• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Msaada wachelewa kuwafikia waathiriwa wa mafuriko Tana River

Msaada wachelewa kuwafikia waathiriwa wa mafuriko Tana River

NA STEPHEN ODUOR

WAKAZI wa kijiji cha Ziwani, Kaunti Ndogo ya Tana Kaskazini, wameililia serikali kwa kuwakejeli baada ya kukosa kupokea misaada waliyotumiwa wiki mbili zilizopita, baada ya kuathiriwa na mafuriko.

Wakazi hao, walitoa lalama zao huhuku maelfu wakiendelea kukabiliwa na athari hizo za mafuriko.

Wiki mbili zilizopita, malori 14 yaliyobeba misaada, ilitumwa na serikali ya kitaifa katika hafla ambayo iliongozwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Hata hivyo, kufikia sasa wakazi hao wanasema bado hawajapokea usaidizi huo na wamebaki kushangaa bidhaa hizo zilipelekwa wapi muda mfupi baada ya hafla hiyo.

Manusura wa mafuriko ambao wanaishi kwenye kambi za muda, wanahisi kuwa walikusanywa kwa ajili ya picha ili kujenga taswira kuwa walikuwa wamepokea msaada huo.

“Kwa muda tulicheza densi na tukadhani afueni imefika. Tuliambiwa kuwa chakula kitagawanywa baadaye lakini tangu wakati huo, tumezungushwa tu,” alisema Bi Fatuma Ali.

Juhudi zao za kutafuta vyakula hivyo hazijazaa matunda.

Bi Mariam Saladh, nyanya anayelea wajukuu wake sita, alisema kila ofisi ambayo wamekuwa wakiulizia kuhusu msaada huo imewatuma kwingine.

Mkuu wa Kambi ya Ziwani, Bw Abdalla Dulo, alisema kwamba ameacha kuulizia, kwani kila mmoja anaonekana kumkwepa.

“Nimeenda kila ofisi, wanaendelea kunituma huku na kule. Ilibidi nije kuwaambia watu wangu kwamba ni mbio zisizo na tija, tunakubali hatima yetu, lakini bado tunataka majibu,” alisema.

Kulingana na Bw Dulo, kambi mbalimbali ziliwakilishwa kwenye hafla ya kuzindua usambazaji wa chakula.

Alisema kuwa waliahidiwa kupokea msaada huo baadaye, lakini unachukua muda mrefu na wanakijiji wana mahitaji .

Kamishna wa Kaunti ya Tana River, Bw Mohammed Noor, hata hivyo alisema kuwa zoezi la usambazaji linaendelea.
Kulingana na Bw Noor, kambi hiyo itahudumiwa ndani ya mpango wa usambazaji.

“Zoezi hilo bado linaendelea, tumefika kambi chache na bado tunaendelea. Hakuna atakayeachwa. Kambi ya Ziwani pia iko katika mpango huo na vitu vyao vitaletwa hivi karibuni,” alisema Bw Noor.

Zaidi ya familia 35,000 zimeathiriwa na mafuriko hayo.

Wakati huo huo, Gavana wa Tana River, Bw Dhadho Godhana, tangu wakati huo amebatilisha likizo ya msimu huu wa sherehe kwa wafanyakazi wa kaunti, akisema kuwa juhudi zote zitahitajika ili kudhibiti athari za mafuriko.

“Hatuwezi kwenda kufanya sherehe wakati ndugu na dada zetu wanateseka kambini,” alisema.

Zaidi ya hayo, amelitaka bunge la kaunti kurejea kutoka mapumzikoni na kuidhinisha bajeti ya ziada ili kurahisisha mipango ya kuingilia kati.

Gavana huyo pia ametoa wito kwa wasamaria wema kuchangia misaada, akibainisha kuwa utawala tangu wakati huo umetumia zaidi ya nusu ya fedha za Hazina ya Kudhibiti Hatari za Maafa, lakini pengo hilo bado halijapungua.

  • Tags

You can share this post!

Mwanawe Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kusuluhisha kesi ya...

Madereva, vijana wagaragaza gozi uwanjani kupambana na...

T L