• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 5:56 PM
Rais Ruto aongoza Wakenya katika Maombi ya Kitaifa vinara wa upinzani wakikwepa

Rais Ruto aongoza Wakenya katika Maombi ya Kitaifa vinara wa upinzani wakikwepa

JUSTUS OCHIENG Na KALUME KAZUNGU

RAIS William Samoei Ruto na Naibu wake, Rigathi Gachagua Jumatano wameongoza Wakenya katika awamu ya 20 ya Maombi ya Kitaifa katika hoteli ya kifahari ya Safari Park jijini Nairobi.

Rais Ruto amekumbusha Wakenya namna alivyomuomba msamaha mtangulizi wake, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta wakati wa Maombi ya Kitaifa ya mwaka 2022.

“Ninanyenyekea kwa Mwenyezi Mungu kwa kusaidia nchi yetu kukabiliana na vikwazo vinavyohujumu maendeleo na amani,” amesema Rais Ruto akihutubu Jumatano.

Vinara wa upinzani (Azimio), Raila Amollo Odinga, Kalonzo Musyoka, na Martha Karua walikwepa kwani hawakuonekana popote.

Jumanne, vinara hao wa mrengo wa Azimio la Umoja One Kenya Alliance tayari walikuwa wameeleza nia yao ya kukosa kushiriki maombi hayo ya kitaifa, japo waliwaruhusu wabunge wao kuhudhuria hafla hiyo kwa hiari yao.

Mamia ya viongozi, ikiwemo wabunge waliojumuisha wachache kutoka mrengo wa upinzani, maseneta, wabunge wawakilishi wa kaunti mbalimbali, viongozi wa kidini na wageni wengine waalikwa walianza kufika hotelini humo mapema kuanzia saa kumi na mbili alfajiri.

Mbunge Mwakilishi wa Wanawake, Kaunti ya Nairobi, Bi Esther Passaris (ODM) ni miongoni mwa viongozi wa mrengo wa upinzani waliohudhuria maombi hayo ya Jumatano asubuhi.

Awali, Bi Passaris alieleza matumaini yake kwamba kinara wa Azimio Bw Raila Odinga atabadili msimamo wake na kuguswa moyoni kuhudhuria maombi hayo ya kitaifa.

“Haya maombi ya kitaifa ya asubuhi ya leo yanahusu msamaha. Ninatarajia kusikia jumbe za upatanisho kutoka kwa viongozi. Natumai kiongozi wetu wa upinzani amebadili nia na kwamba angalau ahudhurie maombi haya. Yeye mara nyingi namfahamu kuwa mtu wa kutafuta njia ya upatanisho licha ya mambo mengi mabaya ambayo ametendewa,” akasema Bi Passsaris.

Mwenyekiti wa Tume ya Uwiano na Utanamano wa Kitaifa (NCIC), Dkt Samuel Kobia amesema tume hiyo ilifanya juu chini kumfikia Bw Odinga kwa matumaini kwamba angebadili nia yake na kuhuduria Maombi ya Kitaifa.

“Ni masikitiko kwamba Bw Odinga alicukua uamuzi wa kutohudhuria maombi haya ya kitaifa asubuhi ya leo. Hata hivyo nilifurahi aliposema wafuasi wengine wa upinzani, hasa bungeni wanaweza kuuduria maombi haya ya kitaifa,” akasema Dkt Kobia.

Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula ambaye pia ni patroni mwenza wa maombi hayo ya kitaifa alitangaza kuwa bunge liliamua kuelekeza fikra zake katika maendeleo na ufanisi wa siku za usoni.

Bw Wetang’ula alisisitiza kuwa maombi ya kitaifa ni miongoni mwa hafla muhimu kwa bunge na kwamba wabunge wako na mpango wa kunakili hafla hiyo kwenye ratiba za shughuli za Bunge.

“Tutazingatia kwamba hafla ya Maombi ya Kitaifa iwe na tarehe maalum kwenye kalenda kwamba kila Alhamisi ya mwisho wa mwezi Mei kila mwaka itambuliwe kuwa siku yetu ya hafla ya Maombi ya Kitaifa,” akasema Bw Wetang’ula.

Hafla hiyo ya Maombi ya Kitaifa ilifaa kuandaliwa juma lililopita lakini ikaahirishwa kwani Rais Ruto alikuwa yuko nje ya nchi.

  • Tags

You can share this post!

Waziri Soipan Tuya apongezwa kwa kuomba kwa Kiswahili...

Jaa la taka lasakama watoto wa Mukuru

T L