• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 12:41 PM
Mombasa yameremeta Krismasi ikibisha hodi

Mombasa yameremeta Krismasi ikibisha hodi

NA CHARLES ONGADI

SHAMRASHAMRA za Sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya zinaendelea kunoga Mombasa huku barabara nyingi katikati mwa jiji zikimeremeta kwa aina mbalimbali ya mapambo.

Katika mzunguko wa Makupa katika barabara ilelekeayo kitovuni mwa jiji la Mombasa, kuna aina tofauti ya sanamu za wanyama wa porini waliopambwa kwa taa zenye rangi tofauti zinazomeremeta na kuvutia.

Pembezoni mwa barabara ya Tom Mboya ikielekea mtaa wa Tudor kumetundikwa sanamu ya kuvutia ya ‘Baba Krismasi’ akiwa na zawadi kibao za kupeana wakati wa sikukuu ya Krismasi.

Mapambo haya yaliyoendelezwa hadi katikati mwa jiji yamefanywa na serikali ya Kaunti ya Mombasa kwa ushirikiano mkubwa na kampuni ya simiti ya Mombasa Cement yamebadilisha sura ya jiji hili la kitalii na kuiweka katika utayari wa kukaribisha  Sherehe za Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Jiji la Mombasa lameremeta. PICHA | CHARLES ONGADI

Aidha, kulingana na uchunguzi uliofanywa Taifa Leo, wafanyibiashara wadogo wadogo wanaouza vyakula na bidhaa zengine pembezoni mwa barabara katikati ya jiji wameanza kuvuna pakubwa kutokana na idadi kubwa ya watalii ambao wameanza kufurika katika jiji hili.

“Tumeanza kupata wateja wengi ambao tunawauzia vyakula vya Kipwani hasa wateja wetu kutoka bara wanaovutiwa na mapishi yetu,” anasema Fatuma Bakari anayeuza aina tofauti za vyakula karibu na kituo cha mabasi ya kuelekea bara.

Bi Bakari anasema baadhi ya wateja wao ni abiria wanaosubiri usafiri na waliowasili na pia wanaojivinjari kufurahia mandhari ya Mombasa nyakati za usiku.

Jiji la Mombasa lameremeta. PICHA | CHARLES ONGADI

Wakati huo huo kampuni nyingi za uchukuzi zilipandisha nauli kutokana na idadi inayoongezeka ya wasafiri.

Kutoka Mombasa hadi Nairobi nauli imeongezeka kutoka Sh1,200 hadi 1,800 huku wanaoelekea Kisumu wakilipa Sh4,500 kutoka nauli ya kawaida ya Sh2,000.

Lakini licha ya kupanda kwa nauli, idadi ya wasafiri ilionekana kuongezeka ijapo kulingana na Bw Pascal Odhiambo ambaye ni utingo katika kituo cha mabasi ya kuelekea bara anasema si wengi wanaosafiri.

“Mwaka 2022 kulikuwa na idadi kubwa ya wasafiri kuliko mwaka huu wengi wakilalamikia hali mbaya ya uchumi,” akasema Bw Odhiambo.

  • Tags

You can share this post!

KCPE: Shule za kibinafsi zalia kuhusu uteuzi wa sekondari

Sabina Chege: Raila angeshinda urais mwaka 2022 ikiwa...

T L