• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Joho: Nikipata nafuu nitaongoza maandamano ya Azimio 

Joho: Nikipata nafuu nitaongoza maandamano ya Azimio 

Na SAMMY WAWERU

ALIYEKUWA Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho amefichua sababu za kutoonekana kwenye maandamano ya Azimio, hata ingawa yalisitishwa kwa muda kuruhusu mazungumzo kati ya upinzani na serikali. 

Bw Joho alisema Ijumaa, alifanyiwa upasuaji ndiposa hakushiriki maandamano yaliyoongozwa na kinara wa Azimio Raila Odinga na mikutano ya umma.

Gavana huyo wa zamani hata hivyo hakufichua tatizo analopitia kiafya.

“Nikijiskia niko vizuri kiafya, kikamilifu, Raila atakuwa nyuma yangu kwa maandamano. Mimi nitakuwa mbele halafu yeye nyuma. Lazima ijulikane hivyo,” Joho alisema.

Alisema hayo baada ya kuungana na waumini wa dini ya Kiislamu kusali, katika Uwanja wa Shule ya Fahari, Mombasa.

Jamii ya Kiislamu Ijumaa iliadhimisha Sikukuu ya Idd-Ul-Fitr 2023, baada ya mfungo wa Ramadhan.

“Watu ambao wanaota ati sijui watu wamestaafu sijui wamefanya nini, mimi ni ODM na ODM ni mimi, mimi ni Raila na Raila ni mimi. Watu wajue hayo tu. Tutakutana hapa mashinani…Tukanyagane hapa hapa,” Joho aliambia wanahabari.

Alisema kwa sasa anaendelea kupata nafuu, na pindi atakapopona hatakuwa na budi ila kujiunga na vuguvugu la Azimio kuongoza maandamano kushikiniza serikali kushusha gharama ya maisha na kutimiza matakwa ya upinzani.

Alilalamikia gharama ya juu ya maisha, akisema mwaka huu mambo yamekuwa mabaya zaidi chini ya serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto.

Hali ya afya ndiyo ilinizuia kushiriki maandamano, Joho akasema, akisisitiza kuwa anaunga asilimia 100 kwa 100 mikakati ya Azimio la Umoja.

Bw Odinga ndiye kiongozi wa ODM, naibu wake akiwa Joho.

“Hali ya afya hainiruhusu kuwa katika msukumano…Usiulize ati kwa nini maji ya bahari yana chumvi; Maji ya bahari yana chumvi kwa sababu ni maji ya bahari. Nasikitika rohoni kwa sababu sipo katikati ya maandamano.”

Bw Joho anaaminika kuwa mmoja wa wandani wa karibu wa Odinga, na kukosekana kwake katika maandamano ya Azimio kulikuwa kunaibua maswali kuhusu msimamo wake.

Odinga ametishia kwamba upinzani utarejelea maandamano wiki ijayo, kwa kile anadai kama serikali ya Dkt Ruto kuonekana kutokuwa na haja ya mazungumzo kutatua malalamishi ya Azimio.

Tayari pande zote mbili zimezindua wawakilishi saba kila moja, kushiriki katika mazungumzo.

  • Tags

You can share this post!

Gachagua ataka Mama Ngina arudishie MauMau mashamba,...

Kiraitu Murungi arejea serikalini

T L