• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Ngoi hodari wa nyimbo

Ngoi hodari wa nyimbo

NA PATRICK KILAVUKA

LUGHA ni njia ya mawasiliano. Inaweza kuwasilisha ujumbe, ushauri na kufahamisha vyema kupitia mzungumzaji. Mnenaji aliye na ufasaha huwa mvuto kwa msikilizi au hadhira.

Kwa upande mwingine, ngoi anayeongoza nyimbo anaweza kuwa kivutio kwa hadhira kutokana na jinsi anavyotumia uelewa wa wimbo kufikisha ujumbe kutokana na wimbo uwe wa kijadi au kileo.

Ngoi Angela Njambi,11, mwanafunzi wa gredi ya sita katika shule ya Moi Force Academy, Nairobi na aliye mwana wa pili katika familia ya Bw Peterson Ndwiga na Bi Felicity Kawira amekuwa mweledi na kivutio kwa wengi.

Aliweza kuumudu wimbo wa Kimaasai na kuukumbatia vilivyo hadi akafikisha shule yake katika mashindano ya Tamasha za Muziki za kitaifa, Kisumu na kuibuka wa tatu bora, 2022.

Kabla ya hapa, alikuwa ameongoza kikundi chake kutamalaki mashindano ya Kaunti ndogo ya Kamukunji na ya kanda ya Nairobi na kuibuka namba wani na ameshikilia uzi huo wa kuutetea ubingwa wao wa Kanda ya Nairobi kwa mara ya pili mtawalia.

Aliongoza kikosi chake katika wimbo wa lugha wa Kimaasai Nanyorrai katika Daraja ya 278.Ngoi Angela anasema anatambua uwezo wa kipaji chake kuwa mzizi wa urithi kwani mzazi wake ni mwimbaji wa nyimbo za injili na hushiriki katika uimbaji.

Angela anahusudu uimbaji kama ada. Utambuzi wa kipawa chake ulionekana pale ambapo mwalimu wake Lerionka Tupunya Sunkuli alikuwa anasaka kiongozi wa nyimbo kwa tamasha za mwaka jana.

Na kwa vile kipaji hakingefichika, kwa sababu kilikuwa kimekolea ndani yake, alimjaribu kupitia sauti, ukakamavu na ujasiri na mwisho wa siku, akabaini wazi kwamba anaweza kuongoza.

“Mashindano yalikuwa yamekaribia na wakati nilitaka ngoi, aliafiki matakwa ya kuongoza wimbo huo uliotajwa kwani, ni wimbo unaohitaji kiongozi mchangamfu, jasiri, sauti ya nyororo na mkakamavu,” anasema mkufunzi Tupunya.

Aliongeza kuwa, alichukua wiki moja kuiva na kuongoza wimbo hadi ngazi ya kitaifa.

Kupitia kushiriki mashindano ya muziki, kiongozi huyu anasema kuwa kumemchochea kujua lugha na hata kuimarisha uelewa wake katika masomo ya Kiswahili, Kiingereza na muziki.

bali na kuenzi uongozi wa nyimbo, anazamia somo la Sayansi kwa sababu angependa kusomea taaluma ya udaktari.

Jambi anasema ingawa mwaka jana yeye na kikosi chake waliibuka mabingwa wa kaunti ndogo ya Kamukunji, kinyang’anyiro hicho ndicho kilikuwa na ushindani mkali zaidi.

Hata hivyo, anasisitiza kwamba wameanza vyema mashinani kwa kuibuka washindi katika kaunti ndogo ya Kamukunji na ya kanda ya Nairobi, 2023.

Yeye huputisha muda wake wa ziada kwa kujifunza kupika vyakula mbalimbali.

Ushauri wake ni kwamba, ukiwa umejaliwa kipawa cha kuongoza nyimbo, usiwe na uwoga bali kuwa jasiri katika kutenda.

Isitoshe, kuwa na mtazamo chanya wa kulenga upeo wa jambo ili uwe kilelezo.

 

  • Tags

You can share this post!

Gavana ataka bustani ya Mama Ngina sasa isimamiwe na kaunti

Hofu eneo la Mlima Kenya watoto wa kiume wakiua wazazi ili...

T L