• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Miaka 60 ya kujitawala imepotea bure, asema Raila akitaka vijana kukataa ‘udikteta’

Miaka 60 ya kujitawala imepotea bure, asema Raila akitaka vijana kukataa ‘udikteta’

Na CECIL ODONGO  

KIONGOZI wa upinzani Raila Odinga ameonya kuwa Kenya inaelekea pabaya na hana haina mengi ya kusherehekea tangu ijinyakulie uhuru mnamo 1963.

Bw Odinga alisema ni masikitiko kwamba baada ya  miaka 60 tangu nchi ijinyakulie uhuru, bado Kenya haijafanikiwa kupambana na umaskini, ujinga na magonjwa. Masuala hayo matatu ndiyo yalikuwa malengo makuu ya Kenya kutokomeza ilipojinyakulia uhuru.

Bw Odinga pia alishutumu serikali ya Rais William Ruto kutokana na kile alichosema ni kuanzisha sera hasi ambayo imewafanya Wakenya walimbikizwe mzigo mkubwa wa ushuru na kupandisha deni la taifa.

Kwa mujibu wa Bw Odinga, Wakenya wamepitia uchungu wa mkoloni, udikteta wa chama kimoja na kuporomoka kwa uchumi wa miaka ya 80 na 90.

Rais William Ruto anatarajiwa kuongoza maadhimisho ya miaka 60 tangu Kenya ijiondoe kwenye utawala dhalimu wa Uingereza,  mnamo Jumanne Desemba 12, 2023.

“Katika vipindi hivi, Wakenya wamepitia mengi. Familia zimesambaratishwa kupitia dhuluma na watu kuzuiliwa. Mahangaiko yamekuwa mengi ila Wakenya hawakukata tamaa,” akasema Bw Odinga.

Waziri huyo mkuu wa zamani ambaye amekuwa kwenye siasa za upinzani kwa miaka mingi aliwataka waendelee kusimama kidete na kupinga udikteta.

“Maadhimisho haya ya miaka 60 ni wakati mzuri wa kutafakari mahali ambapo tumetoka na pia tunakoelekea. Nchi hii itakuwa wapi tukiadhimisha miaka 120 ya uhuru mnamo 2083? Haya ni kati ya masuala ambayo tunastahili kufikiria,” akasema Bw Odinga.

Alikuwa akizungumza katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki ambapo alizungumzia demokrasia na safari ya Kenya tangu ijinyakulie uhuru. Aliandamana na mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi, Naibu Kiranja wa Wachache Mark Mwenje, Mbunge Mteule Irene Mayaka  na aliyekuwa Kiongozi wa Mungiki Maina Njenga pamoja na mbunge wa zamani wa Narok Kaskazini Moitalel Ole Kenta.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa ODM, Kenya inaweza kuinuka tena iwapo wananchi watamakinikia ndoto za wale waliopigania uhuru wa nchi.

“Tutakuwa na nchi ambayo viongozi watakuwa wakiwekeza nguvu zao katika kufadhili elimu na kujenga shule, kupambana na ufisadi, kubuni nafasi za ajira  na kwa ujumla kuwapunguzia Wakenya mzigo mzito wa kutimiza masuala ya kimsingi,” akasema.

Ingawa hivyo, alikiri kuwa Wakenya wamekosa imani na kila tawala baada ya uhuru na kwa sasa wamelimbikiziwa mzigo zaidi wa ushuru, ufisadi na uongozi usiojali maslahi yao.

Aliwataka wanasiasa chipukizi wasimame imara na kukataa udikteta pamoja na kusema hadharani iwapo taifa linaelekea pabaya.

Pia Bw Odingaa alishutumu serikali ya Kenya Kwanza akisema imejikita katika ukabila na unaendeleza ufisadi  huku wananchi wakiumia kutokana na gharama ya juu ya maisha.

“Leo watu wetu wanaendea kazi nje ya nchi kama Israeli na Saudi Arabia na Rais wetu anasema kuwa anasaka wakazi wa Wakenya nje ya nchi badala ya kubuni nafasi hizo hapa nchini,”

  • Tags

You can share this post!

Huzuni mgonjwa akifariki hospitali ikikataa kumhudumia

Kiwanda cha kwanza cha korosho Lamu

T L