• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 6:50 AM
Jaa la taka lasakama watoto wa Mukuru

Jaa la taka lasakama watoto wa Mukuru

NA SAMMY KIMATU

SERIKALI imeamuru wachafuzi wa mazingira wanaodaiwa kuvamia eneo la Mlima kuendesha biashara zisizo na leseni mkabala wa barabara ya Likoni katika kaunti ndogo ya Starehe kuondoka mara moja.

Aidha, malori yanayosafirisha mchanga na kumwaga katika eneo hilo yalipigwa marufuku kuanzia Jumatano.

Akiongea na washikadau wa mazingira, naibu kamishna wa kaunti ndogo ya Starehe Bw John Kisang alisema agizo hilo litatekelezwa mara moja huku akiongeza kwamba maafisa wa polisi watapeana huduma ya usalama.

Bw Kisang aliongea wakati aliongoza mkutano wa kutafuta suluhu ya kero ya moshi na uvundo. Hafla hiyo ilifanyika katika ukumbi wa Mukuru Promotion Centre (MPC) katika tarafa ya South B.

Aidha, kituo cha MPC, ambacho kinaendesha shule tatu maeneo ya Mukuru, kinalalamika kwamba masomo na kazi huvurugwa kutokana na moshi unaosababishwa na wafanyabiashara wakichoma bidhaa katika eneo la Mlima.

MPC wanalalamika kwamba wanafunzi katika Shule ya Msingi ya St Bakhita, Vocational Skills Centre na Shule ya Upili ya St Michael wanapitia katika hali ngumu sana.

“Watu huchoma taka yakiwemo magurudumu, karatasi za plastiki na aina nyingine za plastiki kama vile chupa. Zaidi ya watoto 1,800 wameathirika,” Mshirikishi wa Masuala ya Elimu MPC Bi Lucia Njogu akaambia Taifa Leo.

Walioathirika zaidi ni wanafunzi na walimu katika kituo cha St Michael kwa sababu shule hiyo imepakana na eneo lingine kando ya mto Ngong ambalo hutumiwa kuchoma plastiki.

Kwa upande wa pili, shule hiyo imeangaliana na eneo la kisa kwa wakati huu.

MPC kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu Mtawa Mary Killeen, imethibitisha ni tatizo kubwa kwa watoto na walimu kupumua wakati mwingine kwani moshi mweusi hufunika shule hizo.

La kutamausha, MPC ilisema mtoto mmoja aliye na matatizio ya mtindio wa ubongo (Cerebral Palsy) alifariki kutokana na kushindwa kupumua baada ya moshi kumzidia.

“Ndege wala nyama hubeba mabaki ya minofu kutoka kwa jaa la taka na kuyaleta kwenye uga wa shule ambapo watoto huchezea. Nyama hizo na mifupa nayo imechangia ongezeko la panya shuleni ambao wanatupatia hasara kubwa kwa uharibifu wa mali,” Mtawa Killeen akasema.

Naye Mwakilishi wa Waislamu alisema kila Ijumaa, wakati wa swala ya jamaa wanakuwa na waumini zaidi ya 1,500 na wao hulazimika kufunga madirisha ndiposa wajiokoe kutoka kwa moshi na uvundo kutoka kwenye dampo hilo.

Mwakilishi wa Waislamu akieleza jinsi kero ya taka inavyotatiza shughuli za ibada ikiwemo swala ya Ijumaa. PICHA | SAMMY KIMATU

Vilevile, kampuni zaidi ya 10 zilitoa malalamiko katika mkutano huo huku Taifa Leo ikibaini kwamba baadhi zimelazimika kuhama kutoka eneo hilo kukwepa kero ya uchafuzi wa mazingira.

Waliohudhuria mkutano huo walikubaliana kwamba eneo hilo litazungukwa na ua na pia lilindwe na polisi.

“Nimeamuru kamati iliyoundwa kuwa ikinilelea ripoti kila baada ya wiki mbili kuhusu maendeleo, kumbusho na changamoto zilizopo kufuatia haya,” Bw Kisang akaambia Taifa Leo.

Hatimaye, aliangiza kamati hiyo itafute mwenye ardhi hiyo na ikiwa haina mmliki halisi, akasema serikali itatwaa shamba hilo.

“Ni lazima nijue mwenye shamba ili ndiposa serikali imsaidie kupata ardhi yake kama alikuwa ametishiwa na wanyakuzi. Pili, ikiwa hatutapata mwenye ardhi, bila shaka, shamba hili litatwaliwa na kuwa mali ya serikali,” Bw Kisang asema.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Rais Ruto aongoza Wakenya katika Maombi ya Kitaifa vinara...

Magonjwa ya kisonono, kaswende yalemea vijana nchini...

T L