• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Lami: Hatimaye Lamu Mashariki yafikiwa

Lami: Hatimaye Lamu Mashariki yafikiwa

NA KALUME KAZUNGU

NI mwamko mpya kwa eneobunge la Lamu Mashariki baada ya Rais William Ruto Jumamosi kuongoza uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya kwanza ya lami baada ya miaka 60 ya uhuru.

Barabara hiyo ya kilomita 50 ambayo ni ya kutoka eneo la Mtangawanda kuelekea Faza, Kizingitini na viungani mwake, imekuwa mbovu kwa muda mrefu kwani ni ya changarawe, mawe na pia imesheheni mashimo.

Wakazi wa eneo hilo wamevumilia hali ngumu hasa wakati wa kiangazi kwani barabara hiyo huwa imejaa vumbi ilhali wakati wa mvua ikisheheni matope na vidimbwi vya maji chafu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa barabara hiyo mjini Kizingitini, Rais Ruto alisema azma ya serikali ya Kenya Kwanza ni kuhakikisha kila eneo hapa nchini linaafikia maendeleo sawa kwa manufaa ya wananchi.

Aliitaja barabara ya Mtangawanda-Faza-Kizingitini kuwa muhimu kwani itasaidia kupanua eneo hilo kibiashara, kiuchumi na maendeleo mengine na hata kupiga jeki usalama.

Rais Ruto aliwasihi wananchi kushirikiana na serikali kuu katika kuhakikisha maendeleo yanaafikiwa kila upande.

Alisema serikali ya Kenya Kwanza inamjali mwananchi wake, akisisitiza kuwa furaha yake ni kuona wakenya wakiishi maisha yaliyoboreshwa.

“Kila eneo la nchi hii, ikiwemo Lamu tumelijumuisha kwenye ajenda ya maendeleo ya serikali. Na hii ndiyo sababu tuko hapa kuzindua ujenzi wa barabara ya kwanza ya lami hapa Lamu Mashariki. Mbali na barabara, pia tutajitahidi kuona kwamba wavuvi wetu wanaishi vyema kwa kuwaboreshea miundomsingi yao. Ajenda ya hii serikali ya Kenya Kwanza ni kuhakikisha hata yule mwananchi wa chini kabisa anainuliwa kimaisha,” akasema Rais Ruto.

Kwa upande wake, Naibu Rais, Rigathi Gachagua aliwapongeza wananchi wa Lamu kwa kuepuka siasa mbovu na badala yake kushirikiana na serikali kuu katika kupeleka ajenda za maendeleo mbele.

Aliwashauri wananchi wa Lamu kuwa kitu kimoja ili kufaidi maendeleo zaidi.

Kwa upande wake, Waziri wa Barabara Kipchumba Murkomen ambaye aliandamana na Rais Ruto kwenye ziara ya Lamu alisema mbali na barabara za Lamu Mashariki, serikali pia inalenga kuimarisha barabara za eneobunge la Lamu Magharibi.

Alitaja barabara inayounganisha Bandari ya Lamu na miundomsingi ya uchukuzi wa Kenya, Ethiopia na Sudan Kusini (Lapsset) ya Lamu-Ijara-Garissa kwamba ujenzi wake, hasa wa lami unaendelea.

“Tutahakikisha huku tukjijenga barabara za Lamu Mashariki, pia zile za Lamu Magharibi kama vile ile ya Lamu-Ijara-Garissa zinaendelea kujengwa vyema kwa kutiwa lami. Twaamini barabara zikiboreshwa Lamu na eneo zima la Kaskazini mwa Kenya litapanuka kibiashara, kiuchumi na maendeleo mengine,” akasema Bw Murkomen.

Wakazi wa ziara ya Jumamosi, Rais Ruto pia alifungua rasmi chuo cha kiufundi anuwai cha Kizingitini (TTI).

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Elimu Profesa Ezekiel Machogu aliwasihi wazazi wa watoto Lamu na Kenya kwa ujumla kuhakikisha watoto wao wanasoma kwa manufaa yao ya siku za usoni.

Profesa Machogu alisema serikali tayari imehakikisha miundomsingi yote inayohitajika ya elimu kwenye chuo hicho cha mafunzo anuwai cha Kizingitini imefikishwa au kutekelezwa.

“Twatarajia wanafunzi waanze kusajiliwa kwenye chuo hiki kufikia Januari,2024. Wazazi mwajibike kwani serikali imeweka miundomisngi imara ya masomo chuoni hapa,” akasems Profesa Machogu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Lamu Mashariki, Ruweida Obo alimpongeza Rais Ruto kwa kuzingatia Lamu Mashariki kimiundomsingi, hasa barabara na elimu.

“Nimekuwa nikilia kuhusu barabara na miundomsingi ya elimu kila wakati ninaposimama bungeni au ninapokutana na watu wangu hapa Lamu Mashariki. Nafurahi kwamba leo Rais wetu anazindua rasmi barabara yetu ya Mtangawanda-Faza-Kizingitini. Niko na imani kubwa kwa Rais Ruto kwamba makuu zaidi yatafika eneo hili,” akasema Bi Obo.

Naye Gavana wa Lamu, Issa Timamy aliahidi ushirikiano wake na serikali kuu katika kuhakikisha maendeleo zaidi yanaafikiwa Lamu na nchini kwa ujumla.

Wengine walioandamana na Rais Ruto kwenye ziara ya Lamu ni mawaziri, Aisha Jumwa (Jinsia), Aden Duale (Ulinzi), Salim Mvurya (Uvuvi na Uchumi Baharini), wabunge Kimani Ichung’wah (Kikuyu), Stanley Muthama (Lamu Magharibi), Seneta wa Lamu Joseph Githuku, Shakila Abdallah (Seneta Maalum), Spika wa Bunge la Seneti Amason Kingi, na viongozi wengine wakuu serikalini.

  • Tags

You can share this post!

Mwamko mpya mahakama ya Thika ikipata jaji

AstraZeneca yaifaa KNH kwa mashine ya kisasa ya tiba ya...

T L