• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 3:24 PM
Kaunti kuvuna Ripoti ya Kamati ya Mazungumzo ikipendekeza mgao wake usipungue asilimia 20

Kaunti kuvuna Ripoti ya Kamati ya Mazungumzo ikipendekeza mgao wake usipungue asilimia 20

NA SAMMY WAWERU

SERIKALI za Ugatuzi ni kati ya asasi zinazotarajiwa kuvuna pakubwa kupitia Ripoti ya Kamati ya Mazungumzo (NADCO), iliyotolewa Jumamosi, Novemba 25, 2023.

Ripoti hiyo ya pamoja, iliyowasilishwa na wenyevikiti, Kimani Ichungwah (Kenya Kwanza) na Kalonzo Musyoka (Azimio la Umoja), miongoni mwa wanachama wengine, kamati hiyo inapendekeza mgao wa serikali ya kitaifa kwa kwa kaunti usipungue asilimia 20.

Kwa sasa, serikali kuu huzipa serikali za ugatuzi asilimia 15 ya mapato yake.

“NADCO inapendekeza Bunge lifanye marekebisho ya Katiba ili kuwezesha usawa wa ugavi wa raslimali, Serikali za Kaunti ziwe zinapokea asilimia isiyopungua 20 kwa mapato yote yanayouksanywa na Serikali ya Kitaifa, kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 15,” inasema Ripoti ya Kamati hiyo.

NADCO ilibuniwa kufuatia kupanda kwa joto la kisiasa nchini kati ya mrengo wa upinzani (Azimio) na serikali ya Kenya Kwanza), ili kupatanisha pande zote mbili.

Kati ya Machi na Julai 2023, taifa lilishuhudia maandamano yaliyosababisha maafa ya watu, uharibifu wa mali na biashara.

Ripoti ya NADCO pia inapendekeza kudumishwa kwa Fedha zinazotengewa Kuboresha Maeneobunge (NG-CDF), mgao wa National Government Affirmative Action Fund (NGAAF), na ule unaotengewa maseneta.

Madiwani (MCAs), pia, huenda wakavuna kutokana na mapendekezo ya ripoti hiyo, NADCO ikitaka wadi kutengewa fedha zitakazokabidhiwa wabunge wawakilishi wa wadi kufanya maendeleo.

Wakenya wakitarajia kuwa Ripoti ya Kamati hiyo ingewaletea afueni kupunguza gharama ya juu ya maisha, Kenya Kwanza na Azimio hawakukubaliana kuhusu kushushwa kwa ushuru (VAT) unaotozwa mafuta ya petroli kutoka asilimia 16 hadi 8, na kuondolewa kwa ada ya asilimia 3 inatozwa mwajiri na mfanyakazi kwa minajili ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu.

Badala yake, masuala hayo yaliachiwa Rais William Ruto (Kenya Kwanza) na kinara wa Azimio, Bw Raila Odinga kutoa maamuzi.

Aidha, wawili hao walitumiwa ripoti hiyo kwa njia ya kielektroniki.

Bunge la Kitaifa, baadaye litakabidhiwa ripoti hiyo kuijadili, aidha, kuipitisha au kuiangusha.

 

  • Tags

You can share this post!

Mvinyo wa ‘white wine’ unavyotumiwa kudumisha urembo wa...

Huzuni 1 akiuawa na nyumba 10 kuteketezwa moto kwenye...

T L