• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 5:04 PM
Mwanafunzi wa Moi Girls afungwa jela miaka 5 kwa kuua wenzake

Mwanafunzi wa Moi Girls afungwa jela miaka 5 kwa kuua wenzake

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA mwanafunzi wa shule ya upili ya Moi Girls , Nairobi Alhamisi alihukumiwa kifungo cha miaka mitano kwa kuchoma bweni ambapo wasichana 10 waliangamia.

Huku Jaji Stellah Mutuku akiendelea kusoma hukumu, msichana huyo aliye na umri wa miaka 18 alianza kulia huku wazazi wa wahanga wa moto huo nao wakilia. Kilio kilipasua anga pale Jaji Mutuku aliposema “mshtakiwa ataishi milele na kovu aliloweka mioyoni mwa wazazi na watu wa familia za wahasiriwa wa moto huo.”

“Hii mahakama ilimpata na hatia mshtakiwa ya kusababisha bila kukusudia vifo vya wanafunzi wenzake. Wazazi na watu wa familia za watoto hao ambao waliokufa kutokana na mkasa huo wataishi na kovu la kupoteza wapendwa wao. Hakuna anayejua wahasiriwa wangelikuwa watu wa aina gani maishani,”alisema Jaji Mutuku aliyesoma uamuzi huo kwa njia ya mtandao kutoka Mahakama Kuu ya Kajiado.

Mshtakiwa alifikishwa katika Mahakama Kuu Milimani Nairobi kutoka gereza la Langata anakozuiliwa na ambapo ataanza kutumikia kifungo cha miaka mitano kwa kila msichana aliyekufa. Kwa jumla atatumikia kifungo cha miaka 50.

“Nimetilia maanani mawasilisho ya wazazi wa wahasiriwa pamoja na ripoti ya afisa wa urekebishaji tabia kwamba uadhibiwe kwa kifungo cha gerezani ijapokuwa umejutia matendo yako,”Jaji Mutuku alisema akipitisha hukumu. Mahakama ilisema iko katika njia panda kuhusu adhabu itakayopitisha dhidi ya mshtakiwa kwa vile alitekeleza uhalifu huo akiwa na umri wa miaka 14 na sasa ametimisha 18 akiwa gerezani.

Florence Agoswa mzazi wa mmoja wa wahanga wa mkasa wa moto katika shule ya upili ya Moi Girls Nairobi 2017…Picha/ RICHARD MUNGUTI

“Hii mahakama iko katika njia panda kwa vile sheria imenyamaza kimya kuhusu adhabu mkosaji anayeshtakiwa akiwa mtoto na kutumisha umri wa utu uzima akiwa kizuizini,” alisema Jaji Mutuku. Jaji huyo alisema atatumia Sheria nambari 191 (1) (l) ya Sheria za Watoto ambapo mmoja akikosa anaadhibiwa kwa uhalifu aliotenda.

Jaji huyo alisema makosa aliyofanya mshtakiwa yalishtusha kila mmoja nchini Kenya na “kufikia sasa baadhi ya wazazi hawakuamini majivu ya watoto wao waliyoonyeshwa.”NAlisema kwa kila shtaka ya mauji yakiwa 10 atamuhukumu kifungo cha miaka mitano. Vifungo vyote vitatumika kwa wakati mmoja.

Baada ya hukumu kupitishwa kiongozi wa mashtaka Wangui Gichuhi aliwaeleza wazazi wa wahasiriwa jinsi Jaji Mutuku amepitisha na kuwaambia “haki imetendeka.” Lakini punde tu baada ya Bi Gichuhi kuwaacha wazazi hao walivalia T-Shati zenye maadishi “Haki kwa Watoto wetu.”

Wazazi hao waliangua vilio huku wakisema “walitarajia adhabu kali kuliko hiyo iwe funzo kwa watoto wengine wanaoteketeza shule na mabweni.” Jaji Mutuku alimpa siku 14 kukata rufaa. Baada ya uamuzi huo kusomwa baadhi ya wazazi walizirai kortini hata ikabidi wapepetewe hewa. Wazazi walilalamika kifungo cha miaka mitano ni kidogo sana.

Walieleza Taifa Leo walitarajia mshtakiwa aadhibiwe vikali. “Tulitazamia mshtakiwa aadhibiwe kifungo kikali iwe funzo kwa wanafunzi wengine walio na tabia ya kuteketeza majengo ya shule moto,” alisema Mzee William Ogolla ambaye mjukuu wake aliangamia mle.

Baadhi ya wazazi wa shule ya Moi Girls ambao watoto walichomeka hadi wakafa…Picha/RICHARD MUNGUTI

You can share this post!

Washauri wa Uhuru watajwa kuchangia umaarufu wa Ruto

Mahakama yaambiwa Omwenga aliuawa baada ya kuandaa karamu

T L