• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Waislamu mjini Eldoret walaani hatua ya Papa Francis kukubali wapenzi wa jinsia moja kubarikiwa

Waislamu mjini Eldoret walaani hatua ya Papa Francis kukubali wapenzi wa jinsia moja kubarikiwa

NA TITUS OMINDE

AKINA mama Waislamu na viongozi wa dini hiyo kutoka North Rift wameghadhabishwa na hatua ya kiongozi Kiongozi wa Kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis kukubali wapenzi wa jinsia moja kubarikiwa na viongozi wa kidini.

Wakihutubu wakati wa kufuzu kwa watoto katika Madras ya Maili Nne mjini Eldoret viongozi hao walisema matamshi ya Papa Francis yanadunisha sio dini tu bali maadili ya Kiafrika.

Bi Halima Mohammed ambaye alikuwa miongoni mwa wazazi ambao watoto wao walifuzu katika shule hiyo ya Madrassa, alisema hatua ya uongozi wa Kanisa Katoliki ni ya aibu kwa watoto.

Bi Mohammed alisema hiyo ni kero inayoweza hata kusababisha migogoro ya kidini.

“Sisi kama Waafrika kwa kila hali tunapinga hatua ya Papa kutaka mashoga wabarikiwe kanisani, matamshi hayo ni aibu hasa kwa watoto wetu. Ndoa ya jinsia moja iliharamishwa hata katika Biblia wakati wa Sodoma na Gomora,” alisema Bi Mohammed.

Bi Mohammed aliwataka wazazi kuwa macho kwa kufundisha watoto wao maadili mema katika jamii ili kukabiliana na uovu ambao unazidi kuongezeka duniani.

Alitishia kuwa huenda wanawake wakalazimika kufika mahakamani kutaka dini ya katoliki nchini kufafanua kuhusu pendekezo la Papa Francis.

Msimamo sawa ulitolewa na mwenyekiti wa baraza la wahubiri na Maimam (CIPK) Sheikh Abubakar Bini ambaye alikosoa matamshi hayo kwa kusema kuwa angalau Papa Francis angewataka viongozi wa dini kuombea mashoga na LGBTQ kuokoka na kubadilisha maisha yao.

“Matamshi ya Papa Francis yanaenda kinyume na Biblia na Qur’an. Matamshi hayo ni sawa na kuhalalisha usagaji na tabia za wanachama wa LGBTQ kwa jamla.Maaskofu wa Kiafrika wasikubaliane na wito huo kamwe.Lau Papa Francis angewataka maaskofu wa katoliki kuombea mashoga wabadilishe maisha badala ya kusema wabarikiwe Mungu habariki ndoa ya watu wa jinsia moja,” alisema Sheikh Bini.

Mwenyekiti wa CIPK North Rift Abubakar Bini akiwahutubia wanahabari mjini Eldoret mnamo Desemba 15, 2023. PICHA | TITUS OMINDE

Sheikh Bini alisema matamshi hayo yanahatarisha dini ya Kikristo ambapo huenda waumini wakalazimika kuachana na kanisa na kuanza kudumisha mila za tangu jadi badala ya kwenda kanisani.

“Iwapo kanisa litaendele kukosa msimamo huenda waumini wakalazimika kufunga makanisa na kurudia mila n aidikadi za Mwafrika ambazo haziruhusu ndoa ya jinsi moja,” aliongeza Sheikh Bini

Naye mwalimu wa mswala ya dini ya Kiislam Mubashr Idris alisema dini ya Kiislam haitayumbishwa na matamshi kama hayo huku akitoa mwaliko kwa wakristo kujiunga na dini hiyo kwa mafunzo bora yenye maadili badala ya kupewa ushauri wa kubariki mashoga.

Bw Idris alitaka wazazi kuendelea kufundisha watoto wao maadili mema kupitia mwongozo wa Qur’an na Biblia badala ya kuiga mila na desturi za kigeni.

“Tushirikiane na walimu wa kidini kufundisha watoto wetu maadili mema badala ya kukubali mafundisho ambayo yanaunga mkono ushoga,” alisema Idris.

Kwa pamoja, viongozi hao wanataka maaskofu wa humu nchini kutoa msimamo wao kuhusiana na matamshi ya Papa Francis.

  • Tags

You can share this post!

Mkurugenzi wa kampuni ya ukopeshaji pesa Kilifi ashtakiwa...

Mwalimu asakwa akidaiwa kuwaua kwa kuwachinja wanawe wawili

T L