• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mary Moraa atarajiwa kuwa kivutio kwenye riadha za polisi

Mary Moraa atarajiwa kuwa kivutio kwenye riadha za polisi

Na AYUMBA AYODI

WANAMEDALI wa Jumuiya ya Madola Mary Moraa (mita 800), Beatrice Chebet (5000m) na Daniel Simiu (10000m) watakuwa vivutio kwenye riadha za kitaifa za Idara ya Polisi ugani Moi Kasarani hapo Juni 7-8.

Kocha mkuu wa timu ya polisi ya riadha Isaac Kirwa amesema mashindano hayo yatakuwa ya siku mbili wala sio tatu ilivyoripotiwa hapo awali.

Bingwa wa Jumuiya ya Madola mbio za 800m Wycliffe Kinyamal, mshikilizi wa rekodi ya dunia ya 3,000m kuruka viunzi na maji Beatrice Chepkoech na mshindi wa nishani ya shaba ya Riadha za Dunia za Ukumbini 1500m Abel Kipsang pia watashiriki mashindano haya.

Mabingwa wa zamani wa kitaifa mbio za 100m Monica Safania, Millicent Ndoro na Eunice Kadogo watanogesha kitengo hicho na pia mita 200 naye Peter Mwai anatarajiwa kutumia fursa ya kukosekana kwa bingwa wa Afrika na Jumuiya ya Madola Ferdinand Omanyala, kung’ara. Omanyala yuko jijini Paris, Ufaransa kwa duru ya Diamond League.

Mshindi wa Jumuiya ya Madola 3,000m kuruka viunzi na maji Abraham Kibiwott anatumai kutetea taji lake la polisi.

Moraa atajibwaga uwanjani akiwa na motisha kuendeleza msimu mzuri ambapo amebeba mataji ya Kip Keino Classic Continental Tour na Rabat Diamond League.

Mshikilizi huyo wa rekodi ya kitaifa ya 400m atalenga kuhifadhi mataji yake ya 400m na 800m.

“Kuna presha ya kushiriki mashindano hapa nyumbani ninapowakilisha timu yangu,” alikiri Moraa anayepanga kuelekea Lausanne Diamond League nchini Uswisi akilenga kukamilisha 800m kwa dakika 1:58 Julai 25.

Chebet pia alitawala Kip Keino Classic katika mbio za 5000m mwezi Mei.

“Bado sijaamua nishiriki 1500m kutafuta kasi ama 5000m. Nitaamua kabla ya mashindano,” alisema bingwa huyo wa mbio za nyika duniani.

Chebet aliridhika na nafasi ya pili kwenye mashindano ya polisi mwaka 2022 nyuma ya Mercy Cherono.

Analenga kufuata nyayo za shujaa wake, bingwa mara mbili wa dunia 5000m Hellen Obiri katika kutwaa mataji ya dunia katika msimu mmoja. Obiri alishinda mataji ya mbio za nyika na 5000m duniani mwaka 2019 mjini Aarhus, Denmark na Doha, Qatar, mtawalia.

“Hiyo ndiyo ndoto yangu,” alisema Chebet aliyeshinda mbio za nyika nchini Australia mwezi Februari mwaka huu. Riadha za Dunia ni Agosti jijini Budapest, Hungary.

Simiu alishinda taji lake la kwanza la polisi mwaka 2022. Chepkoech ataweka hatarini mataji yake ya 3000m kuruka viunzi na maji na 1500m nao Kinyamal na Kipsang walishinda 800m na 1500m, mtawalia.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE 

  • Tags

You can share this post!

Bei ya vyakula kuongezeka

Kaunti ya Nyamira yamulikwa kwa kuajiri wafanyakazi wote...

T L