• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
IEBC yakaidi mahakama

IEBC yakaidi mahakama

Na LEONARD ONYANGO

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) jana Jumanne ilisitisha usajili wa wapigakura ambao umekuwa ukifanyika kitaifa licha ya mahakama kuitaka kuuendelea na usajili hadi wiki ijayo.

Tume hiyo ilishikilia kuwa haina fedha za kuongeza siku za usajili wa wapigakura hadi Novemba 9 ilivyoagiza korti.

Mahakama Kuu ya Eldoret, Jumatatu, iliagiza IEBC kuendelea na usajili wa wapigakura hadi kesi iliyowasilishwa na mpigakura, Bw Patrick Cherono, itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Tume hiyo ililenga kusajili wapigakura wapya milioni 6 kote nchini, lakini ilifanikiwa kuandikisha wapigakura wapya milioni 1 pekee.

Bw Cherono aliambia mahakama kuwa, IEBC haifai kusitisha usajili wa wapigakura kwa sababu haijaafikia lengo lake la kusajili wapigakura wapya milioni 6.

Naibu mwenyekiti wa IEBC, Juliana Cherera jana alikosoa mahakama kwa kuagiza tume hiyo kuendelea kusajili wapigakura bila kutoa mwongozo kuhusu jinsi itapata fedha za ziada.

“Inaonekana mahakama ilitoa agizo hilo bila kujua kwamba IEBC inakabiliwa na upungufu mkubwa wa pesa,” akasema.

Jumatatu, kamishna Francis Wanderi alisema atakutana na makamishna wenzake kujadili pendekezo la kutaka wanafunzi wa vyuoni waongezewe muda wa kujisajili kuwa wapigakura.

Bw Wanderi ambaye alikuwa akizungumza katika Chuo Kikuu cha Kabianga, alisema wanafunzi wanastahili kupewa muda zaidi wa kujisajili.

Chama cha ODM, wiki iliyopita, kiitaka IEBC kuongeza muda wa kusajili wapiga kura wapya kwa siku 60 zaidi.

Shughuli ya usajili wa wapiga kura kwa wingi iling’oa nanga mnamo Oktoba 4, 2021 katika vituo vya usajili 27,241 na Vituo vya Huduma 52 kote nchini.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, wiki iliyopita, alisema tume hiyo haitaongeza muda kwa shughuli ya usajili wa wapigakura wapya kwa wingi kutokana na ukosefu wa hela.

Bw Chebukati alisema tume ilikuwa imeomba Sh4 bilioni kwa ajili ya usajili wa wapigakura wapya lakini ikatengewa na bunge Sh1.2 bilioni tu.

“Baada ya Novemba 2 (jana) hatutaweza kuongeza muda wa usajili. Tume ina uwezo wa kusajili wapiga kura wapya kwa siku 30,” akasema Bw Chebukati.

Kulingana na Bw Chebukati, tume pia inahitaji 1.3 bilioni zaidi kukagua daftari la wapigakura na kuondoa majina ya waliokufa na watu ambao taarifa zao zina dosari.

IEBC pia inalenga kusajili Wakenya wanaoishi katika mataifa ya Sudan Kusini, Amerika, Uingereza, Canada, Qatar, Miliki za Uarabuni (UAE), Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na Afrika Kusini.

IEBC imeshikilia kuwa, inahitaji jumla ya Sh40.9 bilioni kuiwezesha kujiandaa vyema kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.

Kulingana na Bw Chebukati, IEBC imepewa Sh36.5 bilioni na inahitaji Sh4.4 bilioni zaidi.

Wabunge wametilia shaka bajeti hiyo ya IEBC huku wakisema ni kubwa mno.

IEBC inasema kuwa Sh5.9 bilioni zitatumika kununua karatasi za uchaguzi; na kila karatasi itagharimu Sh35. Tume hiyo inalenga kutumia Sh5.3 bilioni katika vifaa na mitambo ya kielektroniki kutambua wapigakura, kupeperusha matokeo.

Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ujao yanakumbwa na msukosuko kutokana na mvutano kuhusiana na kandarasi ya karatasi za kura.

Bodi ya Kutatua Mizozo ya Kandarasi za Umma (PPRB) wiki iliyopita ilifutilia mbali kandarasi ya ununuzi wa karatasi za kura iliyokuwa imetolewa kwa kampuni ya Inform P Lykos Holdings ya Ugiriki.

Mnamo Septemba, bodi ya PPRB pia ilifutilia mbali kandarasi ya kununua vifaa ya kielektroniki (KIEMS) lakini uamuzi huo baadaye ulibatilishwa na Mahakama Kuu ambayo iliruhusu IEBC kuendelea na mchakato wa kuagiza vifaa hivyo.

Waziri pamoja na mmoja wa makamishna wa IEBC wametajwa kuwa miongoni mwa watu wanaotatiza kandarasi hizo kwa ajili ya masilahi yao ya kibinafsi.

You can share this post!

Serikali yatangaza likizo fupi

Uhuru ahimiza viongozi kukabili mabadiliko ya tabianchi

T L