• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Hatimaye wanahabari waruhusiwa kushuhudia operesheni ya Shakahola

Hatimaye wanahabari waruhusiwa kushuhudia operesheni ya Shakahola

NA ALEX KALAMA

WIKI chache tu baada ya serikali kupitia kwa agizo la Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki kuzuia wanahabari pamoja na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kuingia katika msitu wa Shakahola, hatimaye serikali imesema itaruhusu wanahabari kuingia katika msitu huo ili kuangazia yanayojiri.

Maafisa wanaendeleza operesheni ya kuwatafuta manusura wa imani potovu waliosalia na kufukua makaburi kuondoa miili ya wahanga ndani ya chaka hilo la Shakahola.

Akizungumza na wanahabari mnamo Jumanne wakati wakuanzisha awamu ya pili ya ufukuaji wa makaburi, Prof Kindiki amesema kila siku maafisa wa usalama wanaoendeleza operesheni hiyo wataruhusu wanahabari wawili pekee kuingia katika msitu huo ili kushuhudia operesheni hiyo na kuangazia yanayojiri.

“Hapo awali tulikuwa tumezuia wanahabari kuingia baada ya kutangaza kuwa “eneo la uhalifu” lakini sasa tutaruhusu muingie ila mtakuwa mnaingia wachache kwa sababu hatuna kitu tunaficha. Kila kitu kinachofanyika lazima tukiweke wazi. Hatuoni sababu ya kuficha… hata tupate miili mingapi tutaweka wazi,” amesema waziri Kindiki.

Vilevile waziri huyo amesema serikali imetoa ruhusa  pia kwa watetezi wa haki za kibinadamu kuingia katika msitu huo ili kufuatilia jinsi shughuli hiyo inavyoendeshwa.

“Pia vilevile tumetoa nafasi moja kwa watetezi wa haki za kibinadamu kutoka mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na nafasi nyingine moja kwa watetezi wa haki kutoka shirika la kiserikali,” akasema.

Haya yamejiri wiki chache tu baada ya  waziri huyo kutoa amri ya kutoruhusu mtu yeyote ambaye si afisa wa polisi kuingia katika msitu huo kutokana hatua yake ya kutangaza eneo hilo kuwa “eneo la uhalifu”.

Ni hatua ambayo ilifanya Baraza la Vyombo vya Habari nchini (MCK) kukashifu vikali kitendo hicho likisema huo ni ukiukaji wa haki za uhuru wa vyombo vya habari.

  • Tags

You can share this post!

KWPL yapamba moto mechi za msimu zikikaribia kukamilika

Miili 21 yafukuliwa idadi ya walioangamia Shakahola...

T L