• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:19 PM
Wezi wa mali ya umma tutawatia adabu – Moi

Wezi wa mali ya umma tutawatia adabu – Moi

Na SAMMY WAWERU

KIONGOZI wa Kanu, Bw Gideon Moi amesema endapo muungano wa One Kenya Alliance (OKA) utatwaa serikali 2022 mojawapo ya ajenda zake itakuwa kufuatilia na kutwaa mali ya umma iliyoporwa.

Akitoa onyo Jumanne, seneta huyo ambaye ni kati ya vinara wa OKA alisema “muda wa matapeli wa mali ya umma umefika”.

“Wanaopora mali ya wananchi, wakati wao umewadia,” Bw Moi akasema, akihutubia umma kufuatia ziara ya OKA Kajiado.

“Mnajua tutakachowafanyia, tutamaliza ufisadi kabisa.”

Moi alikuwa ameandamana na vinara wenza, Kalonzo Musyoka wa Wiper na Moses Wetang’ula (Ford-Kenya).

Kiongozi wa ANC, Bw Musalia Mudavadi hata hivyo hakuhudhuria mkutano huo wa hadhara kupigia OKA upatu.

Muungano huo haujatangaza ni nani atakayepeperusha bendera yake kuwania urais.

Serikali tawala ya Jubilee, na ambayo inaongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, imetajwa kuwa fisadi zaidi katika historia ya Kenya.

Baadhi ya viongozi wakuu serikalini wamejipata kuandamwa na sakata za ufisadi, wengine wakiachishwa kazi na wengine kujiuzulu, ila hakuna aliyeadhibiwa kisheria licha ya kufunguliwa mashtaka mahakamani.

Idara ya Upelelezi wa Jinai na Uhalifu (DCI) na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), imechunguza na kukamata maafisa kadha wa serikali na ambao hata baada ya kushtakiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP), wameachiliwa kwa dhamana.

Kando na kupambana na mafisadi, OKA imeahidi elimu ya bure katika shule za upili za umma, iwapo itatwaa uongozi.

“Isitoshe, tutapunguza ushuru kwa asilimia 50,” akasema Bw Moi.

Licha ya mfumo wa masomo bila malipo katika shule za msingi za umma kuzinduliwa na Rais Mstaafu, Mwai Kibaki na kuendelezwa na Rais wa sasa Uhuru Kenyatta, wazazi hawajakwepa kulipa karo.

You can share this post!

Mahasla njaa Ruto akigawa mamilioni

Madai ya usimamizi mbaya, ubadhirifu FKF ni pigo kwa...

T L