• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
Utafunaji miraa na michanganyiko ya ‘chewing gum’ husababisha kansa – Wataalamu

Utafunaji miraa na michanganyiko ya ‘chewing gum’ husababisha kansa – Wataalamu

NA KALUME KAZUNGU

IWAPO wewe ni mtafunaji miraa na muguka na unapenda kuchanganya na ‘chewing gum’, tambuu na kuvuta tumbaku, basi umeonywa dhidi ya kuendeleza tabia hiyo, wataalamu wakihusisha uraibu huo na maradhi ya kansa.

Wakizungumza katika kongamano la kuelimisha umma kuhusu kansa eneo la Mkunguni kisiwani Lamu, wahudumu wa afya, wakiwemo madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wa sekta ya matibabu, walieleza hofu kuhusiana na ongezeko la ulaji miraa na muguka pamoja na mchanganyiko mwingi wa vitafunio, hali ambayo waliitaja kuhatarisha afya ya watumiaji.

Katika kongamano hilo, wahudumu hao wa afya walifichua kisa kimoja kilichopatikana hivi majuzi cha mgonjwa wa kansa ya ulimi, wakieleza kuwa baada ya kumkagua waling’amua kwamba mwathiriwa alikuwa na historia ndefu ya kutafuna miraa, muguka, tambuu, ‘chewing gum’ na vinginevyo.

Mkurugenzi wa Afya, Kaunti ya Lamu, Dkt Abubakar Baasba, alieleza haja ya wakazi na Wakenya kwa ujumla kutunza afya zao, ikiwemo kuhakikisha miili yao, meno na mdomo wanaiweka safi ili kuepuka kuugua saratani mbalimbali.

Dkt Baasba alitaja uraibu wa kuvuta sigara, kutafuna miraa na muguka kwa kuchanganya na ‘chewing gum’, tambuu, tumbaku na ulevi kupindukia bila kuzingatia afya ya mwili kuwa miongoni mwa changizo cha waraibu kuugua kansa, hasa ile ya kichwa, shingo, ulimi, koo na matumbo.

Takwimu kutoka kwa Global Cancer Observatory (Globocan 2020) zinaashiria kuwa visa vya kansa ya shingo na kichwa vinajumuisha asilimia 4.6 kati ya visa vya kansa aina zote vilivyogunduliwa Kenya.

Asilimia hiyo inatajwa kuchangiwa na hali ya maisha ya waja, ikiwemo uvutaji sigara na kunywa pombe kupindukia.

“Hatujasema kwamba utafunaji miraa na muguka basi ni kisababishi tosha cha kansa. Ila kulingana na tafiti zetu kama wataalamu wa afya, ni bayana kwamba punde mtumiaji anapochanganya miraa, muguka, kuvuta sigara,tumbaku,tambuu na kubugia pombe bila kujali afya yake ya mwili, basi anajiweka kwenye hatari ya kupata kansa za koo, ulimi, tumbo, shingo na aina nyinginezo za saratani zinazolingana. Hivi majuzi hapa Lamu tulipata kijana akiugua kansa ya ulimi. Historia yake tulipoichunguza tukapa amekuwa akitafuna miraa, muguka, tambuu kwa kutumia vichanganyo vingine miaka mingi,” akasema Dkt Baasba.

Mtaalamu huyo wa afya aidha aliwashauri wakazi kubuni tabia ya kutembelea vituo vya afya mara kwa mara kukaguliwa viungo vyao vya mwili, hasa meno, koo, matiti, korodani, masikio na mengineyo ili kupiga vita maradhi ya kansa mapema.

“Hapa Lamu tayari tumepata visa kumi vya watu kuugua kansa mbalimbali, ikiwemo ulimi, matiti, korodani (kwa wanaume), kansa ya mlango wa uzazi (kwa wanawake) na nyinginezo. Hii inamaanisha eneo hili liko kwenye hatari ya wakazi kuugua kansa. Wengi hapa wamedharau mfuatilizio wa afya yao hospitalini. Ninawasihi muwe na hiyo tabia. Tembelea kituo cha afya mara kwa mara kupima kansa na kukaguliwa ili gonjwa hilo likibainika mapema ushughulikiwe badala ya kuacha hadi kansa ifikie awamu ya nne, ambapo inakuwa vigumu mgonjwa kupona,” akasema Bw Dkt Baasba.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Kaunti ya Lamu, Dkt Mbarak Bahjaj alisema kutokana na mzigo wa wagonjwa wa kansa Lamu kila mara kupewa rufaa ya matibabu kaunti ya Mombasa, ambapo inakuwa ghali kwao, serikali ya kaunti iko mbioni kuanzisha kituo cha ukaguzi, matibabu na uuguzi wa saratani eneo hilo.

Alisema tayari Sh50 milioni zimetengwa kuanzisha mradi huo huku akikadiria kima cha Sh200 milioni zinazohitajika kukamilisha na kufungua rasmi kituo hicho.

“Tunakubali kabisa kwamba Lamu tuko na changamoto ya kukithiri kwa visa vya kansa miongoni mwa wakazi. Karibu kila mwaka hatukosi visa vinavyobainishwa 10 vya watu kuugua saratani aina mbalimbali eneo hili. Tayari tumepeleka visa 10 vya watu kuugua kansa hapa Lamu katika hospitali ya Coast General huko Mombasa kwani hapa hatuna kitengo chochote cha kushughulikia wagonjwa wa kansa. Tumetenga Sh50 milioni kuanzisha kitengo hicho ili kupunguza gharama kwa familia za wagonjwa wa kansa kutafuta matibabu maeneo ya mbali,” akasema Dkt Bahjaj.

Kauli yake iliungwa mkono na Muuguzi Mkuu wa Wagonjwa wa Kansa kwenye hospitali kuu ya rufaa ya kaunti ya Lamu-King Fahd, Bi Anne Nkirote, ambaye alisisitiza haja ya kitengo cha matibabhu ya kansa kujengwa Lamu haraka ili kushughulikia wagonjwa hao.

“Kusema kweli ni tatizo tunapopata wagonjwa wa kansa kwani hatuwezi kuwauguza inavyostahili isipokuwa kuwapa rufaa nje ya Lamu. Iwapo kituo kama hicho kitabuniwa hapa basi ninaamini kitapunguzia gharama kwa familia nyingi za waathiriwa wa kansa,” akasema Bi Nkirote.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yaonya wakuu shuleni dhidi ya kuongeza karo

Jinsi Mwangaza alivyoangusha kibomu cha video kilichofanya...

T L