• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
LUGHA NA FASIHI: Tafsiri ya riwaya ‘The Alchemist’

LUGHA NA FASIHI: Tafsiri ya riwaya ‘The Alchemist’

MWANDISHI Ali Attas ni bingwa wa kutumia ala mbalimbali za fasihi kusawiri taratibu za maisha ya wanajamii kupitia tungo za kusisimua.

Aliwahi kutafsiri hadithi mashuhuri Japani, ‘Watoto wa Hiroshima’ (2016) – tafsiri ya insha za kumbukumbu ya maafa ya mabomu ya atomiki yaliyodondoshwa Hiroshima na Nagasaki nchini Japani.

Kitabu ‘Mualkemia’, ambacho kimetafsiriwa kutoka “The Alchemist” chake Paulo Coelho, na mwanahabari Mkenya, Alli Attas. PICHA|HISANI

Mwaka uliopita wa 2022, alitafsiri kazi maarufu sana duniani – hadithi ya ‘Mualkemia’ (Moran Publishers, 2022) kutoka kazi asilia Alquimista (kwa Kireno) na The Alchemist (kwa Kiingereza) – riwaya iliyotungwa 1988 na mwandishi mtajika Paulo Coelho kutoka Brazil. Mualkemia ni tafsiri ya themanini na nane ya riwaya hii mashuhuri.

“Ilinichukua miezi mitatu kutafsiri kitabu hiki ambacho kimetafsiriwa katika zaidi ya lugha 80 na kuuzwa kwa mamilioni nyingi mno kushinda kitabu chochote kingine duniani (kinashikilia rekodi ya dunia katika Guinness Book of Records),” anasema Attas.

Hadithi ya Mualkemia inahimiza kila binadamu mwenye maono kujizatiti na kukiuka vizingiti hadi kuzifikia ndoto zake. Mwandishi anatukumbusha kuwa mtu akitia nia, basi atapata njia ya kufanikisha malengo yake.

Hadithi inaanza kwa mvumo wa upepo kutoka Afrika ukimletea mvulana mchungaji wa mifugo busu la msichana katika safari inayomwezesha kutambua fursa nyingi za kuzimua ndoto zake maishani.

Kufikia sasa, Mualkemia ndicho kitabu cha mwandishi aliye hai ambacho kimewahi kutafsiriwa katika lugha nyingi zaidi duniani. Ni riwaya ya kiistiara inayowasilisha hadithi kuhusu Santiago, kijana mfugaji wa kondoo kutoka eneo la Andalusia, Uhispania.

Ndoto

Usiku mmoja, Santiago akiwa amelala katika gofu la kanisa, anaota ndoto inayojirudia kuhusu hazina iliyozikwa.

Anamwendea mwanamke mpigaramli wa Kijipsi ili amfasirie ndoto yake. Mwanamke huyu anamwambia kuwa itambidi asafiri hadi kwenye mapiramidi ya Misri ilikozikwa hazina hiyo. Ubashiri huu unatiliwa nguvu na Melchizedek, Mfalme wa Salem, ambaye anamshauri Santiago awauze kondoo wake ili asafiri hadi Misri iliko hazina yake.

Anapofika Misri, Santiago anakumbana na kizuizi cha kwanza. Anaibiwa hela zote alizozipata baada ya kuuza kondoo wake na pwagu aliyekuwa amemhadaa kuwa angemsaidia kufika kwenye mapiramidi. Anashurutika kufanya kazi katika duka la bepari muuza vifaa vya mawe ya kioo ili apate hela za kumwezesha kuendelea na safari yake.

Santiago anamsaidia bepari huyu kuikuza biashara yake kupitia mawazo yake bunifu. Hatimaye, Santiago anapata fedha za kumwezesha kuendelea na safari yake. Anajiunga na msafara uliokuwa ukisafiri kupitia Jangwa la Sahara. Kwenye msafara huu, anaungana na Bwana Muingereza aliyekuwa akisafiri kwenda kumtafuta Mualkemia.

Wanapofika kwenye eneo la Jicho huko jangwani, kizuizi kingine kinatokea. Msafara unasitishwa kutokana na vita vya makabila huko jangwani. Akiwa huko, Santiago anakutana na msichana wa Kiarabu anayeitwa Fatima. Anampenda na kumpendekezea ndoa.

