• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Madereva, vijana wagaragaza gozi uwanjani kupambana na ulevi Krismasi

Madereva, vijana wagaragaza gozi uwanjani kupambana na ulevi Krismasi

NA FRIDAH OKACHI

MADEREVA, utingo na vijana kutoka Kikuyu na Kawangware walishiriki mchezo wa kandanda kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya na unywaji wa pombe kiholela msimu huu wa Krismasi.

Makundi hayo yalikusanyika katika uwanja wa michezo wa Kawangware na kushiriki kwenye mchezo ili kupunguza utumiaji wa pombe na kujihusisha na kazi za kuwanufaisha huku wakiepuka wizi.

Msimamizi wa kituo cha kupigania haki Dagoretti, Bw Wainaina Kamau, alisema hatua hiyo itasaidia idadi kubwa ya vijana kuepuka utumiaji wa mihadarati na unywaji pombe kupitia mchezo huo ambao umeandaliwa kufanyika kila wiki siku ya Jumatatu.

“Wakati huu wa sherehe, madereva na utingo ambao ni vijana hujipata kwa majaribu ya kubugia mvinyo kupita kiasi. Pia, kuna wale wana mkono mrefu wakati wa kuelekeza abiria. Katika muda wanaotumia kuja kucheza na kurejea kazini, utawafanya kuwa watu bora wakati huu. Dakika wanazotumia hapa ni wakati, wameegesha magari yao wakisubiri abiria,” alisema Bw Wainaina.

Kwenye mchezo huo, umejumuisha kundi la utingo saba ambalo linafahamika Chini ya Mnazi na kundi la Team Change ambalo lina vijana ambao zamani walikuwa wakishiriki wizi wa kimabavu lakini wakabadilika kuwa watu wema.

Bw George Ochieng aliambia Taifa Leo kuwa ni miongoni mwa vijana ambao walikuwa wakitekeleza wizi wa kimabavu na kisha kutumia mihadarati kwa wingi.

Madereva na utingo pamoja na vijana wa maeneo ya Kikuyu na Kawangware wakicheza soka uwanjani. PICHA | FRIDAH OKACHI

Alisema hatua hiyo itasaidia vijana kujumuika na kutangamana na viongozi wanaohakikisha usalama unadumishwa.

“Hapa tuna makundi matatu. Unapata dawa za kulevya na wizi zinaandamana. Iwapo hatutaweza kushirikisha kila mmoja, jamii itaumia kwa kuporwa au hata kufa iwapo madereva watakunya pombe kupita kiasi. Team change lina vijana zaidi ya 50 ambao wamebadilika,” alisema Bw Ochieng.

Dereva wa matatu za ruti ya Kikuyu-Kawangware alisema unywaji wa pombe huongezeka wakati huu, kutokana na mapato ya juu na wengi wakishindwa jinsi ya kutumia. Dereva huyo alishukuru kupata mafunzo ya kutumia pesa zake.

“Nashukuru kwa sababu sasa nitajua jinsi ambavyo nitatumia pesa zangu. Anasa ya pombe hukolea wakati tunasimama sehemu mbalimbali. Kwa siku kadhaa nimeweza kuelimika kwamba nahitaji kufanya nini na nina uhakika Januari sitasumbuana na familia yangu kwa kukosa karo ya mtoto wangu katika wakati unaofaa,” alisema dereva huyo.

  • Tags

You can share this post!

Msaada wachelewa kuwafikia waathiriwa wa mafuriko Tana River

Pendekezo la kufungwa mangweni za pombe ya mnazi lazua...

T L