• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:26 PM
Kioni asisitiza NDC ya Jubilee iliyoitishwa na mrengo wa Uhuru itaendelea

Kioni asisitiza NDC ya Jubilee iliyoitishwa na mrengo wa Uhuru itaendelea

Na CHARLES WASONGA

VIONGOZI wa Jubilee wanaounga mkono Rais mstaafu Uhuru Kenyatta wameshikilia kuwa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) la Jubilee litaendelea Mei 22, 2023 jinsi ilivyopangwa.

Wakiongozwa na Katibu Mkuu Jeremiah Kioni viongozi hao waliwaagiza wajumbe wote wa chama hicho kujiandaa kuhudhuria kongamano litakalofanyika katika jumba la mikutano ya kimataifa ya Kenya (KICC), Nairobi.

“Mkutano huo utafanyika mnamo Mei 22 hadi Mei 23; kwa hivyo tunawaomba wajumbe wa Jubilee kupuuzilia mbali yale ambayo yametangazwa na wale waasi na kuchapishwa magazetini,” akasema kwenye kikao na wanahabari Alhamisi jijini Nairobi.

Bw Kioni ambaye ni mbunge wa zamani wa Ndaragua alikuwa ameandamana na naibu mwenyekiti David Murathe..

“Nitaongoza mkutano huo na Uhuru atakuja tu kuidhinisha yale ambayo tutakubaliana,” akaongeza.

Mkutano huo ulifanyika kwa ajili ya kuweka mikakati ya kongamano hilo la NDC na ukahudhuriwa na wenyeviti wa Jubilee katika ngazi za kaunti.

Bw Kioni alisema hayo siku mbili baada ya mrengo wa Mbunge wa Afrika Mashariki (EALA) Kanini Kegan na Mbunge Maalum Sabina Chege kutangaza kuwa NDC hiyo iliyoitishwa na Bw Kenyatta imefutuliwa mbali.

Kiongozi huyo alisema kuwa chama hicho kinamilikiwa na wananchi na kwamba NDC hiyo itaendelea ilivyopangwa.

“Hii sio suala la Uhuru Kenyatta, ni suala la wanachama na ndio maana tunasema kwamba twapaswa kupigania,” Bw Kioni akaongeza.

Kwa upande wake, Bw Murathe aliwashauri wanachama ambao wanataka kuwania nyadhifa za uongoza katika Jubilee kuhudhuria mkutano huo wa NDC.

“Ikiwa wanataka kutuondoa kwenye afisi waje na mapendekezo yao na yakipitishwa tutaondoka kwa heshima, yakifeli sharti wahame,” Bw Murathe akasema akirejelea Bw Kega na viongozi kwenye mrengo wake.

Bw Murathe pia alidai kuwa Rais William Ruto ndiye anachochea mzozo wa uongozi kati yake na Bw Kega.

“Tudanganyane. Hii sio vita kati ya Kioni na Kega bali mtu ambaye anataka kututhibitishia kwamba sasa yeye ni mkubwa kwa sababu tulimfurusha kutoka chama hiki,” akasema.

Mnamo Jumatano kundi la Bw Kega kupitia tangazo magazetini lilitangaza kuwa NDC hiyo ya Mei 22, 2023 imefutiliwa mbali.

“Zingatia kwamba Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) ya Jubilee imesimamisha notisi ya kongamano maalum la kitaifa ya wajumbe iliyochapishwa magazetini mnamo Aprili 29,” ikasema taarifa hiyo ya kundi la Kega, ambaye mnamo Februari 2023 aliteuliwa kuwa kaimu Katibu Mkuu wa Jubilee.

Mbunge huyo wa zamani wa Kieni alisema hivi karibuni chama cha Jubilee kitaitisha kongamano maalum.

“Hivi karibuni chama kitatoa notisi ya kuitisha Kongamano Maalum ya Kitaifa la Wajumbe kulingana na maamuzi ya mkutano wa baraza kuu la kitaifa (NEC) uliofanyika Februari mwaka huu,” akasema Bw Kega.

Alisema Bw Kenyatta hakufuata utaratibu ufaao kuitisha kongamano hilo, akiongeza kuwa mkutano wa NDC sharti uungwe mkono na wanachama wote.

“Juzi, Rais wa zamani alivamia makao makuu ya chama akiandamana na watu ambao hata sio wanachama wa Jubilee,” akasema Bw Kega.

Uamuzi wa Bw Kega unajiri wakati ambapo mbunge wa zamani Hassan Osman amewasilishwa kesi kwa Jopo la Kutatua Mizozo ya Vyama (PPDT) akimshtaka Bw Kenyatta.

Osman ambaye alihudumu kama Mbunge Maalum katika bunge la 11, alisema uamuzi wa Bw Kenyatta wa kuitisha NDC ni kinyume cha sheria na kwamba PPDT inapaswa kusimamisha kongamano hilo.

  • Tags

You can share this post!

Jowie atolewa jasho kueleza damu ya Monica Kimani...

Kibo Africa yazindua pikipiki ya injini ya 160cc

T L