Fatima anakubali kuolewa na Santiago lakini anampa sharti la kukamilisha safari yake kwanza. Ingawa jibu la Fatima linamvunja moyo awali, Santiago anabaini baadaye kuwa mapenzi ya kweli hudumu na haikuwa busara aitelekeze ndoto yake kwa sababu ya mapenzi kwani kwa kufanya hivyo, mapenzi hayo yangekosa kuwa ya kweli.

Hatimaye, Santiago anakutana na Mualkemia anayemfunza kujitambua. Kujitambua huku kunamwezesha kusoma ishara za maumbile. Baadaye, Mualkemia huyo anamsindikiza Santiago katika safari yake ya kwenda kwenye mapiramidi. Uwezo wa kusoma ishara za maumbile unawasaidia kukwepa kuuliwa na wapiganaji hatari wa makabila.

Mualkemia anapomwacha Santiago, ishara fulani inamwelekeza hadi pahali karibu na mapiramidi ambapo angechimbua na kuipata hazina. Huku akichimbua, anavamiwa na wahuni wanaomuibia dhahabu yake na kumpiga hadi kumjeruhi.

Wanapoanza kuondoka, kiongozi wa wahuni hao anarudi alipokuwa Santiago na kumwambia, “Miaka miwili iliyopita hata mimi niliota ndoto zilizojirudia… Niliota kwamba ninapaswa kusafiri katika mbuga za Uhispania na kutafuta gofu la kanisa ambapo nikichimbua kwenye mizizi ya mkuyu ulio karibu ningekuta hazina iliyofichwa. Lakini mimi si mjinga kuvuka jangwa zima kwa sababu tu ya ndoto zinazojirudia mara kwa mara.”

Santiago anarudi hadi Uhispania kwenye gofu alimokuwa akilala wakati alipoota ndoto yake. Alifukua kwenye mizizi ya mkuyu uliokuwa karibu na kanisa hilo na kuipata hazina aliyokuwa akiitafuta. Hazina hiyo ilikuwa kasha la sarafu za dhahabu za Uhispania, mawe ya dhahabu pamoja na sanamu za mawe zilizopachikwa vito vya thamani.

Safari ya Santiago ni istiara ya umuhimu wa mwanadamu kufuatilia ndoto zake bila kukatizwa tamaa na vizuizi anavyokumbana navyo. Safari yenyewe itakuwa na pandashuka zake lakini hatimaye juhudi zote zitazaa matunda.

Funzo

Funzo kuu linalojitokeza katika riwaya hii ni kuwa, mwanadamu anapoamua kuzifuata ndoto zake, maumbile yote huchangia ufanisi wa juhudi zake.

Mbali na ujumbe unaojitokeza katika riwaya hii, msomaji atabaini uongo mkuu unaowakumba wanadamu wote ulimwenguni. Aidha, msomaji atafurahia taharuki inayoteka makini hadi kwenye hatima ya safari ya mhusika mkuu. Vilevile, atachangamshwa na ucheshi unaotanda kote katika ploti.

Kwa mfano, uzuzu wa Bwana Mwingereza anayesoma matopa ya vitabu ili ajue siri ya ualkemia. Vilevile, msomaji atatekwa na mazungumzo ya kiajabu kati ya Santiago na jua, jangwa na upepo. Mualkemia ni hazina kwa jumuiya inayozungumza Kiswahili.

Tafsiri hukuza lugha pokezi kwa njia mbili – lugha pokezi hunufaika kutokana na mtafsiri kubuni msamiati wa kuelezea dhana ngeni kutoka kwa utamaduni wa kazi asilia; na kazi zilizotafsiriwa hukuza fasihi ya lugha pokezi. Kwa mintarafu hii, kuchapishwa kwa riwaya tafsiri ya Mualkemia kumeifaidi lugha na fasihi ya Kiswahili.

“Ni hadithi ya kuvutia ambayo imesomwa na watu wengi duniani, akiwemo rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton. Ni kazi iliyonipa fursa nyingine ya kuoanisha kipaji cha utunzi na tafsiri katika kuchangia ukwasi wa taaluma ya tafsiri,” anasisitiza Attas.

  • Tags

You can share this post!

Kifafanuzi: Je, wajua alichoenda kufanya Dubai Rais William...

Harusi hatuna: Jinsi gharama imeingiza baridi wapenzi...

T L