• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 4:32 PM
El-Nino: Ukarabati wa barabara Gamba wagharimu Sh15 milioni

El-Nino: Ukarabati wa barabara Gamba wagharimu Sh15 milioni

NA KALUME KAZUNGU

ZAIDI ya Sh15 milioni zimetumika kutekeleza ukarabati wa sehemu ya barabara iliyokatwa na maji ya mafuriko eneo la Gamba majuma matatu yaliyopita.

Kampuni ya Equistar Limited ndiyo iliyokuwa imekabidhiwa zabuni ya kutekeleza ukarabati huo Wa eneo la Gamba.

Ilipewa kandarasi hiyo na Mamlaka ya Ujenzi na Usimamizi wa Barabara kuu Nchini (KeNHA).

Katika mahojiano na Taifa Leo muda mfupi baada ya kukamilisha ukarabati huo na kuruhusu magari kupita, Mkurugenzi wa Equistar Limited Bw Fahim A. Ahmed, alisema karibu kilomita tatu za barabara eneo hilo la Gamba zilikuwa zimeharibiwa na mafuriko.

Bw Fahim alisema waliafikia kujaza mawe,mchanga na kokoto kwenye sehemu nne za Gamba ambapo mafuriko yalikuwa yameikata barabara na kuigeuza mto uliokuwa ukipitisha maji mengi,hivyo kusambaratisha kabisa usafiri kwenye barabara hiyo.

Alitaja baadhi ya changamoto walizopitia wakati wakiendeleza mradi huo, ikiwemo kusafirisha vifaa vya ujenzi,hasa mawe kutoka sehemu za mbali zilizoko nje ya kaunti za Lamu na Tana River, ikiwemo Kilifi na Mombasa.

“Twashukuru kwamba leo tumekamilisha ukarabati Wa eneo hili la Gamba japo kwa muda tu. Ni kazi inayohitaji fedha nyingi ili iwe ya kudumu. Tumejaza sehemu zote nne zilizokuwa zimekatwa na mafuriko hapa Gamba. Tayari magari yameanza kupita. Hali ni shwari kwa sasa,” akasema Bw Fahim.

Afisa huyo aliongeza, “Ili kuukamilisha ukarabati huu haraka ilivyotakikana,tuliamua kujikaza na kufanya kazi masaa 24 kila siku bila kupumzika. Ni changamoto kubeba mawe,mchanga,kokoto na vifaa vingine kutoka mbali kama vile Kilifi na Mombasa ilmradi tuvitumie hapa Lamu kutekeleza ukarabati uliohitajika. Hilo halikutuogopesha na twashukuru tumekamilisha kazi.”

Miongoni mwa watu wa kwanza kutumia eneo la Gamba kuvuka baada ya kukarabatiwa ni Gavana wa Lamu Issa Timamy aliyesifu serikali, KeNHA na mwanakandarasi kwa jitihada zao kurejesha hali ya kawaida, hasa usafiri wa barabara uliokuwa umekatizwa kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita.

“Nimefurahia jitihada ya serikali, KeNHA na mwanakandarasi kuona kwamba usafiri kwenye barabara yetu kuu unarejelewa. Nilikuwa na wasiwasi wa jinsi watu wetu wangeendelea na maisha Lamu bila kuwepo kwa usafiri wa barabara. Nimefurahi kwamba ukarabati umetekelezwa vyema na tayari magari yameanza kuvuka Gamba. Hiyo ni dalili njema,” akasema Bw Timamy.

Baadhi ya wamiliki wa magari ya usafiri wa umma na wakazi pia walisifu hatua ya kuipa kampuni ya Equistar kandarasi hiyo.

Bw Emmanuel Wanyoike Kimwa aliisihi serikali kuzipa kipaumbele kampuni za nyumbani kazi za ujenzi wa miradi ya serikali.

“Nafurahia kusikia kuwa kampuni ya Equistar ni ya papa hapa. Ni jambo jema ikiwa kampuni za nyumbani zitapewa kandarasi kutekeleza miradi ya serikali kwani huwa zinatekeleza kazi kwa nia safi na kwa haraka kama vile Equistar Limited ilivyokarabati Gamba,” akasema Bw Kimwa.

Bw Said Swaleh, mmoja wa makondakta wa mabasi ya usafiri wa umma yanayohudumia barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen,alitaja kurejelewa kwa usafiri barabarani kuwa mwanzo mpya kwao.

“Hata sisi watoaji huduma za mabasi ya usafiri wa umma tumeumia. Biashara ilikosekana kipindi chote cha majuma mawili ya mafuriko. Kukarabatiwa kwa Gamba ni kumaanisha biashara ya usafiri imerejea sasa. Twashukuru angalau familia zetu zitapata riziki,” akasema Bw Swaleh.

Barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen ndicho kiunganishi cha pekee cha Lamu na maeneo mengine ya Kenya,hasa kwa wale wanaotumia usafiri wa nchi kavu.

Lori la trela likipita katika sehemu mojawapo ya eneo la Gamba iliyokarabatiwa na kampuni ya Equistar Limited kwa kima cha Sh15 milioni, hivyo kuruhusu kurejelewa kwa usafiri kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen. PICHA | KALUME KAZUNGU
  • Tags

You can share this post!

Mjane amtaka Kindiki kumtafuta bintiye aliyetoweka kwa deti

Miguna atoa kauli nzito dhidi ya serikali iliyomsaidia...

T L