• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Kaunti ya Nyamira yamulikwa kwa kuajiri wafanyakazi wote kutoka kabila moja isipokuwa mmoja

Kaunti ya Nyamira yamulikwa kwa kuajiri wafanyakazi wote kutoka kabila moja isipokuwa mmoja

NA MARY WANGARI

SENETI huenda ikabuni sheria itakayoruhusu watumishi wa umma kuhamishwa kutoka kaunti moja hadi nyingine katika juhudi za kuangamiza ukabila katika ajira za kaunti.

Maseneta wanalitafakari hili baada ya kuibuka kwamba baadhi ya serikali za kaunti zinakiuka sheria kuhusu ajira za watumishi wa umma kwenye mabunge ya kaunti zao.

Sheria kuhusu Serikali za Kaunti 2012 inasema kuwa, angalau asilimia 30 ya nyadhifa zinazosalia tupu mwanzoni mwa usimamizi mpya, zinapaswa kujazwa na watu wasio wa kabila la wakazi wa kaunti hiyo.

Serikali ya Kaunti ya Nyamira ni miongoni mwa kaunti zinazokiuka sheria hiyo huku ikiibuka kwamba watumishi wote wa umma, isipokuwa mmoja tu, ni wa kabila moja.

Kamati ya Bunge la Seneti inayosimamia Hesabu za Pesa za Umma katika kikao jana Jumatatu ilielezwa kuwa asilimia 99.9 ya wafanyakazi wote 223 katika Bunge la Kaunti ya Nyamira wanatoka katika jamii ya Wakisii.

Wakijitetea mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang, Spika na Katibu wa Bunge la Kaunti ya  Nyamira – Enock Okello na Dan Orina – mtawalia, walisema kuwa idadi kubwa ya wakazi wa Nyamira ni Wakisii.

Kulingana na Spika wa Bunge la Kaunti hiyo, wengi wanaotuma maombi wakitaka nyadhifa mbalimbali wanatoka eneo hilo.

Aidha, alisema wafanyakazi waliopo kwa sasa waliajiriwa wakati mfumo wa ugatuzi ulipoanzishwa, akiahidi kuwa uongozi wa kaunti hiyo unashughulikia suala hilo.

“Kosa lilitendeka mwanzoni kabisa wa ugatuzi lakini tutashughulikia tatizo hilo kadri tunavyoendelea,” alisema Bw Okello.

“Suala hili linazidi kushughulikiwa kwa sababu sasa serikali ya kaunti ipo kwenye mchakato wa kutekeleza mapendekezo iliyopatiwa kuhusu wafanyakazi wake.”

Spika Okello na Katibu Orina walikuwa wamefika mbele ya Kamati hiyo kujibu maswali yaliyozuka kwenye Ripoti ya Mkaguzi Mkuu kuhusu bajeti iliyokamilika 2019/2020.

“Katika hali hii, Bunge la Kaunti limekiuka sheria kuhusu uimarishaji wa kujumuisha makabila yote katika ajira,” ilisema ripoti ya Mkaguzi Mkuu.

Waundasheria wakiongozwa na Seneta wa Kaunti ya Nairobi, Edwin Sifuna, walihoji ni vipi kaunti hiyo inaweza kuajiri wafanyakazi wote kutoka kabila moja ilhali inajipiga kifua kwamba inadumisha usawa katika ajira.

“Unataka kusema watu kutoka kaunti jirani za Bomet, Homabay na Kericho kamwe huwa hatumi maombi ya kazi Nyamira,” aliuliza Seneta Sifuna.

“Ninahofia kuhusu mwajiriwa huyo mmoja ambaye si wa jamii ya Wakisii. Nashangaa ni vipi anaweza kuendeelea na shughuli zake za kila siku miongoni mwa watu ambao wote wanatoka jamii moja,” alisema.

Hata hivyo, Bw Okello alisisitiza kuwa nyadhifa zote za kazi katika Serikali ya Kaunti ya Nyamira hutangazwa kupitia vituo vikuu vya habari na kwamba huwa ziko wazi kwa Wakenya wote kutuma maombi yao pasipo kubaguliwa.

  • Tags

You can share this post!

Mary Moraa atarajiwa kuwa kivutio kwenye riadha za polisi

Ulinzi Starlets walenga kutwaa taji la KWPL msimu ujao

T L