• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
Makahaba Tana River watangaza nyongeza ya bei ya huduma za ngono

Makahaba Tana River watangaza nyongeza ya bei ya huduma za ngono

NA STEPHEN ODUOR

MAKAHABA katika Kaunti ya Tana River wametoa notisi ya kuongeza bei ya huduma wanazotoa kwa kile wanataja kama “kuchangiwa na hali ngumu ya uchumi wa nchi”.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, ina maana kuwa wanaosaka huduma za ngono hawatakuwa na budi ila kufukua mfuko zaidi kugharamia starehe.

Akizungumza kwa njia ya simu, kiongozi wa kundi hilo eneobunge la Tana Delta, Janet Simon amesema kuwa kuanzia mwezi ujao, Agosti 2023 wataongeza bei ya ngono kwa asilimia kumi, kwani pesa walizokuwa wakitoza haziwezi kamwe kukimu mahitaji yao kama hapo awali.

“Bei ya mipira (kondomu) imepanda, sawa na mahitaji mengine ya kimsingi kama vile chakula na maji. Wamiliki wa madanguro pia wanapandisha bei ya vyumba, sasa nasi inatubidi kupandisha,”aliambia Taifa Leo Dijitali.

Janet anaelezea kuwa hali inazidi kuwa ngumu, na hivyo kuwataka wateja kuelewa na kukubali hali halisi.

Anasema, ili kuhakikisha kuwa biashara hiyo inafana na kila mtu anaridhika, bei ya ngono haitapungua Sh500.

“Sote tunasaka riziki na ikiwa unataka nikufurahishe, huna jingine ila nawe pia unifurahishe. Maelewano ya chini sana yasipungue Sh500, na tutawachunguza wenzetu kuhakikisha tunazungumza lugha moja,”alisema.

Mjini Hola, Anne Sharry, ambaye ni mweka hazina wa kundi hilo anasema kuwa wangali wanajadiliana kuhusu suala hilo, kwa kile anahoji “ipo sababu ya kuongeza bei”’.

Anaeleza kuwa gharama ya maisha mjini Hola imepanda, huku wamiliki wa nyumba wakiongeza kodi kuchao.

“Ukitoka mtaani na Sh1, 000 haikutoshi, inabidi ujinyime sana ndipo utimize mahitaji ya nyumbani na ya kazi pia,” alisema.

Miongoni mwa masuala anabainisha kuwa kikundi hicho kinafikiria, ni kuongeza huduma kwa wateja ili kulandana na ongezeko la bei ile.

“Wengi wetu tunafanya huduma hizi nyumbani kwa wateja wetu na wakati mwingine kwa nyumba zetu, basi hapo tunatafakari kuongeza kukanda kati ya majukumu mengine kulingana na malipo ya yule mteja,” alisema.

Pia makahaba hao wanawazia kutoka katika madanguro na kutumia nyumba zao ili kupunguza gharama au kujadiliana na wenye madanguro kushukisha bei ya vyumba.

Hili, wanasema kuwa ni kwa manufaa ya mteja, kwani pia wanazingatia usalama.

“Huwa tunapima maradhi ya zinaa mara kwa mara, hususan Ukimwi, kwa sababu ndio hofu kubwa ya makahaba,” Sharry alieleza, akisema vifaa vya kupima pia ni gharama ambayo mteja hataepuka kuibeba.

Bi Sharry anaeleza kuwa baadhi ya makahaba hujipata wakitibu magonjwa kadha wa kadha ya zinaa, ambayo huwagharimu pesa nyingi mno.

Hata hivyo, baadhi ya wateja wao wameridhia wazo hilo, wakisema kuwa hakika gharama ya maisha imepanda na lilikuwa suala la muda tu kabla yote haya kujitokeza.

“Itabidi tuzoee, wao wana msaada kwetu nasi ni wahitaji tu kama wao, sasa tufanyeje kama si kuwapiga jeki tu. Ikitushinda itabidi tutafute mbinu mbadala basi,” alisema Silas Arik.

 

  • Tags

You can share this post!

Hofu eneo la Mlima Kenya watoto wa kiume wakiua wazazi ili...

Kamanda Francis Kooli: Afisa tajiri wa utu na moyo...

T L