• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
Worldcoin iliingiza Sh2.5 bilioni nchini bila ufahamu wa CBK, kamati yaambiwa

Worldcoin iliingiza Sh2.5 bilioni nchini bila ufahamu wa CBK, kamati yaambiwa

NA CHARLES WASONGA

JUMLA ya Sh2.5 bilioni ziliingizwa nchini na kutolewa na Wakenya ambao walijitokeza mwezi Agosti 2023 ili kupeana data zao kwa kampuni ya Worldcoin.

Walitoa pesa hizo kupitia huduma mojawapo ya kutuma na kupokea pesa kwa simu.

Gavana wa Benki Kuu ya Kenya (CBK) Dkt Kamau Thugge mapema wiki hii aliwaambia wabunge wanaochunguza shughuli za kampuni hiyo, ya asili ya Amerika, kwamba Hazina ya Kitaifa au maafisa wa usalama hawakutambua kitendo hicho cha upitishwaji fedha.

Dkt Thugge aliambia Kamati ya muda inayochunguza sakata hiyo kwamba CBK haikushiriki katika utoaji leseni na uidhinishaji wa wamiliki wa Worldcoin.

Dkt Thugge pia aliiambia kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Narok Magharibi kwamba CBK haikufahamu chochote kuhusu shughuli za Worldcoin nchini.

Alisema benki haikugundua kuwa kampuni hiyo ilipitisha Sh2.5 bilioni kupitia huduma hiyo ya kutuma na kupokea pesa kwa simu.

“Huduma hiyo ya kutuma na kupokea pesa hupitisha mabilioni ya pesa kwa siku moja. Kwa hivyo, itakuwa vigumu kutambua asili ya pesa zote zinazopitishwa kupitia jukwaa hilo,” Dkt Thugge akaiambia kamati hiyo.

Gavana huyo alisema kile kinachopaswa kufanyika ili kudhibiti biashara ya sarafu za kidijitali maarufu kama “cryptocurrencies” ni kutungwa kwa sheria thabiti za kusimamia sekta hiyo.

Wiki jana maafisa wakuu wa Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Uhalifu wa Kimatandao (NC4) waliambia kamati hiyo kwamba hadi kufikia wakati wa kusitishwa kwa shughuli za Worldcoin mnamo Agosti 8, 2023, jumla ya Wakenya 350,000 walikuwa wamejitokeza kujisajili na Worldcoin ili mboni za macho yao zimulikwe.

  • Tags

You can share this post!

Maumivu Tanzania bei ya mafuta ikipaa na kupita ya Kenya

‘Mizimu’ ya Shakahola yaandama mochari na...

T L