• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Uhuru ahimiza viongozi kukabili mabadiliko ya tabianchi

Uhuru ahimiza viongozi kukabili mabadiliko ya tabianchi

Na MARY WAMBUI

RAIS Uhuru Kenyatta ametoa wito kwa viongozi wote ulimwenguni kushirikiana ili kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Akihutubia mkutano wa ukaguzi wa hali ya hewa (COP26), jijini Glasgow, Scotland, Rais alisema majanga ya mafuriko na ukame yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa yanasababisha maafa na mazao duni ulimwenguni.

Alisema wakati umefika ambapo nchi zote ulimwenguni zinafaa kuungana ili kupambana na athari hizo.

“Tunapasa kuweka mikakati ya kupambana na athari za majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa. Tukijipanga dhidi ya ukame na mafuriko, tutalinda vizazi vijavyo,” akasema Rais Kenyatta.

Alisema Kenya imejiandaa kupambana na majanga kama hayo kwa kuteua kamiti itakayosafisha maji, kupanda mti na kuhakikisha misitu imelindwa.

Hali hiyo ni kuhakikisha kuwa mazingira ya nchi yamelindwa na kusaidia Kenya kufikia lengo lake la asilimia 100 ya matumizi ya nishati iliyoboreshwa ifikapo 2030.

Rais pia alitoa wito kwa kampuni zinazotoa kaboni duniani kutoa ahadi ya kupunguza uchafuzi huo.

“Nchi zinazoendelea zimeahidiwa dola bilioni 100 kwa mwaka lakini bado hazijafikishwa. Tunaomba ahadi kama hizo zitimizwe.”

Alisema kila mmoja anapasa kuwa jasiri na kuwa na umoja ili kutatua athari zinazosababishwa na madabiliko ya hali ya hewa.

You can share this post!

IEBC yakaidi mahakama

Ronaldo aokoa Manchester United kinywani mwa Atalanta...

T L