• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Hofu eneo la Mlima Kenya watoto wa kiume wakiua wazazi ili kurithi mali

Hofu eneo la Mlima Kenya watoto wa kiume wakiua wazazi ili kurithi mali

NA MWANGI MUIRURI

WAZAZI wengi eneo la Mlima Kenya wanaishi kwa hofu ya kuangamizwa na watoto wao wa kiume, kufuatia njama zinazochochewa na urithi wa mali.

Katika hali hiyo, wazazi wengi haswa walio na vijana waliozama katika ulevi na mihadarati hawawezi kuthubutu kuweka hatimiliki za mashamba na nyumba katika boma, ama stakabadhi zingine muhimu za umiliki.

“Tuko kwa shida kubwa sana kama eneo kwa kuwa watoto wa kiume wanageuka kuwa wanyama wa kuwala wazazi wao wakisukumana na mali,” asema Mzee Joseph Kaguthi.

Bw Kaguthi alisema kwamba “Tulikofika kwa sasa ni kumuomba Maulana awape watoto busara ya kuwa na utulivu wazazi waage kifo cha Mungu na mali watapata tu”.

“Mila zetu zinawahamasisha watoto watie bidii wajitafutie mali yao ili katika urithi wazidishiwe. Lakini ilivyo kwa sasa ni njama za uzembe na maangamizi,” akasema.

Aliongeza kuwa “Wengi wa watoto hao hata wakishadhulumu wazazi ili wapate mali, wanaishia kuimaliza katika mtandao wa anasa na kuishia kuwa masikini”.

Mwenyekiti wa Jamii ya Agikuyu Bw Wachira Kiago alisema kwamba “hali ilivyo kwa sasa ni hatari kwa wazazi walio na mali kwa kuwa shetani wa ukatili amefikia nafsi za watoto”.

Alisema kwamba mikakati ya uhamasisho itazinduliwa eneo hilo ili kueneza injili ya bidii ya kujitafutia mali bila kulalia ya wazazi mlango wazi.

“Tutatafuta ushirikiano na wataalamu wa sheria za urithi kuwahamasisha wazazi jinsi ya kuchora wosia mapema ili kujiondolea hatari ya kusukumwa kwa kaburi ili mali itwaliwe,” akasema Bw Kiago.

 

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Ngoi hodari wa nyimbo

Makahaba Tana River watangaza nyongeza ya bei ya huduma za...

T L