• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Ghasia zatatiza biashara nchini

Ghasia zatatiza biashara nchini

NA WAANDISHI WETU

SHUGHULI za biashara zilitatizwa sehemu mbalimbali za nchi kutwa nzima Jumatano kutokana na maandamano yaliyoongozwa na wanasiasa wa upinzani, kupinga sera za utawala wa Kenya Kwanza na kulalamikia gharama ya juu ya maisha.

Maandamano ya Jumatano yalikuwa ya pili baada ya yale ya Ijumaa iliyopita, yaliyofanyika siku ya Saba Saba.

Maandamano yalikolezwa pia na mgomo kwenye sekta ya uchukuzi wa umma ambapo madereva walikuwa wakipinga mafunzo mapya serikali inataka wafanyishwe.

Shughuli za kawaida zilisimama Nairobi, Mombasa, Kilifi, Nyeri, Kisii, Nyamira, Homa Bay, Kisumu na Migori huku wafuasi wa upinzani wakikabiliana na polisi.

Hali ilikuwa vivyo hivyo, Machakos Mjini, Mlolongo, Emali, Kirinyaga, Kakamega, Busia, Kitengela miongoni mwa maeneo mengine.

Haya yalifanyika huku Muungano wa Wafanyabiashara kwenye Sekta ya Kibinafsi (KEPSA) ulitangaza kuwa Kenya imekuwa ikipoteza jumla ya Sh3 bilioni kila siku ya maandamano.

Jiji la Nairobi jana liligeuka mahame huku biashara nyingi zikifungwa nao makundi ya vijana katika mitaa mbalimbali yakikabiliana na polisi.

Uwanja wa Kamukunji ambako Kinara wa Upinzani Raila Odinga alikuwa aandae mkutano wake wa kisiasa nao uligeuka kituo cha makabiliano kati ya polisi na makundi ya vijana.

Mtaani Kibera, polisi walilazimika kutumia vitoa machozi kutawanya makundi ya vijana waliokuwa wamejikusanya kuanza safari ya kuingia katikati mwa jiji.

Aidha, uharibifu mkubwa ulitekelezwa kwenye barabara kuu ya Nairobi Expressway na wahuni japo haikufahamika iwapo walikuwa wafuasi wa upinzani. Katika maeneo ya Pwani, biashara ziliathirika kutokana na upungufu wa watu waliofika mijini.

Mjini Mombasa, watu kadha walikamatwa walipojaribu kuziba barabara mtaani Bakarani mwendo wa saa mbili asubuhi. Katikati mwa mji, waandamanaji wakiongozwa na mashirika ya kijamii na baadhi ya viongozi wa ODM walifyatuliwa vitoa machozi punde walipoanza maandamano yao.

Mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko alisema, watu 18 walikamatwa na polisi. Biashara katika Kaunti ya Taita Taveta ziliathirika, hasa kutokana na mgomo wa waendeshaji malori.

Miji iliyopakana na barabara kuu ya kuelekea Nairobi ilipata pigo kwani biashara nyingi hutegemea wahudumu wa magari na wasafiri wa masafa marefu.

Jijini Kisumu, waandamanaji walipambana vikali na polisi siku nzima hata baada ya Bw Odinga kutangaza kuwa alikuwa amefuta mkutano wa Kamukunji. Mtu mmoja alipigwa risasi huku wengine wawili wakijeruhiwa wakati wa maandamano hayo.

Hakukuwa na shughuli zozote za kibiashara jijini humo huku makundi ya vijana nayo yakiwapiga mawe polisi hasa katika maeneo ya Kondele na Jua Kali.

Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyongo, Naibu wake Mathew Owili na wabunge Joshua Oron (Kisumu ya Kati) na Onyang’o K’Oyoo (Muhoroni) walitimka mbio mguu niponye baada ya polisi kuyatibua maandamano waliyokuwa wakiyaongoza.

Katika Kaunti jirani ya Homa Bay, watu 15 walikamatwa kwenye maandamano yaliyoongozwa na mbunge wa Kasipul Ong’ondo Were.

Sawa na maeneo mengine, kulikuwa na fujo kati ya vijana na polisi na hakukuwa na shughuli zozote za kibiashara na uchukuzi.

Kufuatia maandamano makubwa ya wiki iliyopita yaliyowapata walinda usalama bila kujipanga vyema, jana wakuu wa polisi Kisii walikuwa ange na waliwazuia waandamanaji kuingia katikati mwa mji.

Biashara nyingi zilifungwa huku vijana nao wakifunga Barabara ya Kisii-Kilgoris. Kaunti ya Nyamira haikuachwa nje wakati huu huku waandamanaji wakifunga Barabara Kuu ya Kisii-Nyamira kutoka Getare hadi Kebirigo.

Nakuru ambayo inachukuliwa kuwa ngome ya utawala wa Kenya Kwanza pia ilishuhudia maandamano katika mitaa ya of Mazembe, Pondamali na Shaabab.

Wafanyabishara mtaani Shaabab walilazimika kufunga biashara zao baada ya vijana waliokuwa na hasira kuanza kuwapora na kutekeleza uharibifu wakati wa makabiliano na polisi.

“Walinipora bidhaa zangu kama unga wa ngano na ule wa ugali na bidhaa nyingine. Nimepata hasara kubwa ambayo sijui jinsi nitakavyoifidia,” akasema mfanyabiashara wa Nakuru John Kamau.

Kaunti miji ya Nanyuki, Nyeri, Nyahururu, Kirinyaga, Murang’a, Tharaka-Nithi na Meru, maandamano ya Wana Azimio japo yalikuwa machache, yalipigwa jeki na mgomo wa wahudumu wa matatu ambao ulitatiza kabisa shughuli za uchukuzi.

“Nimekuwa dereva kwa miaka 10 ila natakiwa kupata mafunzo tena. Wale wanaostahili kuandaa mafunzo hayo ni wanaoendesha magari vibaya,” akasema dereva Evans Mwangi.

Ingawa hivyo, wafuasi wa upinzani Murang’a, Kirinyaga na Nyahururu walijitokeza, baadhi wakinyakwa na polisi.

Machakos, Mlolongo, Emali na Kitengela pia hakukuwa na shughuli zozote za kibiashara kwa kuwa raia walijibwaga barabarani kulalamikia uchumi mgumu na sera dhalimu walizosema zinapendekeza waongezewe ushuru.

Ripoti za Cecil Odongo, Wycliffe Nyaberi, Valentine Obara, Stanley Ngotho, Mercy Koskei, Eric Matara, Ruth Mbula, James Murimi, Gitonga Marete, George Munene, Mwangi Ndirangu, Alex Njeru, Shaban Makokha, Lucy Mkanyika, Sammy Kimatu na Benson Matheka

  • Tags

You can share this post!

Polisi atapika baada ya kunusa vidole vya mshukiwa wa bangi

Nikivuta bangi vibarua vya shambani ni mboga kwangu –...

T L