• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Mwanamume na wakwe wazozania maiti, mochari yasubiri mkwamo wa mahari utatuliwe

Mwanamume na wakwe wazozania maiti, mochari yasubiri mkwamo wa mahari utatuliwe

NA STANLEY NGOTHO

KIZAAZAA kimeshuhudiwa Ijumaa asubuhi kwenye mochari ya Hospitali ya Kitengela, eneobunge la Kajiado Mashariki, ‘mume’ wa marehemu alipozuia wakwe kuchukua mwili wa mwendazake.

Wazazi wa marehemu Agatha Khasandi Kulabi,47, aliyefariki mnamo Agosti 20, 2023, walikuwa wamewasili hapo kuchukua mwili wake kuenda kuuzika nyumbani Kakamega kwa sababu mwanamume aliyekuwa akiishi naye hakuwa amelipa mahari.

Mwanamume huyo, Bw Nicholas Muranda,  alikuwa akiishi na marehemu kama mume na mke na ingawa alikuwa na shughuli Lamu, alikuwa akimtembelea mwanamke huyo aliyekuwa akiishi Mlolongo akifanya kazi za nyumba. Walijaliwa mtoto mmoja. Ingawa hivyo, marehemu alikuwa na watoto wengine watatu aliowapata kabla ya kukutana na mwanamume huyo.

Mwanamume huyo aliwasilisha barua ya wakili wake kuzuia mochari kuruhusu familia hiyo kutoka Kakamega kuuchukua mwili hadi swala la mahari litakapotatuliwa. Taifa Leo imeona barua hiyo.

Hata hivyo, Bw Muranda hakuwa hapo mochari na tulipompigia simu hakupokea.

Mamake marehemu, Bi Pamela Mbone,70, aliyekuwa amesafiri kutoka Kakamega kuuchukua mwili wa binti yake wa upili tayari kwa mazishi ambayo yalifaa kufanyika kesho Jumamosi, ameambia Taifa Leo kwamba ‘mume’ hakuwa amelipa mahari ndipo aruhusiwe kumzika marehemu.

“Binti yangu angalau alikuwa na wanaume watatu kwa nyakati tofauti na hakuna hata mmoja aliyelipa mahari licha ya yeye kuwazalia watoto. Hii ndiyo sababu familia imeamua azikwe nyumbani kwa babake katika Kaunti ya Kakamega,” amesema.

Ameongeza kwamba ‘mume’ huyo amekuwa akiwazungusha kwa siku tatu na kuleta mvutano ulioishia kwa kituo cha polisi cha Kitengela kwamba watoto wakubwa wa marehemu walikuwa wamemhangaisha.

Inadaiwa kwamba ‘mume’ huyo wa marehemu alipigwa na upande wa wakwe wake katika nyumba ya Mlolongo mnamo Alhamisi jioni.

“Alikuwa amepanga kuja kijijini kulipa mahari lakini akaghairi nia. Pia alikataa kununua jeneza au kuvalisha maiti,” mama huyo ameelezea.

Naye Bw Godfrey Okwiri, mwanawe marehemu, ameambia Taifa Leo kwamba mgogoro huo unafanya mamake hawezi akapata mazishi ya heshima baada ya tarehe ya kwanza kuahirishwa kwa sababu hiyo ya mvutano.

“Babangu wa kambo hatendi haki. Tulikuwa tumeweka mipango yote tayari na tukapata stakabadhi zinazohitajika ili kumzika mamangu,” amesema akitokwa na machozi.

Familia hiyo imesema itaendelea kupambana hadi ipate haki.

Nao usimamizi wa mochari ya hospitali ya Kitengela umezitaka pande mbili zimalize mvutano huo wa mahari kabla ya kuruhusiwa kuondoa mwili.

  • Tags

You can share this post!

Gachagua aendelea kushambulia majadiliano, ataka...

Nataka nidhamu ya juu, Raila atetea kutimuliwa kwa waasi ODM

T L