• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Pendekezo la kufungwa mangweni za pombe ya mnazi lazua mgawanyiko baina ya viongozi wa kidini, wafanyabiashara

Pendekezo la kufungwa mangweni za pombe ya mnazi lazua mgawanyiko baina ya viongozi wa kidini, wafanyabiashara

NA ALEX KALAMA

VIONGOZI wa kidini na wale wa kibiashara katika Kaunti ya Kilifi wamehitilafiana vikali kuhusu pendekezo la kufungwa vituo vya kuuzia pombe ya mnazi mjini Malindi.

Hatua hiyo imejiri baada ya mwenyekiti wa vuguvugu la usalama wa wafanyabiashara mjini Malindi, Bw Athman Said, kupendekeza kufungwa kwa maeneo ya kubugia mnazi almaarufu kama mangweni kwa misingi kuwa yanaharibu watoto katika eneo hilo.

“Mangweni ambazo ni za kuuza mnazi zimekuwa nyingi sana katika mji wetu wa Malindi na kuna nyingi ambazo zinatumika kama sehemu ya kuficha majambazi na kama sehemu ya kuuzia dawa za kulevya na kuharibu vijana wetu. Nakuomba naibu kamishina wa eneo hili la Malindi ukishirikiana na serikali ya kaunti uweze kushughulikia hilo jambo ipasavyo,” akasema Bw Said.

Ni kauli ambayo ilipingwa vikali na aliyekuwa Mwakilishi wa Wadi ya Ganda Bw Abdulrahaman Omar aliyeshikilia kwamba sehemu hizo hazifai kufungwa kwa misingi kuwa zimekuwa za misaada kwa uchumi wa wakazi wa Malindi na Kilifi kwa ujumla.

Aliyekuwa Mwakilishi wa Wadi ya Ganda Bw Abdulrahaman Omar. PICHA | ALEX KALAMA

“Usalama kupatikana haimaanishi mangweni lazima kufungwa tafuteni njia ya kutatua shida ya ukosefu wa usalama, manake kuwa mangweni ndizo zinazochangia usalama kudorora hapa Malindi mimi hilo sikubaliani nalo. Kwa sababu mangweni zile ndizo tegemeo kubwa la jamii za sehemu hii katika kujipatia riziki ya kujikimu kimaisha na kulea familia zao, na mnazi sio haramu. Kwa hivyo tafuteni njia mbadala ya kutatua shida ya ukosefu wa usalama,” akasema Bw Omar.

Hata hivyo badala yake Bw Omar amesisitiza haja ya kunaswa kwa walanguzi wa mihadarati badala ya wauzaji wa mnazi.

“Dawa za kulevya ziko kila mahali… kila mwaka ni dawa za kulevya lakini mbona haziishi. Shikeni wale wenye kuuza ndio wale wanaovuta watakoma lakini acheni kusumbua wauzaji mnazi. Na hizi mangwe kuna vijana wamesoma ndani ya hii nchi kupitia mnazi au kuuza pombe. Kama kuna changamoto waangalie njia ya kusuluhisha lakini swala la kufunga mangwe hilo hatukubali manake hapa ndipo jamii inapata mkate wa siku,” alisisitiza Bw Omar.

  • Tags

You can share this post!

Madereva, vijana wagaragaza gozi uwanjani kupambana na...

Musalia ataka Ruto ashauriane na Museveni kuokoa Wakenya 41...

T L