• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Mahakama yamuonya mzungu aliyedai wakuu serikalini ni wanachama wa ‘Illuminati’

Mahakama yamuonya mzungu aliyedai wakuu serikalini ni wanachama wa ‘Illuminati’

NA RICHARD MUNGUTI

MMISHENARI kutoka nchi ya Uholanzi aliyeshtakiwa kwa kupatikana nchini kinyume na sheria za uhamiaji ameonywa dhidi ya kuwatusi wakuu serikalini kwa kudai ni wanachama wa ‘Illuminati’.

Hakimu mkuu wa Mahakama ya Milimani Lucas Onyina alimwonya Christian Brons dhidi ya kuwadhihaki Rais Dkt William Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua.

“Nakuonya usithubutu kuwadhihaki wakuu wa nchi hii na pia hii mahakama kwa kudai tunashiriki ibada zisizoeleweka. Huna ukweli wowote kwamba wakuu wa nchi hii wanashiriki ibada za aina hiyo,” Bw Onyina alimuonya Brons aliyedai kortini ni Mmishenari na Pasta aliyefadhili miji ya watoto mayatima na maskini.

Aliomba aachiliwe huru na apewe Visa ya kuishi nchini badala ya kushtakiwa ikizingatiwa kwamba amekuwa akiwasaidia watoto maskini.

“Nchi hii inaongozwa na watu ambao ni wanachama wa Illuminati na Freemason. Hata wewe hakimu ni mmoja wao. Chukua tahadhari jinsi unavyoamua kesi hii inayonikabili. Ujue Illuminati na Freemason ndio walimsulubisha Yesu nyakati za makuhani ambao walikuwa viongozi,” alidai Brons, huku kiongozi wa mashtaka Anderson Gikunda na hakimu wakishtushwa na mkurupuko huo wa madai na maneno.

Brons alimweleza hakimu alikamatwa alipokuwa ameenda katika afisi za idara ya uhamiaji kuomba kibali cha Visa.

Brons alidai kortini maafisa wa idara ya uhamiaji walimwitisha hongo ndipo wamsaidie.

“Nimeshangaa badala ya kuhudumiwa niliitishwa hongo,” alidai Brons huku akiongeza: “Nchi hii iko na ushetani mwingi na tamaa ya pesa.”

Ilibidi hakimu amuulize maswali.

“Eti umesema wewe ni Mmishenari na Pasta?” Onyina alimuuliza Brons.

“Ndio,” mshtakiwa alijibu.

Onyina alimweleza: “Lakini ninataka ujue kwamba mapasta wengi wamejitokeza humu nchini na wamekuwa wakihubiri Injili ya kupotosha ambayo imesababisha watu wengi kuangamia. Hata sasa kuna madai kwamba Pasta Paul Mackenzie alifundisha itikadi kali zilizosababisha watu zaidi ya 200 kuangamia.”

Hakimu huyo alimtahadharisha dhidi ya kutoa matamshi asiyoweza kuthibitisha kisha akaamuru azuiliwe rumande ili ahojiwe na maafisa wa idara ya urekebishaji tabia watathmini ukweli wa madai yake kwamba ni Mmishenari.

Onyina alisema ataamua ikiwa mshtakiwa ataachiliwa kwa dhamana baada ya kupokea ripoti ya maafisa wa urekebishaji tabia.

Bw Onyina alimweleza mshtakiwa ikiwa anataka kuwasiliana na Ubalozi wa Uholanzi, atasaidiwa na idara ya urekebishaji tabia na polisi.

Brons alikabiliwa na shtaka la kukaidi sheria za uhamiaji kwa kukataa kujiandikisha kama mgeni.

Alikamatwa katika afisi za idara ya uhamiaji jengo la Nyayo mnamo Mei 18, 2023.

Mahakama iliagizwa mshtakiwa azuiliwe kwa muda wa wiki mbili.

  • Tags

You can share this post!

Uingereza kuwakilishwa na vikosi vinane kwenye soka ya bara...

Mwanamume akimbilia pasta baada ya mganga kumpa likizo ya...

T L