mashamba. MauMau na watoto wao wanazikwa kwa makaburi ya umma.

“Tunauliza hao tu kama wamepata hiyo roho Mungu amewagusa kuonea watu wa MauMau na watoto wao huruma, wazingatie kuwagawia sehemu ya mashamba waliyonyakua. Hayo mashamba ni makubwa sana,” alisema.

Bw Gachagua aidha alisema yuko tayari kuhamasisha MauMau na watoto wao, kupata mgao huo endapo familia ya Mzee Jomo itaitikia.

Alisema atasaidia katika shughuli ya upataji hatimiliki ya ardhi, akisema miaka 60 baada ya Kenya kupata uhuru ni muda mrefu mashujaa walioshiriki MauMau kusubiri kufurahia matunda ya bidii zao.

  • Tags

You can share this post!

Miili ya watoto 2 kati ya 3 iliyofukuliwa Shakahola

Joho: Nikipata nafuu nitaongoza maandamano ya Azimio 

T L