• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Mkurugenzi wa kampuni ya ukopeshaji pesa Kilifi ashtakiwa kwa kuwatapeli wateja wake

Mkurugenzi wa kampuni ya ukopeshaji pesa Kilifi ashtakiwa kwa kuwatapeli wateja wake

NA MAUREEN ONGALA

MKUREGENZI mkuu wa Shirika la kupeana mikopo la Chembe Merchants Limited amefikishwa mahakamani Kilifi kwa kosa la kuwatapeli wateja maelfu ya pesa kwa kudai kuwa angewapa mikopo.

Maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI) walimtia mbaroni Bw Ahmed Ali Bahatisha mnamo Jumamosi, Desemba 16, 2023, ambapo walifunga ofisi yake mjini Kilifi.

Alikabiliwa na makosa sita mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kilifi Bw Daniel Sitati na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho au Sh300,000 pesa taslimu.

Miongoni mwa makosa hayo kulikuwa na njama ya kuwaibia wateja wake na kupokea pesa kwa njia ya udanganyifu.

Kampuni hiyo ya Chembe Merchants imekuwa ikiendeleza shughuli zake za kupeana mikopo katika ofisi zao zinazopatikana katika soko la Oloitiptip mjini Kilifi.

Mbali na kupeana mikopo ya pesa, kampuni hiyo pia hudai kuwasaidia wateja wake kununua na kumiliki magari na mali nyingine.

Mmoja wa waathiriwa ni Bw Stephen Chiriba ambaye alitapeliwa Sh170,000 kati ya Agosti 26 na Oktoba 2, 2023, kwa mujibu wa nakala ya mashtaka.

Waathiriwa wengine ni Bw Ellon Baya na Joyshine Wairimu ambao walitapeliwa Sh47,000.

Kulingana na mashtaka kortini, Bw Bahatisha alitekeleza uhalifu huo pamoja na wenzake ambao hawakufikishwa mahakamani.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya kupeana mikopo ya Chembe Merchants Limited ya mjini Kilifi Bw Ahmed Ali Bahatisha akiwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kilifi Daniel Sitati mnamo Jumatatu, Desemba 18, 2023. PICHA | MAUREEN ONGALA

Kiongozi wa mshtaka alieleza mahakama  kuwa kando na walalamishi katika kesi iliyowasilishwa kotini zaidi ya watu 50 walikuwa wamejitokeza kulalamikia kutapeliwa na mshtakiwa.

Kiongozi wa mashtaka alieleza mahakama kuwa mafisa wa polisi bado walikuwa wanendeleza uchunguzi  na ingekuwa bora iwapo angesalia gerezani.

Maafisa wa upelelezi wanataka kubainisha iwapo mshtakiwa alikuwa anaendeleza biashara yake kihalali na alikuwa amejisajili na kisheria kukopesha na kupokea pesa kutoka kwa umma.

Hata hivyo, hakimu Sitati alipinga ombi la kiongozi wa mashtaka kumnyima dhamana mshtakiwa na kusema ya kwamba hakutoa sababu za kutosha kuunga mkono ombi lake.

“Ni lazima kiongozi wa mashtaka athibitishe ya kuwa mshukiwa atatoroka na pia ataharibu uchunguzi unaondelea na kulingana na kiapo cha afisa anayechunguza kesi hii swala hili hali halijapewa sababu za kutosha,” akasema Bw Sitati.

Inadaiwa mkurugenzi huyo aliwalaghai wateja wake takriban zaidi ya Sh650 milioni.

Kesi hiyo itasikilizwa mnano Machi 25, 2024, baada ya kuwa imetajwa Januari 8, 2024.

Mkurugunzi huyo alijitetea na kueleza mahakama kuwa yeye ni kati ya wale ambao wana idhini ya kusimamia maswala ya fedha katika kampuni hiyo ambayo iko katika miji mbalimbali nchini na hatua ya kumnyima dhamana ingeleta changamoto kubwa sana.

Alisema maafisa wa polisi walifunga ofisi yake na kuondoka na vifaa vya kazi na stakabadhi muhimu na wafanyakazi wake hawajui la kufanya kwa sasa.

Baada ya habari ya kukamatwa kwa mkurugenzi huo kuenea, watu wengi walijitokeza katika afisi za DCI Kilifi kulalamikia kutapeliwa.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

David Mugonyi ateuliwa Mkurugenzi Mkuu wa CA kujaza nafasi...

Waislamu mjini Eldoret walaani hatua ya Papa...

T L