• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 5:56 PM
Washauri wa Uhuru watajwa kuchangia umaarufu wa Ruto

Washauri wa Uhuru watajwa kuchangia umaarufu wa Ruto

NA MWANGI MUIRURI

WANDANI wa Rais Uhuru Kenyatta wamelaumiwa kwa kuchangia kudidimia kwa umaarufu na ushawishi wake katika eneo la Mlima Kenya.

Mchanganuzi wa siasa, Prof Ngugi Njoroge anasema viongozi walio karibu na rais wamekuwa wakisukuma ajenda zao za kibinafsi bila kujali maslahi ya wananchi wa kawaida, hali anayotaja kama kiini cha wengi kuwa na hisia kali dhidi ya rais.

Mdadisi Herman Manyora naye anasema, Rais Kenyatta alichangia umaarufu wa Dkt Ruto eneo la Mlima Kenya alipomtaja kama mrithi wake walipokuwa wakifanya kampeni za 2013 na 2017.

“Wengi wa wakazi wa Mlima Kenya wanahisi Uhuru aliwasaliti kwa kumkumbatia kinara wa ODM Raila Odinga ilhali katika chaguzi za 2013 na 2017, kampeni zake zilikuwa ni kumpiga vita kinara huyo wa ODM,” aeleza Bw Manyora.

Wakazi pia wanahisi kwamba iwapo sio kwa mchango wa Dkt Ruto, Jubilee haingeshinda chaguzi hizo, na hivyo ingekuwa bora kumrudishia mkono wa shukrani kwa kumuunga mkono mwaka huu.

Wakazi wengi waliohojiwa na Taifa Leo wanasema Rais Kenyatta amewapuuza tangu 2018, ndiposa amefanya ziara chache sana eneo hilo kipindi chake cha pili.

“Kila mara tunamsikia yuko Kisumu, Mombasa na sijui wapi! Huku kwetu sijui alikuja mara ya mwisho lini, na kila anapokuja amekuwa akitusuta tu. Kwa vile uchaguzi umekaribia ametambua anatuhitaji. Afahamu kuwa mambo mwaka huu ni tofauti na 2017,” akasema Njuguna Kimari, mkazi wa Murang’a.

Kauli ya Bw Njuguna ilidhihirika katika chaguzi ndogo za ubunge na udiwani Kiambu, Nyandarua, Murang’a, Meru na Nakuru ambapo wagombeaji wa Jubilee waliangushwa na wale wa Dkt Ruto.

Aliyekuwa mkuu wa mkoa kwa muda mrefu, Joseph Kaguthi anawalaumu washauri wa Rais Kenyatta akisema ndio walileta ‘uadui’ uliopo kati yake na wakazi wa Mlima Kenya.

Lakini msomi Prof Peter Kagwanja anasema wandani wa Dkt Ruto wanatumia changamoto za kiuchumi zinazokabili wenyeji kumharibia sifa rais wakisema ameshindwa kuwasaidia.

Anasema Dkt Ruto ndiye wa kulaumiwa kwa kukosa kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya rais.

Mwanasiasa Irungu Nyakera anakubaliana na Prof Kagwanja akisema Rais Kenyatta ametekeleza mengi kuinua hali ya uchumi ya wakazi hasa katika kilimo cha mchele, chai, kahawa na maziwa, lakini mrengo wa Dkt Ruto unaeneza propaganda kuwa amewapuuza wakazi.

You can share this post!

Magoha aonya wakuu wa shule kuhusu karo

Mwanafunzi wa Moi Girls afungwa jela miaka 5 kwa kuua...

T L