• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Kifafanuzi: Je, wajua alichoenda kufanya Dubai Rais William Ruto?

Kifafanuzi: Je, wajua alichoenda kufanya Dubai Rais William Ruto?

NA MARY WANGARI

RAIS William Ruto ni moja kati ya viongozi 100 wa dunia ambao wamekusanyika katika Milki ya Kiarabu (UAE) jijini Dubai kuhudhuria Kongamano Kuu la Kimataifa kuhusu Mazingira, UNFCCC COP28.

Kiongozi wa taifa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Viongozi wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Anga (CAHOSCC) alisafiri Alhamisi Novemba 30, 2023 kuelekea Dubai kwa mujibu wa Msemaji wa Ikulu, Hussein Mohamed.

Kando na kusoma hotuba kwa niaba ya Bara la Afrika, Rais Ruto anatazamiwa kuangazia masuala nyeti yanayodhamiriwa kupigia debe ajenda ya Kenya na Afrika kuhusu hali ya anga.

Aidha, Dkt Ruto anatazamiwa kupigia debe Maazimio ya Nairobi yaliyoafikiwa na viongozi wa Afrika katika Kongamano la kwanza kabisa kuwahi kufanyika Afrika kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Anga, lililoandaliwa jijini Nairobi mnamo Septemba mwaka huu.

Kuambatana na maazimio hayo, Rais ataongoza hafla tatu kuu katika Kongamano hilo ikiwemo uzinduzi wa mradi wenye thamani ya Sh687.2 bilioni kuhusu Mpango wa Uwekezaji katika Kawi Salama Afrika (AGII) ukiongozwa na UAE.

AGII ni ushirikiano baina ya uongozi wa COP28, serikali ya Kenya na mataifa mengine Barani Afrika kwa lengo la kuharakisha mabadiliko muhimu kupitia uwekezaji katika miradi inayohusu kawi salama.

Mpango huo unanuiwa kusaidia nchi za Afrika kuanzisha viwanda vinavyotumia kawi salama hatua itakayochochea biashara, kuunda ajira na ukuaji kiuchumi.

“Lengo kuu ni kuharakisha ukuaji wa viwanda na biashara zinazohusu uzalishaji wa kawi salama Afrika, kuendeleza mikakati ya kustahimili na kuzuia mabadiliko ya hali ya anga ikiwemo kuwezesha uundaji wa ajira na ukuaji kiuchumi barani,” ilisema taarifa kutoka Ikulu iliyofikia Taifa Leo.

Tangu alipotawazwa kama Rais mwaka jana mnamo Septemba, Dkt Ruto amekuwa akisisitiza haja ya kuwepo mikakati madhubuti ya kupambana na janga la mabadiliko ya hali ya anga duniani.

Alijitwalia umaarufu kwa hotuba ya kutajika aliyotoa katika Kongamano la COP27 lililoandaliwa Misri mnamo Novemba mwaka jana, ambapo aligeuza mtazamo wa nchi za Afrika kuhusu hali ya anga kuwa nafasi za uwekezaji badala wahasiriwa.

Kenya na Bara la Afrika kwa jumla zinasheheni utajiri wa raslimali asilia, chemichemi za kawi salama ambazo bado hazijaanza kutumia na idadi inayozidi kukua ya wafanyakazi, sifa zinazowezesha ustawishaji wa maendeleo na kutoa mchango muhimu kwa juhudi za kuhifadhi mazingira kimataifa.

Rais Ruto anakusudia kugeuza Kenya na afrika kuwa vituo vikuu vya kufanikisha ajenda ya kupunguza viwango vya hewa sumu angani kote duniani kupitia uzalishaji wa kawi salama.

Katika juhudi za kufanikisha haya, Dkt Ruto amekuwa akipigia debe mageuzi thabiti kwenye mifumo ya fedha huku akisisitiza haja ya kuoanisha taasisi za fedha kimataifa kama vile Benki ya Dunia na Hazina ya Fedha Kimataifa (IMF) na malengo ya Afrika kuhusu maendeleo na hali ya anga.

  • Tags

You can share this post!

Demu wangu amekuwa akichati kisiri na kakangu mkubwa,...

LUGHA NA FASIHI: Tafsiri ya riwaya ‘The Alchemist’

T L