• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Utamu wa Lamu ni maisha ‘simple’ ya matajiri kutembea miguu peku

Utamu wa Lamu ni maisha ‘simple’ ya matajiri kutembea miguu peku

NA KALUME KAZUNGU

MARA nyingi, mja amekuwa akikadiriwa hadhi yake au tabaka lake na wengi kulingana na kiwango au mwonekano wake, hasa  mavazi.

Utapata kwamba wengi huwachukulia watu waliovalia suti au makoti yaliyopigwa pasi iliyokoleza au kulainika vyema na pia kuvalia viatu vya ngozi nyeusi vilivyokoleza kiwi kuwa watu wenye hela au wa tabaka la juu.

Aghalabu utapata watu wanaotembea wakiwa miguu peku,wakivalia kaptura au kujifunga vikoi kiunoni ilhali wakikaa vivi hivi, iwe ni barabarani au vibarazani, wakichukuliwa kuwa wa hadhi ya chini,waliochanganyikiwa maishani na maskini.

Kwa kaunti ya Lamu aidha,unapowazingatia na  kuwakadiria watu hadhi zao kulingana na muonekano wao,iwe ni mavazi na vinginevyo huenda ukapotoka kimaamuzi.

Kwenye visiwa mbalimbali vya Lamu, maisha hapa ni ‘simple,’ iwe wewe ni mwenye ukwasi wa hela, mali au mchochole.

Kwa wanaoishi hapa watakuambia kuwa Utamu wa Lamu ni maisha ya kawaida,ambapo matajiri hapa hasa ndio wanaotembea wakiwa wamejifunga vikoi na kukanyaga ardhi wakiwa miguu peku kwa jina la mtaa ‘miguu chuma’ kwa kutembea bila viatu na ndara.

Mtu akitembea miguu peku, mtindo ambao hufahamika kama ‘miguu chuma’ kwa kutembea bila viatu na ndara. PICHA | MAKTABA

Utawapata matajiri hawa wakitangamana na kila mmoja,iwe ni wa tabaka la juu au lile la chini.

Ni hawa hawa wakwasi wa hela na rasilimali ambao mbali na kutembea nyayo wazi bila vitau, pia mara nyingi utawapata bila shati au fulana za kuziba miili yao.

Yaani ukimpata njiani utadhani huyu jamaa kweli ‘kachapa’ au kuchanganyikiwa.

Kuna wengine hata wamejipata wakiwatania matajiri hawa eti wawasaidie kununua viatu Na nguo nzuri kuwastiri.

Wasichokijua aidha ni kwamba wao wanaotaka kusaidia ndio wanaofaa kuuliza mabepari hao msaada kwani hela au mavazi kwao si shida.

Lakini je, tabia hii ilitoka wapi au chimbuko lake ni nini?

Bw Mbwana Titi, mmoja wa wazee kisiwani Lamu anasema wengi wa wadosi wa Lamu mara nyingi huishi maisha ya kawaida kutokana na kwamba wao wenyewe walizaliwa wakiwa maisha yao ni ya chini.

Kulingana na Bw Titi, ukichunguza maisha ya wakwasi hao utapata kwamba walikuwa vibarua waliohudumia wadosi wengine huku wakiwekeza polepole hadi pahali walipo.

“Hawa matajiri wa Lamu wengi walikuwa watumwa kwa mabwana zao. Walitumika kwelikweli lakini wakawa na maarifa ya kuwekeza hadi na wao wakawa matajiri  wa kuajiri wengine. Cha kufurahisha ni kwamba kwa sababu wamezoea maisha ya kutumikia,wao wamesalia na tabia hizo hizo za kuwa vibarua hadi katika maisha yao ya sasa ya utajiri,” akasema Bw Titi.

Naye Bw Mohamed Bakari, mzee wa kisiwa cha Pate, Lamu Mashariki, analinganisha maisha ‘simple’ ya matajiri wa Lamu na kazi wanazozifanya kuwapatia hela.

Tegemeo kubwa la jamii ya Lamu kujipatia mtaji ni uvuvi, ikizingatiwa kuwa karibu asilimia 80 ya mapato Na uchumi wa Lamu hutokana na uvuvi.

Kulingana na Bw Omar, mvuvi hawezi kuvalia suti au koti anapoelekea baharini kinyume na matajiri ambao kazi zao ni za ofisini.

Licha ya wavuvi kujizolea mamilioni kila wakati wanapotekeleza kazi yao baharini,wao utawapata wakivalia kaptura au kujifunga vikoi ili kuwawezesha kufanya uvuvi vyema.

“Mahali kama Pate ama Kizingitini kuna Hela si haba. Utapata muungano wa wavuvi ukivuna Karibu Sh5 milioni kila mwezi au baada ya miezi miwili,yote yakitokana na uuzaji wa samaki aina aina. Nyumba nyingi hapa watu ni matajiri ila ukiwatazama kimuonekano utawaona ni fukara kabisa. Ujue huwezi kwenda baharini kuvua ukiwa umefunga tai. Ukitoka baharini ni kuoga na kuvalia kikoi kubarizi ukisubiri mida ifike kuchomoka tena kuingia baharini. Hayo ndiyo maisha yetu na tumeyakubali,” akasema Bw Omar.

Wavuvi Lamu wakitoa nyavu katika Bahari Hindi mnamo Mei 14, 2020. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bi Fatma Hassan, mkazi wa mji wa kale wa Lamu, analinganisha maisha ya kawaida wanayoishi wadosi wa Lamu na mila na desturi za eneo hilo.

Lamu ni ngome ya jamii ya Waswahili wa asili ya Wabajuni ambao dini yao ni ya Kiislamu.

“Hapa tunaishi Maisha ya kawaida kulingana Na vile tumekuzaa tangu jadi. Utamaduni wa hapa ni kwamba kila mmoja a heshimu mwenzake, iwe ni kwamba una mali au ni fukara. Hakuna ubaguzi wa kitabaka hapa. Ndiyo sababu maskini kwa matajiri tunatangamana bila kusutana,” akasema Bi Hassan.

  • Tags

You can share this post!

Miguna atoa kauli nzito dhidi ya serikali iliyomsaidia...

Msongamano mkubwa wa magari Wakenya wakielekea...

T L