• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:35 AM
Miguna atoa kauli nzito dhidi ya serikali iliyomsaidia kurejea nchini

Miguna atoa kauli nzito dhidi ya serikali iliyomsaidia kurejea nchini

NA CECIL ODONGO

NDOA kati ya utawala wa Kenya Kwanza na mwanaharakati Miguna Miguna imeanza kuingia doa, wakili huyo maarufu akikosoa Rais William Ruto kutokana na madhila mbalimbali yanayozonga nchi.

Bw Miguna ambaye alikuwa mfuasi sugu wa Kenya Kwanza na hata kuunga mkono azma ya Rais Ruto katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, ameonekana kuishiwa na subira kutokana na Wakenya kulimbikizwa ushuru, ufisadi miongoni mwa changamoto nyinginezo

Mnamo Jumatano, wakili huyo mkosoaji mkubwa wa Kinara wa Azimio Raila Odinga, alimkaba koo Rais mtandaoni, akisema katika uchaguzi mkuu wa 2027, Wakenya watakumbuka tu changamoto walizopitia kwenye utawala wa  Kenya Kwanza.

“Nawahakikishia kuwa mnamo 2027, Wakenya hawatamkumbuka ufasaha wa @WilliamsRuto, safari zake za ng’ambo wala suti za kaunda anazovaa. Watakumbuka tu njaa yao, umaskini, ukosefu wa ajira na ufisadi ambao unaendelea kupanda. Msiseme si kuwaonya,” akaandika Bw Miguna katika mtandao wake wa X (zamani twitter).

Rais Ruto amekuwa akikashifiwa kwa safari zake za ng’ambo ambazo sasa zimefikia 45 ya mwisho ikiwa ni ya Djibouti mnamo Disemba 9. Hata hivyo, Rais amekuwa akijitetea kuwa ziara hizo ni za kusaka kazi kwa Wakenya hasa katika milki ya kiarabu.

Bw Miguna anaonekana kuungana na Bw Odinga ambaye ameitaka serikali ibuni nafasi za ajira akisema kuwatafutia Wakenya kazi nje kunaonyesha serikali imeshindwa katika wajibu wake.

Juzi Bw Miguna, alishambulia Tume ya Maadili ya Kupambana na Ufisadi Nchini (EACC) kwa kushindwa kupigana na ufisadi. Bw Miguna alisema maafisa wa tume hiyo wanamakinikia kuwahangaisha polisi barabarani wanaochukua hongo za Sh20 ilhali kuna samaki wakubwa wanaopora pesa za umma.

“Rais @WilliamsRuto. Ufanisi wa uongozi wako utaamuliwa na iwapo ufisadi ukuwa chembechembe za DNA ya nchi wakati wa utawala wako,” akaandika kwenye mtandao wa X. Alikuwa akirejelea ufichuzi wa ripoti ya Mdhibiti wa Bajeti ulioonyesha kuwa baadhi ya magavana hawajatumia hata senti kwenye miradi ya maendeleo.

Mnamo Novemba 10, Bw Miguna alikosoa hatua ya  utawala wa Kenya Kwanza kuwaongezea Wakenya mzigo wa ushuru na kuitaka serikali pia iache kukopa kutoka kwa Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia.

“Serikali ya Kenya Kwanza haitabadilisha Kenya na kuimarisha hali ya maisha ya raia iwapo haitajiondoa kwenye minyororo ya IMF na Benki ya Dunia.

“Bila kujiondoa, matrilioni yanayokusanywa  kama ushuru na mikopo nchi inapewa, itaishia mikononi mwa viongozi wanaoshikilia afisi za umma wawe wamechagulia au kuteuliwa,” akaandika  Bw Miguna.

Kabla ya kuhamia mrengo wa Rais Ruto,  Bw Miguna alikuwa mshirika wa karibu wa kisiasa wa Bw Odinga na ni kati ya wale ambao walimwaapisha baada ya uchaguzi tata wa 2017.

Hata hivyo, alitofautiana na Raila baada ya waziri huyo mkuu wa zamani kuanzisha ushirikiano na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ambaye wakati huo alikuwa uongozini.

Uhasama wa Bw Miguna dhidi ya utawala wa Jubilee mnamo 2017 ulichangia kufurushwa kwake nchini mnamo Februari 7 2018 kisha Uhuru na Raila wakakubaliana kisiasa mnamo Machi 9, 2018.

Alirejea nchini mnamo Oktoba 20 baada ya kuwa Canada kwa siku 1687 na hata amewahi kufika ikulu kumsalimia Rais Ruto ambaye alimpigia debe sana kabla ya uchaguzi kufanyika.

Kwa mujibu wa mchanganuzi wa kisiasa Martin Andati, Bw Miguna anazidisha mashambulizid dhidi ya serikali kwa sababu hajapewa kazi jinsi alivyotarajia baada ya kupigia UDA debe 2022.

“Alikuwa amemwambia Rais ampe kazi lakini ni kama Rais amekataa. Miguna ni kichwa ngumu  na hawezi kuchukua maagizo kama kile anachoambiwa haiko katika Katiba. Alituma maombi ya kupata kazi ya DPP lakini akakosa kuorodheshwa na hilo linaonyesha alitemwa,” akasema Bw Andati.

“Sasa ameishiwa subira na pia serikali haiwezi kumfurusha tena kwa sababu ndiyo ilimresha. Pia hawezi kurudi mrengo wa Raila kwa sababu alishakosana nao vibaya. Ataendelea kupiga kelele ila sioni akipewa kazi ndani ya Kenya Kwanza,” akaongeza Bw Andati.

  • Tags

You can share this post!

El-Nino: Ukarabati wa barabara Gamba wagharimu Sh15 milioni

Utamu wa Lamu ni maisha ‘simple’ ya matajiri...

T L